Serikali yakabidhiwa sekondari ya kisasa ya wasichana Geita

Mwanafunzi Roseline Joackim wa kidato cha tano mchepuo wa masomo ya sayansi (bailojia, kemia na fizikia), akionyesha kwa vitendo somo la fizikia na kemia katika maabara ya shule hiyo wakati wa uzinduzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Nyankumbu iliyojengwa kwa ufadhili wa Mgodi wa Dhahabu wa Geita, wilayani Geita juzi. Picha: Renatus Masuguliko.
Wananchi wametakiwa kujiepusha na baadhi ya Wanasiasa ambao wamekuwa wakipandikiza chuki dhidi ya wawekezaji kwa madai hawafanyia lolote, wakati juhudi zinazofanywa katika kusaidia jamii zinaonekana wazi.
Wito huo ulitolewa juzi na Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale, Ibrahim Marwa, katika makabidhano ya shule ya sekondari ya wasichana ya Nyankumbu iliyojengwa kwa ufadhili wa Mgodi wa wa dhahabu wa Geita ambayo hadi kukamilika itagharimu Sh. bilioni 10.

 Akitoa hotuba hiyo kwa niaba ya Mkuu mpya wa Mkoa wa Geita, Fatuma Mwasa, alisema kuwa wanasiasa hao wanavuruga juhudi za kuletea jamii maendeleo.

“Pamoja na kuwapo changamoto ... lakini pia yapo mazuri yanayofanywa na wawekezaji hawa kama ujenzi wa shule hii ya sekondari ya wasichana iliyozinduliwa leo ni moja ya mifano hai ya mchango wao,” alisisitiza Marwa katika sherehe hzo za kukabidhi shule hiyo kwa serikali.

Mkuu wa shule hiyo, Scholastica Manyahi, alisema shule hiyo ilianzishwa mwaka 2006 ikiwa na wanafunzi 80, walimu watano, vyumba vya madarasa tisa, nyumba mbili za walimu na jengo moja la utawala, lakini kwa sasa kutokana na ufadhili wa GGM vyumba vya madarasa vimeongezeka hadi 21, nyumba za walimu 19 zenye uwezo wa kuhifadhi familia 36 na idadi ya wanafunzi imeongezeka hadi 622.

 Manyahi alisema walimu nao wameongezeka hadi 51, kati yao 11 ni wa masomo ya sayansi na hisabati.  Aliongeza Shule hiyo ina bwalo kubwa la kisasa la chakula, mabweni tisa yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 576 kwa wakati mmoja, vyumba vitatu  vya maabara, maktaba ya kujisomea na makatba mbili za kompyuta.

Hata hivyo, alisema pamoja na mafaniko hayo, bado wana changamoto za kukosekana kwa huduma ya maji ya bomba, umeme wa gridi na usafiri. Akizungumzia utekelezaji mradi wa ujenzi wa shule hiyo Christian Rampa Luhembwe Makamu Mwandamizi wa Rais wa Kampuni ya Anglo Gold Ashanti (AGA) inayomiliki mgodi wa dhahabu wa Geita, alisema changamoto zilizotajwa zitapatiwa ufumbuzi kwani ni sera ya kampuni yao kuboresha huduma za kijamii na kuchangia maendeleo ya kijamii.

 Hata hivyo, alisisitiza kuwa wanaona fahari kufanikisha ujenzi wa shule hiyo ya kisasa kwa ajili ya kuwapatia elimu watoto wasichana kwani kuna usemi maaruu kwamba kumuelemisha mtoto wa kike ni kuelemisha Taifa zima tafauti na kumpatia elimu mtoto wa kiume ni kumuelimisha mtu mmoja.

Alisema shule hilyo itakuwa nyenzo ya kuwapatia watoto wa kike elimu bora kwa kuwandaa kuwa viongozi wa taifa la kesho na kuhimili mikikimikki ya ushindani wa utandawazi wa maisha ya dunia ya sayansi na teknolojia.

 Akizungumzia changamoto zinazowakabili wawekezaji katika makabidhiano hayo, Makamu wa Rais Maendeleo Endelevu ya Jamii wa AGA, Simon Shayo, alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa chanzo cha migogoro na kupandikiza chuki kati ya jamii na wawekezaji ikiwamo kuingilia masuala yanayohusu sera za kampuni hususani utoaji tenda na zabuni ambayo yapo kisheria.

 Alisema tayari baadhi ya malalamiko yao wameyasilisha kwa vyombo vya usalama kwa ajili ya kufanyiwa kazi kwani kampuni imelazimika kuchukua hatua hizo kwa kuhofia kuwapo kwa uwezekano wa kutumiwa upotoshwaji na uchochezi huo ili kuathiri shughuli za mgodi na kwa usalama na maslahi ya wafanyakazi na mali za kampuni.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم