Dar es Salaam. Ikiwa imebaki miezi 10 tu kabla ya kufanyika kwa
Uchaguzi Mkuu mwakani, CCM kinaonekana kuteswa na tuhuma za rushwa
inayodaiwa kutolewa na makada wake wanaotajwa kutaka kuwania nafasi
mbalimbali ukiwamo urais.
Hali hiyo inabainishwa na kauli za baadhi ya
makada wa chama hicho katika ngazi mbalimbali ambao wameamua kulalamika
waziwazi ama kupitia vyombo vya habari au kwenye mitandao ya kijamii.
Moja ya kauli hizo ni ile iliyotolewa juzi na
Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki kwenye akaunti yake ya
Twitter akisema: “Mgawo wa Xmass na Mwaka Mpya kwa wajumbe husika wa CCM
ni kucheza na ugumu wa maisha uliopo. Ni ununuzi wa nafasi na si uwezo
wa uongozi. Aibu.”
Alipotakiwa kufafanua kauli yake, Kagasheki
alisema kwenye maoni yake hakutaja mtu licha ya kwamba wapo wengi
wanaotoa zawadi, lakini baada ya kuandika katika mtandao ameandamwa na
baadhi ya watu huku wengine wakimtolea lugha chafu.
“Hii ni line yangu ninaitumia kutoa mawazo siku
zote, lakini nimeshangaa leo watu wameshikia kidedea maoni hayo mpaka
wengine wanatumia lugha kali... sijamtaja mtu kwa sababu najua wapo watu
wengi wanaotoa zawadi,” alisema Balozi Kagasheki aliyewahi kuwa Waziri
wa Maliasili na Utalii huku akisisitiza kuwa hayo ni mawazo huru ambayo
anayaamini.
Waliyonena kuhusu rushwa
Kauli ya Kagasheki haina tofauti na zile
zilizowahi kutolewa na makada wengine, akiwamo mwenyekiti wake, Rais
Jakaya Kikwete na wengine waliowahi kushika nyadhifa za juu ndani ya
chama hicho na Serikali yake juu ya kukithiri kwa rushwa katika kusaka
madaraka.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula
alimwambia mwandishi wetu jana kuwa suala hilo linafuatiliwa kwa karibu
na dawa yake itaiva Februari baada ya kamati yake ya maadili
iliyofuatilia kutoa tathmini yake.
“Tulipotangaza kuwafungia, tuliunda kamati ya
ufuatiliaji harakati za kila mmoja kuona je, yale tuliyomtaka
kutoyafanya ametekeleza? Sisi tunaheshimu vikao vyetu, hivyo tunasubiri
kamati hiyo itakapotuletea taarifa yake.
“Katika tathmini hiyo kama watakuwapo wa kusamehewa watasamehewa na kama watakuwapo wa kuongezewa adhabu wataongezewa.”
Kauli ya Mangula ilikuwa inafafanua makada wa
chama hicho waliopewa onyo kali kwa kufanya kampeni mapema na
kujihusisha na vitendo vinavyokiuka maadili ndani ya chama na ndani ya
jamii.
Mangula alisema hayo wakati kukiwa na madai kuwa
baadhi ya wanachama wake kudaiwa kugawa fedha kwa wajumbe wa mkutano
mkuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) Zanzibar na maeneo mengine ya
nchi.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق