Risasi zatembea uchaguzi wa mitaa

  Vurugu zatanda, karatasi za kura zakosekana
Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Kigagila, jijini Dar es Salaam, wakizozana na mmoja wa maafisa wa uchaguzi kata ya Kiwalani, kufuatia tangazo la kuahirishwa kwa uchaguzi kutokana na dosari zilizoibuka wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa katika eneo hilo jana. Picha na Oma Fungo
Chaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji uliofanyika nchini kote jana, ulitawaliwa na kasoro na vurugu kubwa zilizosababisha polisi kutumia risasi za moto na baadhi ya wapigakura kuchapana makonde, jijini Dar es Salaam.
Vurugu hizo zilitokana na uchaguzi huo kugubikwa na kasoro nyingi na hivyo kusababisha baadhi ya vituo kulazimika kuahirisha uchaguzi hadi wiki ijayo.

Baadhi ya kasoro zilizozua vurugu hizo, zilitokana na baadhi ya vituo kuchanganya majina ya wagombea, kuchelewa kuanza kwa uchaguzi, kukosekana kwa vifaa vya kupigia kura pamoja na baadhi ya wagombea kuwahujumu wengine.
Uchaguzi huo ulipangwa kuanza saa 2.00 asubuhi, lakini katika maeneo mengi ulichelewa kuanza kutokana na vifaa kuchelewa kufika vituoni.
Pamoja na mwitiko mkubwa wa wananchi waliojitokeza mapema katika vituo vya kupigia kura, baadhi ya vituo vilichelewa kufunguliwa na hata baada ya kufunguliwa zoezi hilo lilichelewa kuanza.

Katika kituo cha Matembele ya Kivule, wananchi walifika majira ya saa 1.00 asubuhi, lakini mawakala na wasimamizi wa uchaguzi hawakuwapo mpaka saa 5.00 asubuhi.

Baada ya kufika katika kituo cha uchaguzi, uchaguzi ulishindwa kuanza kufanyika kutokana na masanduku ya kupigia kura na wino kuchelewa kufika na hivyo, kusababisha zoezi hilo kuanza saa 6.00 mchana.
Katika kata ya Chamanzi-Mbagala, katika vituo vya Saku A, Saku B na Mzambarauni, karatasi za kura na wino havikuwapo, hali iliyosababisha zoezi hilo kuchelewa kuanza hadi saa 7: 00 mchana.

Kasoro nyingine zilizojitokeza ni pamoja na kuchanganya wagombea kulikosababisha baadhi ya wagombea wa Chadema kukutwa katika orodha ya wagombea wa CCM na wale wa CCM kukutwa katika orodha ya wagombea wa Chadema.

Baadhi ya vituo vilivyoahirisha uchaguzi, ni Luanga, Siimbwa, vilivyopo Tabata Kimanga, Machimbo, Misewe, Mfaume na Tembo Vigwaza.

Katika kituo cha Kimara Bucha, kulitokea vurugu baada ya mawakala kugombea  kuwasaidia wapigakura kuweka alama ya vema kwa wagombea pamoja na baadhi ya watu kutaka kurudia kupiga kura.

MSIMAMIZI UCHAGUZI APIGWA
Msimamizi wa kituo hicho, Stanslaus Ntakive, alipigwa na wapigakura kutokana na kukerwa na kitendo cha baadhi ya watu kurudia kupiga kura.

Japokuwa kulikuwa na idadi kubwa ya watu katika eneo hilo, ambalo lilikuwa na wasimamizi watatu, polisi hawakuonekana na kusababisha wasimamizi kupata wakati mgumu kudhibiti vurugu.

Jana asubuhi masanduku ya kupigia kura yanadaiwa kufikishwa katika kituo hicho yakiwa na karatasi zilizodhaniwa kuwa za kura na hivyo kulazimika kuchomwa moto.Katika manispaa ya Ilala uchaguzi uliahirishwa katika vituo 27 kutokana na kukosewa kwa karatasi za kupigia kura.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Issa Mngurumi, alisema makosa hayo yamefanywa na ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali na kwamba, kasoro hiyo imesababisha uchaguzi kuahirishwa.

MTENDAJI APIGWA MAWE
Afisa Mtendaji, Justine Mywenjwa, alipigwa mawe baada ya kutangaza kuahirisha uchaguzi huo.

MTAA MIGOMBANI
Katika Mtaa wa Migombani, vyama vimekubaliana kupiga kura katika nafasi ya uenyekiti tu nafasi, ambayo ndiyo ilikuwa na karatasiza kupiga kura.Sababu nyingine ni kutokuwapo  na vifaa vya kupigia kura wala makarani wa kusimamia zoezi hilo katika vituo hivyo.Mitaa mingine ambayo iliahirisha uchaguzi huo, ni Ilala Sharifu Shamba, Mchikichini, Kinondoni Mjini na Vingunguti.

MTAA MACHIMBO
Upigaji kura katika Mtaa wa Machimbo, Manispa ya Ilala, ulikumbwa na tafrani baada ya uchaguzi huo kugubikwa na vurugu jambo lililosababisha wananchi kususia kupiga kura.

Mtaa huo uliogawanywa kutoka Mtaa wa Ugombolwa, uchaguzi wake umeahirishwa kwa amri ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala hadi Desemba 21, kutokana na vifaa kutokuwapo.

Amri hiyo ilizua hamaki kwa baadhi ya wagombea wa vyama kwa pamoja wakamzingira Afisa Mtendaji wa Kata ya Segerea, kupinga kuahirishwa kwa uchaguzi huo hadi wiki ijayo.
Hatua hiyo ilisababisha wakazi wa mtaa huo kuilalamikia serikali kwa kutokamilisha vifaa hivyo wakisema ina lengo la kuwakosesha kura kwa kuwa watakuwa wamesafiri kwenda kusherehekea sikukuu za Krismas na mwaka mpya.

Uchaguzi katika Mtaa wa Machungwa-Vingunguti ulitawaliwa na vurugu na mapigano, huku wakiimba nyimbo za kuishutumu CCM kwa madai ya kujihusisha na wizi wa kura katika maeneo mbalimbali.

Wakazi wa mtaa wa Malapa Ilala Dar es Salaam,  ambao walikuwa katika foleni ya kupiga kura walisema tabia ya CCM ni kuvuruga uchaguzi ili kujinyakulia uchaguzi kinyume na mapendekezo ya wananchi kutokana na wengi wao kuchoshwa na chama hicho.

Katibu Mkuu wa Chama ADC, Lydia Bendera, alisema chama hicho kimesimamisha wagombea watatu  mmoja manispaa ya Kinondoni na wawili katika manispaa ya Ilala, hivyo kitendo cha CCM kuwa chanzo cha vurugu katika maeneo hayo  ni kuashiria wizi wa kura za wagombea wa vyama vya upinzani.

MNYIKA AMVAA PINDA
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliitaka serikali kupitia Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kurekebisha kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi haraka iwezekanavyo ili kupisha zoezi hilo kuendelea kama lilivyopangwa.

Alisema kitendo cha kusitishwa kwa uchaguzi kutokana na upungufu wa vifaa, majina kuingiliana, ni mchezo unaofanywa na CCM ili kuvuruga uchaguzi.

Zaidi ya wananchi 200 katika Mtaa wa Saranga, Kinondoni, hawakupiga kura baada ya ya majina yao kuwa kwenye orodha ya waliopiga kura kutoka katika maeneo mengine.

Kadhalika, walisema katika mtaa huo zilipelekwa gari 10 aina ya Noah kwa nyakati tofauti zilizokodi watu kutoka maeneo tofauti kutoka CCM kwenda kupiga kura.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema watuhumiwa watatu wanashikiliwa na polisi kutokana na kusababisha vurugu zilizosababisha kuvunjwa kwa masanduku manne yaliyohifadhi kura katika Mtaa wa Kinondoni Mjini.

MTAA WA TWIGA
Katika Mtaa wa Twiga, zoezi la upigaji kura lilianza saa 1.00 asubuhi, lakini ilipofika saa 3.00 asubuhi, lilisimama kabla ya kuahirishwa hadi wiki ijayo.

Hali hiyo ilitokea baada ya jina la mmoja wa wagombea, Scholastica Mgalula (Chadema), kuonekana likiwa limeandikwa kwenye orodha ya wagombea wa viti maalumu na wa makundi, huku jina la mgombea mwingine, Chidole Raphael (ujumbe-Chadema) likiwa halimo katika karatasi ya kura.

Licha ya wagombea uenyekiti kukutana kwa dharura na afisa mtendaji na kufikia mwafaka kwamba, kasoro iliyobainika irekebishwe papo hapo na zoezi la upigaji kura liendelee, mgombea wa Chadema, Judith Mgege, aliweka kikwazo akidai kwamba, hawezi kuamua mpaka kwanza ashauriane na mumewe.

Wagombea wengine wa nafasi ya mwenyekiti katika mtaa huo ni Said Runje (CCM) na Mohamed Kibira (CUF).

Kasoro hiyo mbali ya kusababisha mvutano mkubwa baina ya wapigakura na msimamizi wa uchaguzi, ilizua tafrani kubwa kiasi cha wafuasi wa Chadema na wa CCM kutaka kurushiana makonde na hivyo kusababisha askari polisi kuingilia kati na kutuliza vurugu.

Mvutano huo uliibuka baada ya wapigakura kutaka kura zilizokuwa zimekwishapigwa zichanwe kwa vile uchaguzi umevurugika, huku msimamizi wa uchaguzi akipinga suala hilo kwa madai kwamba, hakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.

Hata hivyo, wapigakura walichachamaa wakisisitiza kura hizo zichanwe mbele yao kwani ni mali yao, lakini baadaye walibadili msimamo baada ya polisi kuingilia kati.
Polisi walifanya kikao cha dharura kati yao na mawakala wa wagombea pamoja na msimamizi wa uchaguzi na kuafikiana kuwa masanduku yaliyokuwa na kura yapelekwe ofisi za kata zikachanwe huko na kwamba, wiki ijayo uchaguzi katika mtaa huo utaanza upya.

MTAA WA MBONDOLE
Uchaguzi katika Mtaa wa Mbondole, Kata Msongola, umeahirishwa hadi wiki ijayo kutokana na majina mawili ya wagombea wa CUF kukosekana kwenye karatasi ya kupigia kura.

Mgombea wa CUF, Mrisho Jogoo, aliwatangazia mamia ya wapigakura waliofurika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Mbondole kuwa majina ya wagombea hayaonekani.

Mgombea wa CCM, Thomas Nyanduli, alisema hakuna sababu ya kunyosheana kidole wala kutafuta mchawi, kwani kosa tayari limeshatokea.

Mtendaji wa Kata ya Msongola, Omary Ally, akiahirisha uchaguzi huo, alisema kasoro hiyo imetokea hata katika mitaa mingine, ukiwamo wa Kiboga.

Uchaguzi katika mitaa ya Mogo, Stakishari na Karakata, Kata ya Kipawa, umeahirishwa hadi wiki ijayo kutokana na kuchelewa kuwasili kwa vifaa vya kupigia kura katika vituo.

Mgombea uenyekiti Mtaa wa Mogo (Chadema), Castin Christopher, alisema anaamini kuahirishwa kwa uchaguzi katika mitaa hiyo ni hujuma zinazofanywa na serikali ya CCM ili kuwakatisha tamaa wananchi wasiwapigie kura wapinzani.

Katika mitaa hiyo, wananchi walionekana wakiwa na hasira baada ya kuelezwa kuwa uchaguzi umeahirishwa hadi Jumamosi wiki ijayo na kusikika wakisema CCM inataka kuleta machafuko nchini.

KITUO CHA ALIMAUA
Katika kituo cha kupigia kura cha Alimaua A, Manispaa ya Kinondoni, hali haikuwa shwari kutokana na idadi kubwa ya wapigakura wa mtaa huo kutokufanikiwa kupiga kura hadi muda wa kufunga shughuli za upigaji kura kituoni hapo.

Wapigakura hao walilalamikia utaratibu wa kuitwa kwa kutumia kipaza sauti na kunyimwa haki yao ya msingi ya kupiga kura, huku wakipoteza muda mwingi kituoni hapo.

Pia vituo vya kupigia kura vya Mfenesini na Morovian, Mtaa wa Mkondogwa, Kata ya Chamazi, wananchi waliwasili tangu saa 2 asubuhi, lakini hadi kufikia saa 7 mchana hawakufanikiwa kupiga kura kutokana na karatasi za kura za nafasi ya ujumbe kwa wagombea wa viti maalumu kukosekana pamoja na wino wa kupigia kura.

KITUO CHA MKUNDUGE
Mgombea uenyekiti, Tamimu Omari Tamimu, alisema hali ya uchaguzi katika kituo hicho, kilichopo Tandale kwa Mtogole, haikuwa nzuri kutokana na baadhi ya wapigakura kukuta majina yao yakiwa yameshapigiwa kura na watu wengine hali iliyozua mtafaruku.

RISASI ZAPIGWA
Vurugu kubwa ziliibuka jioni katika kituo cha Shule ya Msingi, Mwenge, Dar es Salaam baada zoezi la kuhesabu kura kukamilika.

Alitokea wakala wa CCM akachukua sanduku la kura na kutoka nalo nje ya kituo na kumwaga kura zote, hali iliyowalazimisha wafuasi wa Chadema kuingilia kati na kuanza kupigana na wafuasi wa CCM.

Polisi waliingilia kati kuwatawanya kwa kufyatua risasi za moto na wafuasi hao kutawanyika.Baadaye msimamizi wa uchaguzi aliwaita wahusika na kutangaza kuwa uchaguzi umevurugika na alipoulizwa kama utarudiwa, hakujibu zaidi ya kuingia kweney gari la polisi na kuondoka nao.

KILIMANJARO
Mkoani Kilimanjaro maeneo mengi hayakufanya uchaguzi kutokana na dosari mbalimbali.Katika Jimbo la Vunjo, Zoezi la upigaji kura limesitishwa kwa muda usiojulikana baada ya kutokea vurugu katika Kijiji cha Mamba Lekura na kusababisha kituo hicho kufungwa baada ya wananchi kuchoma moto karatasi za kupigia kura.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ya Vunjo na Moshi Vijijini, Fulgence Mpochi, alisema bado hajapata taarifa za uhalifu huo na  kama itathibitika kwamba wamefanya kweli tukio hilo, kwa mujibu wa kanuni na sheria za uchaguzi, Kijiji hicho cha Mamba Lekura, zoezi la uchaguzi litaahirishwa hadi baada ya siku 90.

Katika tukio jingine, mgombea wa Chadema, Juvenaly Kioro wa Kijiji cha Kilema Kusini amewekewa nembo ya CCM kwenye picha yake ili kuwachanganya wapiga kura wa Chama cha NCCR Mageuzi na Chadema.

Aidha, katika vituo vya Mamba Lekura, zoezi hilo limeahirishwa kwa muda usiojulikana baada ya karatasi za kupigia kura kusambazwa kidogo vituoni tofauti na idadi ya wapiga kura iliyobandikwa kwenye mbao za matangazo.

Baadhi ya vituo ikiwamo Njia Panda ya Himo, Darajani na Mwika Kati vimelazimika kuahirisha zoezi hilo kwa muda usiojulikana baada ya kutokea kwa vurugu kati ya wananchi na wasimamizi wa vituo vya uchaguzi baada ya wananchi kudai majina yao hayaonekani.

Moshi Mjini; Uchaguzi wa viongozi wa serikali za Mitaa ya Matindigani Kata ya Pasua na Kilimani Bar, Kata ya Bomambuzi, umeahirishwa hadi Desemba 21, mwaka huu baada ya kukosekana majina ya wagombea na karatasi za kupigia kura.

Mbali ya kuahirishwa kwa chaguzi za maeneo hayo, Meya wa Manispaa hiyo, Jafari Michael ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jimbo la Moshi Mjini, amelalamikia kukosekana kwa wino maalum ambao hutumika kama alama kwa mtu aliyekwishapiga kura, akisema kwamba chama tawala (CCM) kimetengeneza fursa ya wanachama wake kupiga kura zaidi ya mara moja.

Pia vituo vya Mashineni na Mbaoni, Kata ya Kariwa chini, zoezi la upigaji wa kura lilisimama  kwa zaidi ya saa tano kutokana na kukosekana kwa karatasi za kupigia kura pamoja na kuchanganywa kwa majina ya wagombea wa nafasi zinazogombewa.

Katika Jimbo la Hai dosari zilizojitokeza na kusababisha uchaguzi huo kuahirishwa leo katika vijiji vitano vya Foo, Wari Sinde, Wari Ndoo, Nshara na Uduru vilivyopo Kata ya Machame Kaskazini ni pamoja na kukosekana kwa karatasi za kupigia kura kwenye vijiji hivyo. Katika Kijiji cha Isawerwa, msimamizi wa uchaguzi alikimbia kituoni na kusababisha wananchi kukifunga kituo cha kura hadi hapo jina la mgombea uenyekiti wa kijiji hicho kupitia Chadema litakaporejeshwa.

Aidha, katika Kijiji cha Lyamungo Kati, Kata ya Machame Mashariki, wagombea wawili wa Chadema picha na majina yao yameondolewa kituoni na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo wakaruhusu wagombea pekee wa CCM kupigiwa kura bila ya kueleza iwapo waliwekewa pingamizi au laa.

Hali hiyo imejitokeza pia katika Kijiji cha Losaa, Mfomu, Shoshe na Mungu wa Mae, ambapo wasimamizi wa uchaguzi wamelazimika kusitisha zoezi hilo kwa muda usiojulikana kutokana na kukosekana kwa karatasi za kupigia kura.
Katika jimbo la Siha, Zoezi la upigaji kura limesitishwa kwa zaidi ya saa sita katika Kijiji cha Mbingati, Kata ya Biriri baada ya wakazi wa kijiji hicho kugoma kupiga kura hadi hapo jina la mgombea wa Chadema litakapoonekana kwenye sanduku la kupigia kura. Kijiji cha Mkombozi, Kata ya Orkolili na Kitongoji cha NARCO cha Kata ya Gararagua, vituo vyake vya kupigia kura vilikuwa havijafunguliwa hadi saa nne asubuhi kutokana na kukosekana kwa karatasi za kupigia kura.
Katika Jimbo la Rombo,  wakazi wa vitongoji vya Ture, Kahe na Kingachi vimekosa haki ya kuchagua viongozi wao baada ya watu wasiojulikana kuiba fomu za wagombea wa nafasi za wenyeviti wa kitongoji na kutokomea nazo kusikojulikana.
Mkurugenzi wa Wilaya hiyo, Mohamed Maje, alisema baada ya kubainika kuwapo kwa tatizo hilo, Kamati ya Rufaa imeridhia kwamba uchaguzi uahirishwe  hadi hapo utakapotangazwa tena.
Same Magharibi; Wagombea 21 wa Chadema walioomba mbalimbali hawatapigiwa kura na wananchi baada ya majina yao kutoonekana na hivyo kusababisha wananchi kuwapigia wagombea pekee wa CCM.
Katika jimbo hilo hilo, wananchi 180 wa Kijiji cha Marwa, Kata ya Ruvu walishindwa kupiga kura baada ya majina yao kutoonekana katika mbao za matangazo.

IRINGA
Mjini Iringa, viongozi wa  wa CCM na Chadema walizua mvutano katika  ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa wakidai kuwa watendaji wake wamevurugu  uchaguzi .

Vituo vingi vilichelewa kuanza kupiga kura kwa saa tano na   zaidi hali iliyowakatisha tama baadhi ya wapiga kura walioamua kuondoka katika vituo.

Akizungumza katika kituo cha Mwangata “A” ambacho ni miongoni mwa vituo vilivyocheleweshewa vifaa, Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alisema kilichotokea ni njama za CCM kutaka kuvuruga uchaguzi baada ya Chadema kuwabana kila kona.

“Serikali inastahili kubeba lawama kubwa kwenye hili   na hizi ni njama zao CCM za kutaka kuhujumu uchaguzi huu, hiyo ni baada ya Chadema kuwabana kila kona kwani tumesimamisha wagombea karibia mitaa yote wakati kitendo ambacho hatujawahi kukifanya kabisa,” alisema Msigwa.

Katibu wa CCM mkoa wa Iringa, Hassan  Mtenga, aliishukia ofisi ya  mkurugenzi wa manispaa ya Iringa akidai imevuruga uchaguzi huo.

“Katika kipindi chake cha  utendaji kazi ndani ya Chama sijawahi kuona uchaguzi wenye kasoro nyingi kama huu, nimetembelea vituo 39 kati ya 192 vya Mansipaa ya Iringa, kati ya vituo vyote hivyo ni vituo tisa  tu ndivyo havina kasoro yeyote,” alisema Mtenga.

Kwa upande wake kaimu  mkurugenzi wa Mansipaa ya Iringa,  Erasto Kiwale, alithibitisha kuwapo kwa tatizo hilo na kuongeza kuwa ofisi yake ilikuwa ainaendelea kulishughulikia.Wapigakura kadhaa walilalamikia ucheleweshaji huo baada ya kufika saa 5:00 bila upigaji kura kuanza.

Hamad Athumani ambae alikuwa kwenye kituo cha kupigia kura cha mwangata A alisema:

“Hadi sasa ni saa 5:30, hatujaanza kupiga kura na hatujui kama huo muda wetu  tutaongezewa jioni ama laa kwa sababu mwisho ni saa 10:00 jioni.”

Wakati hilo likiktokea katika katika kituo cha Mwangata A, mtaa wa Frelimo A , mgombea nafasi ya mwewnyekiti mtaa huo kupitia CCM, Domina Mgongolwa,  alikutwa akifanya kazi ya uawakala katika eneo la uchaguzi kinyume cha kanuni na taratibu za uchaguzi huo.

 Baada ya mvutano huo baina Mgongolwa   na Mwenyekiti wa Chadema Iringa Mjini, Frank Nyalusi, mgombea huyo aliondolewa katika eneo hilo.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa  katika Manispaa ya Iringa uliahirishwa kwenye mitaa ya Wazo A na B,  Ikonongo A na B,  Don Bosco A na B, Bwawani B na Imalanongwa B.Uliahirishwa na Kaimu Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Erasto Kiwale huku bado sababu za msingi zikiwa bado hazijafahamika.

MOROGORO
Mkoani Morogoro, dosari kubwa ilitokea katika wilaya ya Ulanga, yenye majimbo ya Ulanga Mashariki na Ulanga Magharibi kutokana na upigaji kura kuanza saa sita mchana.
Msimamizi wa uchaguzi wa wilaya hiyo, Isebara Chilumba, alisema kuwa kilichosababisha ucheleweshaji ni makosa ya kiuchapaji ya kuchanganya majina ya wagombea na ya vyama vyao na hivyo kulazimika kurudia upya kuchapishaji..

Kwa upande wa Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mvomero, Wallace Karia , ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo alisema kuwa ni Kata mbili za Mvomero na Dakawa vituo vilichelewa kufunguliwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo na uchache wa karatasi za kupingia kura.

Alisema Kata ya Mvomero vilichelewa kufunguliwa kwa muda uluiopangwa, lakini suala hilo lilipatiwa ufumbuzi na kazi ya upigaji kura uliendelea kama kawaida isipo kuwa Kata ya Dakawa  hadi mchana havikuwa vimefunguliwa kutokana na upungufu wa karatasi za kupinga kura.

DODOMA
Katibu wa Chama CCM Wilaya ya Dodoma Mjini, Othuman Dunga, gari lake lilishambuliwa na kuvunjwa vioo na wananchi baada ya kufika katika kituo cha kupiga kura cha Mlimwa Kusini katika Manispaa ya Dodoma.

Mmoja wa mashuhuda alisema, katibu huyo alikwenda katika kituo hicho kwa gari namba T 627 BFJ akiwa na takribani vijana sita.

“Mara baada ya kufika kituoni wananchi wakaanza kuwauliza wamekuja kufanya nini na kuwataka kuonyesha vitambulisho wakagoma wakidai wao ni usalama wa Taifa...baada ya hapo wananchi wakaanza kushambulia gari lake, wakalipasua vioo,” alisema shuhuda huyo.

Kwa upande wake Mgombea wa  nafasi ya uenyekiti kutoka Chama Cha Wananchi (CUF) Ismail Seif Mohamed alisema katibu huyo wa CCM pamoja na vijana wake walifika katika kituo hicho na kuanza kuwapanga watu.

Kwa upande wake mgombea wa nafasi hiyo wa CCM, Zubeda Rajab alithibitisha  kushambuliwa kwa gari hilo, lakini alidai katibu huyo hakuwapo ndani ya gari.
Msimamizi wa uchaguzi mkaoni Dodoma, Emmanuel Kuboja, alisema kama ilivyo kwa mikoa mingine nchini kote, Dodoma pia hakukuwa na wino kwa ajili ya kumuwekea alama kila mpiga kura aliyepiga kura.

Tatizo la kuchelewa kufunguliwa kwa baadhi ya vituo, alisema lilitokana na kasoro zilizobainika kwenye karatasi za kupigia kura na kufanyiwa marekebisho kwanza.

Chamwino, Kijiji cha Mpwayungu Kuboja alisema uchaguzi utafanyika kesho kutokana na majina ya wagombea kubainika kuwa yalichanganywa ndani ya fomu za uchaguzi.

Katika Kata ya Makulu, baadhi ya wanachi walisababisha vurugu, wakitaka kupigia kura mgombea wa uenyekiti wa mtaa wa Medelii, kwa tiketi ya Chadema, Joseph Chiuyo, huku sanduku la kupigia kura za mwenyekiti likiwa halipo.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Dodoma, Augustino Kalinga, alisema Mgombea huyo alijitoa kwa hiari yake kabla na baadaye akaandika barua kwamba aliahirisha kujitoa.
Wilayani Bahi - Kata ya Chikola Kwenye kituo cha Mpole, sanduku la kupigia kura kuchagua Mwenyekiti wa Kijijini cha Chimendeli, halikuwapo, ingawa wagombea wa nafasi hiyo kutoka CCM na Chadema, walikuwepo.

Ilipofika Saa 7:300mchana, NIPASHE iliondoka eneo hilo huku hali ikiwa bado tete, pia idadi kubwa ya wapiga kura waliondoka, wakihusisha tukio hilo na hujuma.

TANGA
Watu kadhaa walishindwa kupiga kura jana katika Jiji la Tanga kutokana na majina yao kutoonekana walipofika kwenye vituo vya kupigia kura.

Wananchi hao walisema  serikali ilikurupuka katika zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa na haikuwa tayari imejipanga kikamilifu.

Kusema kweli kuna mapungufu makubwa sana katika mchakato huu…kwanza mtu unakuja tangu asubuhi, lakini kwanza uchukue namba yako kwenye orodha iliyopo nje halafu ukiingia ndani kwa msimamizi unakuta nako kuna orodha ndani ya daftari ambayo aidha jina halionekani au namba zimejirudia, sasa unaona shida hiyo ndiyo wengine wanaamua kuondoka,” lisema Amina Khamis mkazi wa Kisosora.

NIPASHE ilitembelea vituo mbalimbali vya kupigia kura na kukuta wafuasi wa vyama kutupiana maneno ya kukejeliana na kushutumiana kwamba wagombea wao ni mapandikizi na hawatoki kwenye maeneo husika.

Hali hiyo ilijitokeza katika Kata ya Ngamiani Kusini ambayo ina mitaa minane ambapo polisi walipelekwa kuongeza ulinzi kwenye maeneo hayo ambayo wananchi walipinga agizo la kupiga kura na kuondoka vituoni badala yake wakalazimika kukaa kwenye makundi makundi wakisubiri muda wa matokeo kutangazwa.

Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Mtaa wa Mapinduzi A kwa tiketi ya CCM, Said Baka  ni miongoni mwa wagombea wanaoshutumiwa kuwa si mkazi wa eneo husika.

Hata hivyo, Baka alisema kuwa anashangazwa na maneno hayo hasa kwa kuzingatia kuwa amekuwa Mwenyekiti wa Mtaa huo kwa miaka mitano tangu 2009 alipokuwa CUF kabla ya kuhamia CCM mwaka jana.

Kwa upande  Wilaya ya Kilindi, Mkuu wa Wilaya Suleiman Liwowa, alikitangaza CCM kushinda kabla ya muda na taratibu za kumalizika kwa uchaguzi uliopangwa licha ya mitaa yake kuwa na kasoro za kutokuwepo kwa majina na baadhi ya namba za wapiga kura.

Baadhi ya wananchi waliokuwa wakitafuta majina yao kwa ajili ya kupiga kura walisema wanashangazwa na hatua ya Liwowa, kutangaza mshindi wakati wengi wao hawajapiga kura kutokana na majina yao kutokuwepo katika orodha.

MANYARA
Wilaya yote ya Hanang mkoani Manyara, vifaa vya kupigia kura vilianza kugawiwa saa 7.30 mchana.
Vituo vyote vya kata ya Endasaki, Niasikironi, Basutu, Barangi Wilayani Hanang`i mkoani Manyara zowezi la kupiga kura halikufanyika kutokana na kukosekana kwa vifaa huku.

TABORA
Wilaya  yote ya Kaliua mkoani Tabora uchaguzi huo uliahirishwa mpaka Jumapili ijayo kutokana na vifaa kuchelewa.

MWANZA
Katika kata ya Mahina wilayani Nyamagana, uchaguzi huo uliingia dosari baada ya wapigakura wa mtaa wa Isenghe A na B katika kituo cha shule ya msingi National na kituo cha kilimo kukuta majina yao yakiwa yamechanwa na mengine kutoonekana.

Mkazi wa kata hiyo, Andrew Pius, alisema licha ya kufika kituoni mapema kupiga kura, lakini bado majina yao hayaonekani huku karatasi zikiwa zimechanwa na nyingine majina kufutika kutokana na kulowa na mvua.

“Hapa tumefika asubuhi na mapema kupiga kura, lakini cha ajabu tunakuta majina yetu hayapo…tunashindwa kuelewa utaratibu uliopo kutokana na kutopewa jibu sahihi na wahusika,” Pius.

Hali hiyo kama hiyo ya majina kufutika, ilijitokeza katika kituo cha Ushirika mtaa wa Nyakahoja, huku vituo vilivyopo shule ya msingi Mkuyuni, mtaa wa Kang’anga, Mulumbani A, B na C wapigakura wengi walionekana kulalamika kutoona majina yao ambayo hayakupangwa katika mtiririko wa alfabeti.

Msimamizi msaidizi wa kituo cha Mulumbani A, B na C, James Chilagwile, alisema changamoto kubwa iliyoonekana tangu asubuhi ni kwa baadhi ya wapigakura kutoyaona majina yao ingawa baada ya kuwasaidia yalionekana.

“Hali ni ya utulivu katika kituo hiki, iwapo watu watakuwa wengi tutaendelea kupiga kura hadi mwisho wake,” alisema Chilagwile.

Kwenye kata ya Mandu kituo cha kupigia kura shule ya msingi National, baadhi ya wapiga kura waligundua kuchakachuliwa kwa fomu za wajumbe wa CCM na Chadema.

Fomu hizo ambazo zinatakiwa ziwe na nafasi ya wajumbe sita zilikutwa zikiwa na majina ya wajumbe wanne jambo lililoibua hasira kwa wapiga kura na kutaka kurudiwa kwa zoezi la kupiga kura.

Baada ya muda mfupi, kutokana na kelele kuzidi, msimamizi wa uchaguzi alitoka nje ya chumba cha kupigia kura na kuwaeleza fomu hizo zimepatikana.

Vituo vingi vilionekana kukosa vifaa vikiwamo karatasi, peni na mihuri kama ilivyokuwa baadhi ya mitaa maeneo ya Sengerema, Buchosa na Kwimba.

Mratibu wa uchaguzi mkoa wa Mwanza, Isack Ndasa, alithibitisha kuwapo na upungufu wa vifaa katika sehemu hizo, lakini lilipatiwa ufumbuzi mapema, huku vituo vilivyochelewa kuanza vitaongezewa muda.

SHINYANGA
Wananchi wa kitongoji cha Katunda kata ya Kizumbi mjini Shinyanga, waligoma kupiga kura baada ya majina ya wagombea wao kutoonekana katika daftari la uchaguzi, huku majina ya wagombea wa viti maalum na wajumbe wa serikali ya kijiji wakichanganywa nyadhifa zao, wengine wakipelekwa vitongoji ambavyo hawakugombea.

Walisema hawawezi kupiga kura kutokana na uendeshwaji mbovu uliosababisha baadhi ya majina ya wagombea wanaowataka kutokuwapo katika daftari la uchaguzi.

“Kwanza kituo kimechelewa kufunguliwa, baadhi ya majina ya wagombea kutoonekana huku wagombea wengine wakichanganywa nyadhifa zao, hivyo kutupa ugumu wa kupigakura na kuona haina haja ya kushiriki zoezi hili na kuamua kusambaa,” alisema Patric Mabula

Msimamizi wa uchaguzi katika kituo hicho, Spesioza Bulengwa, alithibitisha  kutoonekana kwa majina ya wagombea hao huku wagombea wengine wakichanganywa nafasi zao na kudai inawezekana walikosea kuchapisha majina hayo.

SIMIYU
Wapigakura kata ya Kiloleli wilayani Busega, mkoani Simiyu waliitupia lawama serikali na wasimamizi wa uchaguzi katika kata hiyo kwa kuchelewesha vifaa vya uchaguzi.

Kata hiyo yenye vijiji vitano vya Yitwimila A na B, Ijitu, Ihale na Ilumya masanduku ya kura yalicheleweshwa huku sehemu nyingine yakichelewa kufika kwa wakati.

Msimamizi wa uchaguzi katika wilaya hiyo, Yuna Yassin, alisema hawakutarajia kuchelewesha masanduku hayo bali ilikuwa ni muingiliano wa kazi na uhaba wa usafiri kwani halmashauri ina magari machache ya kusambazia sana hivyo wananchi wasiwe na wasiwasi ni lazima wapige kura alisema mkurugenzi huyo.

Mkuu wa wilaya Busega, Paul Mzindakaya, alisema katika mji wa Lamadi wagombea wa uchaguzi kupitia CCM walijiondoa dakika za mwisho.

Viongozi hao inadaiwa walijiondoa kutokana na kutishiwa kuuawa, kuchomewa moto nyumba zao pamoja na familia na wafuasi wa Chadema.

Mzindakaya alisema katika uchaguzi huo, wagombea wa Chadema walienguliwa kutokana kwa kutokidhi vigezo baada ya kuwekewa pingamizi na CCM.

Kamanda wa polisi mkoani Simiyu, Charles Mkumbo, alisema jeshi lake limejiandaa kukabiliana na vurugu itakayojitokeza katika mji huo wa Lamadi.

KAGERA
Mjini Bukoba kasoro mbalimbali zimejitokeza baada ya baadhi ya majina ya wagombea kuondolewa katika orodha kwa kuwekewa pingamizi na kutoonekana katika karatasi za kupigia kura.

Baadhi ya vituo ilishuhudiwa watu wakishindwa kuona majina yao katika orodha kutokana na nakala za orodha zilizobandikwa wino wake kufifia, lakini pia karatasi nyingine zikiwa maandishi yake yamefutika kabisa.

Katika kituo cha mtaa wa Jamhuri, uchaguzi haukuanza kwa muda uliopangwa kutokana na kuonekana kwa majina ya wagombea wawili katika karatasi za kupigia kura ambao waliwekewa pingamizi, majina mengi yaliondolewa.

Kutokana na tatizo hilo uchaguzi ulisitishwa kwa muda hadi msimamizi alipotoa ruhusa ya kuanza saa 3:10 asubuhi kuamua kuwapigia kura mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya mtaa huku kipengele cha viti maalum kikiamuliwa kuachwa ili wagombea wawili ambao hawakuwekewa pingamizi wapite bila kupingwa.

Kasoro nyingine ni mawakala wa vyama vya siasa kulalamikia kutokuwapo kwa fomu za kuandika kasoro zilizojitokeza katika vituo husika mfano kituo cha Katatolwanso.

Katika vituo vingine vya Kyakailabwa shule ya msingi na mtaa wa Nyangoye, kutokana na watu kutoona majina yao wasimamizi wa vituo hivyo akiwamo Deus Mugabi wa mtaa wa Nyangoye.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo katika jimbo la Bukoba mjini, Erick Bazompora, alisema watu wote waliojiandikisha watapiga kura maana majina yao yapo kwa wasimamizi wa vituo hata kama yamefutika.

GEITA
Wilayani Chato, mkoani Geita baadhi ya majina ya wapiga kura yalipelekwa maeneo tofauti na vituo vyao, watendaji wa vijiji kufanya kampeni wakati zoezi likiendelea pamoja na vituo kutobandikwa majina ya wagombea.

Baadhi ya vituo vya kupigia kura, masanduku yamecheleweshwa kufika hasa katika kituo cha Kalema vifaa hivyo vimefika saa 3 asubuhi badala ya saa 1:30.

Katika kituo cha Mtakuja kata ya Muganza msimamizi msaidi zi wa uchaguzi, Masalu Kalemanya, hakupelaka sanduku la kumpigia kura mwenyekiti wa kitongoji hicho kwa madai mgombea wa CCM alipita bila kupingwa baada ya mgombea wa Chadema kuwekewa pingamizi hatua iliyosababisha mtafaruku mkubwa.

Msimamizi wa uchaguzi wilaya ya Chato, Clement Berege, alisema hajapokea taarifa za mapungufu yoyote kutoka kwenye vituo wala kwa viongozi wa vyama vya siasa.

Wakati zoezi la kupiga kura likiendelea wapiga kura katika kijiji cha Nyawilimilwa kata ya Kagu wilayani Geita, wamechelewa kuanza kupiga kura hadi saa nne wakihofia kupigia kura kutokana na vurugu zinazodaiwa kuibuka usiku wa kuamkia jana.

Mkurugenzi wa uchaguzi katika Halmashauri ya mji wa Geita, Magarate Nakainga, alithibitisha kuwapo kwa hali hiyo na kuongeza uchaguzi katika mtaa huo umeahirishwa baada ya wananachi kususia.

MARA
Tarime: Mkazi mmoja wa kitongoji cha Kemwita Wahende,  anayedhaniwa mfuasi wa CCM, amepewa kipigo na wanaodaiwa wafuasi wa Chadema baada ya kukutwa na fomu za mfano ambazo ni batili kuwapo kituoni hapo hadi alipookolewa na polisi.

Msimamizi wa uchaguzi wa kata ya Sirari, Maisori, alisema mpigakura huyo alijisahau kuwa na fomu za mfano katika eneo la kituo baada ya kubanduliwa kutoka katika ubao wa matangazo.

Katika vituo vingi vya uchaguzi kumekuwapo na misuguano mikali huku kukiwa na vurugu za hapa na pale katika vitongoji vya Nyamorege, Gwitiryo, Sokoni, Pemba, Mama Kibasa, Songambele na kituo cha Sabasaba.

Mjini Musoma, tofauti na ilivyokuwa juzi wakati wa hitimisho la mikutano ya kampeni kwa wafuasi wa vyama vya CCM na Chadema kugombana na polisi kutumia mabomu ya machozi, hali ilikuwa shwari katika vituo mbalimbali vya kupigia kura.

Juzi wafuasi wa vyama hivyo walipigana na kusababisha vurugu kubwa hadi jengo moja la mfuasi wa CCM kuvunjwa vioo baada ya kufurumishiwa mawe.

SHINYANGA
Kahama:  Dosari za kupiga kura zimejitokeza katika baadhi ya kata wilayani Kahama mkoani Shinyanga kutokana na kuchelewa kwa vifaa vya kupigia kura kwenye baadhi ya vituo.
Baadhi ya vituo hivyo ni vya kata ya Malunga, Nyahanga, Igalilimi na Majengo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa mji wa Kahama, Felix Kimaryo, alisema vifaa vilichelewa kufika katika vituo vya kupigia kura lakini vimefika huku mtendaji wa kata ya Nyahanga, Nambo Ntaki, akikimbia ofisi yake na kuzima simu.

WAGOMBEA WAWILI CCM WAFARIKI GHAFLA
WAGOMBEA wawili wa nafasi ya uenyekiti katika mitaa ya Sweya kata ya Mkolani jijini Mwanza na Nyasebe katika kijiji cha Gamasara kata ya Nyandoto wilayani Tarime mkoani Mara kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamefariki dunia ghafla wakati uchaguzi ukiendelea.

Mkurugenzi wa jiji la Mwanza ambaye ni msimamizi wa uchaguzi, Hassan Hida, alisema mgombea wa mtaa wa Sweya, Pius Mihayo, alifariki ghafla wakati uchaguzi huo ukiwa unaendelea.

“Hatuelewi tatizo ni nini, lakini hatuwezi kuahirisha uchaguzi kutokana na msiba huo kwani umetokea wakati watu wanapiga kura ila tutangaza matokeo ya wajumbe na viti maalum tu,” alisema Hida.
Hida alisema kesho leo watakaa na kutangaza ndani ya siku saba kufanyika nafasi hiyo ya uenyekiti.

Huko Tarime, Wankyo Matiko (52), mgombea wa CCM, alifariki dunia kabla hajapiga kura yake baada ya kukumbwa na shinikizo la damu, na kusababisha uchaguzi huo kuahirishwa.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya mji Tarime, Venance Mwamengo, alisema wamesimamisha uchaguzi huo wa mtaa huo hadi watakapotangaza tena.
Daniel Mkate, Rose Jacob, Lilian Lugakingira, Daniel Limbe, Shushu Joel, Happy Severine, George Marato, Renatus Masuguliko,  Marco Maduhu, Mohab Dominick, na Samson Chacha.

Imeandikwa na Elizabeth Zaya, Efrasia Masawe, Frank Monyo, Hussein Ndubikile, Kamili Mmbando, Muhibu Said, Leonce Zimbandu, Thobias Mwanakatwe, Isaya Kisimbilu, Enles Mbegalo na Christina Mwakangale, Imeandikwa na Godfey Mushi, Charles Lyimo, George Tarimo, Friday Simbaya,  Ashton Balaigwa; Editha Majura, Agusta Njoji; Lulu George; Halima Ikunji, Mohamed Isambula,
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم