Katuni
Taarifa mojawapo ya gazeti hili jana ilieleza kwa kina juu ya dosari kadhaa zilizojitokeza na pia namna vurugu zilivyoibuka katika baadhi ya maeneo. Kwingineko, mbwa walitumika, virungu vilitembezwa na risasi kadhaa kupigwa hewani na polisi ili kutuliza vurugu.
Kuna maeneo karatasi za kura ziliibwa, ngumi zilitembea na zomeazomea ilitanda. Kwa ujumla, yapo maeneo mengi ambayo hali haikuwa nzuri.
Hakika, jambo hili haliashirii mema. Katika taifa hili ambalo wananchi wake wengi huridhia misingi ya demokrasia, kamwe vituko hivi havitarajiwi.
Ni kwa sababu siku zote, maamuzi ya wengi kupitia sanduku la kura ndiyo huchukuliwa kuwa njia pekee ya kupatikana kwa viongozi wa ngazi zote za serikali; kwa maana ya kuanzia serikali za mitaa, udiwani, ubunge hadi urais. Hili ni jambo la kujivunia. Hakuna njia nyingine bora ya kupata viongozi zaidi ya hii ya kutumia sanduku la kura.
Upo ushahidi wa kuwapo kwa mapigano yanayoishia kumwaga damu nyingi za watu wasio na hatia katika mataifa yaliyojaribu kupuuza sanduku la kura kupata viongozi wao. Hivyo, nasi hatupaswi kufuata njia nyingine isipokuwa hii ya uchaguzi kama wa juzi.
Hata hivyo, NIPASHE tunaamini kwamba kwa kasoro hizi, ni dhahiri kwamba sasa tunaelekea kusikostahili. Badala ya kuimarika kwa misingi ya demokrasia kwa kuwa na uchaguzi usiokuwa na chembe ya mizengwe, sisi tumeonyesha dalili za kurudi nyuma kwa kasi kubwa.
Hali hii ni ya hatari. Na haipaswi kuachwa iendelee. Mamlaka ya usimamizi wa uchaguzi huu wa mitaa, ambayo ni Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) iliyoko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, inapaswa kutafuta suluhisho la kudumu la kuondoa kasoro zilizojitokeza ili kuliepusha taifa na vurugu zinazoepukika.
Sisi tunakumbushia yote haya kutokana na ukweli kwamba mambo mabaya ndiyo hupata nguvu kulinganisha na mazuri. Hali ya amani na utulivu iliyotawala katika maeneo mengi ya uchaguzi juzi imegubikwa kwa kiasi kikubwa na taarifa za kuwapo kwa wingi wa kasoro kwenye baadhi ya vituo, tena karibu katika kila mkoa.
Ni wajibu wa Tamisemi kushughulikia kasoro hizi ambazo nyingi ziko ndani ya uwezo wao na kuhakikisha kwamba mambo haya hayajirudii katika chaguzi zijazo. Na hilo litafanikiwa zaidi ikiwa Tamisemi wataendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa uchaguzi huo, ambao ni pamoja na vyama vya siasa, asasi za kiraia na pia wananchi wenyewe.
Kwa mfano, NIPASHE tunashangazwa na kuwapo kwa taarifa kwamba kuna vituo vingi vilishindwa kufanya uchaguzi huo kutokana na ukosefu wa vifaa.
Katika baadhi ya vituo, wananchi waliojiandikisha walitekeleza wajibu wao wa kujitokeza kwa nia ya kupiga kura, lakini wakaishia kupoteza muda wao mwingi wakiwa katika foleni kabla ya kuambiwa baadaye kuwa zoezi hilo limeahirishwa kwa vile hakuna karatasi za kupigia kura.
Wapo waliokwama pia baada ya kukosekana kwenye orodha ya wapiga kura, na wapo waliobahatika kupiga kura lakini ikawa kazi bure kwao baada ya vurugu kuibuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kuchelewa kutangazwa kwa matokeo hadi usiku wa manene.
Yote haya ni mambo ambayo hayastahili kupata nafasi katika jamii iliyoamua kwa dhati kufuata misingi ya demokrasia. Aidha, inasikitisha zaidi kusikia Tamisemi wakitoa majibu mepesi kuhusiana na kasoro hizi. Mathalan, madai kwamba eneo la nchi ni kubwa na ndiyo maana kasoro zimekuwa nyingi hayana mashiko.
Ni kwa sababu Tamisemi ilishajua kitambo kirefu kwamba uchaguzi huo ungehusisha watu zaidi ya milioni 11 kati ya milioni 18 waliotarajiwa. Tamisemi ilijua vilevile kwamba uchaguzi huo wa juzi ungehusisha vitongoji 64,000 nchini kote. Hata siku chache kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, Tamisemi ilitangaza kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuwa kila kitu kiko sawa.
Kwa msingi huo, ndipo sisi tunaposisitiza kuwa Tamisemi ni lazima ifanye kazi ya ziada ya kuhakikisha kuwa chanzo cha kuwapo kwa utitiri wa kasoro katika siku ya uchaguzi kinafahamika na mwishowe suluhu ya kudumu inapatikana.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment