Tamisemi yafurahia mwamko wananchi kwenye uchaguzi

Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda
Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda, amesema wananchi wamepata mwamko mkubwa kushiriki katika chaguzi licha ya changamoto mbalimbali zilizojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Akizungumza jana katika mahojiano na NIPASHE kuhusiana na kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo, alisema changamoto hizo zimetokana na idadi kubwa ya wananchi kujiandikisha katika uchaguzi huo na hivyo maeneo mengi kulazimika kuahirisha kufanya uchaguzi.

Luanda alisema kasoro zilizojitokeza katika uchaguzi huo ni changamoto kwa serikali ambayo itahakikisha zinatafutiwa ufumbuzi ili hali hiyo isiweze kujitokeza katika uchaguzi mkuu mwakani.

Alisema tatizo la watu kupiga kura mara mbili kutokana na kukosekana kwa wino wa kuwatambulisha kama wamepiga kura ilitokana na uchaguzi huo kufanyika ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji ambako wanaoishi katika eneo moja wanafahamiana kwa sura na ukoo.

 “Vijijini watu wanafahamiana na ndiyo maana tuliamua kuachana na mambo ya wino kwa sababu kama kuna mtu ambaye ni mgeni amefika katika eneo ambalo siyo lake kupiga kura ni lazima watu watamjua na kuhoji kuwa anatoka wapi.. uchaguzi huu ni tofauti na uchaguzi mkuu,” alisema Luanda.

Luanda aliipongeza mikoa ya Kusini kwa kufanya uchaguzi huo kwa amani na utulivu kwa kuwa hakuna tukio lolote baya la fujo na uvunjifu wa amani lililotokea katika mikoa hiyo.

Alisema Mkoa wa Mtwara kulikuwa na hofu ya kutokea fujo kutokana na historia ya kuzuia gesi isitoke lakini katika uchaguzi huu hali imekuwa shwari kuliko ilivyotegemewa.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post