SIMU ZA KISASA NI HATARI KWENYE MAPENZI!-2


Sikukuu ya Krismasi ndiyo imekwisha, ni matumaini yangu kwamba kila mmoja wetu ameinjoi sikukuu hiyo. Kwa wale ambao imewakuta vibaya kwa namna moja au nyingine, niwape pole. Wasijisikie wanyonge, Mungu atawafanyia wepesi katika matatizo yao na watarudi katika hali ya kawaida.
Kwa wale ambao wana tamaduni za kutoka na wapenzi wao, najua mtakuwa meitumia vyema nafasi hiyo kupanga mikakati mizuri ya penzi lenu kwa mwaka ujao.Tukirudi katika mada tuliyoianza wiki iliyopita, ilikuwa ikitufundisha athari za matumizi ya simu za kisasa katika uhusiano wa mapenzi. Tuliona namna ambavyo simu hizo zinavyokuwa tatizo katika uhusiano na kufikia hata watu kuachana. Tuendelee kutoka pale tulipoishia wiki iliyopita:
Kuna mwingine anaweza kukuvumilia, uvumilivu ukimshinda pia anaweza kuibua ugomvi ambao huwezi kuutegemea. Hiyo itadhihirisha ni kiasi gani amechoka na katika ugomvi huo kuna mawili, yawezekana mkaelewana au msielewane tena.
Kwa mtazamo wa kawaida mtu anaweza kuona suala hili ni dogo lakini niwaambie ndugu zangu, linaweza kusababisha ugomvi mkubwa na watu wakaachana na kila mtu akaendelea na maisha yake.
Uchunguzi unaonesha kwamba, ‘uchizi’ huo wa simu unakolea zaidi maana siku hizi kuna mitandao ya kuweka picha na kuchangia kama Facebook na Instagram. Mtu anapoteza muda mwingi kutazama picha, kuchangia au ‘ku-like’ picha ya mwenzake hata wakati ambao yupo kwenye uwanja wa sita kwa sita.
Ili kujua madhara ya hizi simu za kisasa, nikupe mfano halisi wa binti mmoja ambaye aliniomba ushauri. Binti huyo aliyejitambulisha kwa jina la Kerry aliandika hivi:
“Kaka samahani naomba unisaidie nimetengana na mume wangu kwa sababu tu alikuwa hapendi nichati na rafiki zangu katika grupu la kazini, sikuwa nachati na wanaume wengine wala nini lakini alinivamia na kuninyang’anya simu yangu na kuipasua chini.
“Alinipiga sana siku hiyo, nilijitahidi kumuomba msamaha lakini akadai nimezidi kumdharau kwani si mara moja ninampuuza kufanya mambo ya muhimu pindi ninapokuwa bize na simu. Huwezi amini alifikia uamuzi wa kuniambia niondoke nyumbani hadi pale nitakapojirekebisha, nifanye nini wakati bado nampenda mume wangu?”
Kupitia binti huyo tunajifunza nini? Wakati simu za kisasa hazijaingia, simu zilikuwa haziwezi kuwapotezea watu muda mrefu. Mtu alikuwa anatumia pale tu anapotaka kupiga au kumtumia mwenzake ujumbe mfupi.
Lakini baada ya ujio huu wa simu za ‘kujismatifonisha’, watu wamelewa na programu mbalimbali ambazo zipo kwenye simu hizo. Wanandoa, wapenzi wanajikuta wakiingia katika migogoro kila kukicha chanzo ni simu.
Madhara yamekuwa makubwa tofauti na faida za simu hizo. Simu hizo zina vitu vizuri kama tutazitawala lakini pale tunaporuhusu zitutawale ndipo zinapogeuka kuwa tatizo.
Kinachotakiwa kufanyika hapa ni kutoruhusu matumizi ya kupindukia ya simu hizo. Kerry asingekubali kutawaliwa au mtu wa kuchati kila wakati pengine wasingefikia hatua ya kutengana na mumewe.
Wapendanao au wanandoa wanapaswa kujua kwamba kuna wakati wanapaswa kutumia simu hizo lakini kuna wakati wanapaswa kuziweka pembeni na wakaogelea penzini.

Tenga muda wako vizuri kulingana na mahali ulipo. Kuna mahali simu inapaswa kuzimwa kabisa ili kupisha jambo fulani lifanyike.Marafiki kwa leo tuishie hapo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine nzuri!

Post a Comment

Previous Post Next Post