Ofisa uhusiano wa TBS, Roida Andusamile
Ofisa uhusiano wa TBS, Roida Andusamile, alisema, kutokana na uhaba wa rasilimali watu, shirika hilo linashindwa kuwa na udhibiti wa saa 24 kwenye bandari zinazotambulika na bubu ambazo ni malango mikubwa ya bidhaa feki kutoka nje.
Baadhi ya bandari bubu ni pamoja na Bagamoyo iliyopo mkoani Pwani na Mbweni, jijini Dar es Salaam.
“TBS inapeleka watendaji wake kila siku katika maeneo ya bandari kwa ajili ya kudhibiti bidhaa ambazo hazina ubora kutoka nje ya nchi…tunatakiwa tuwepo saa 24, lakini hatuko hivyo kutokana na uhaba wa watendaji,” alisema ofisa huyo.
Kwa mujibu wa Andusamile, awali shirika hilo lilikuwa na watumishi 188, lakini kwa sasa lina wafanyakazi 233 baada ya serikali kuwaongeza wengine 45 kati ya 200 ambao wanatarajiwa kuongezwa katika mwaka huu wa fedha.
Alisema watumishi hao watasaidia kudhibiti uingizwaji wa bidhaa feki katika ofisi mpya za TBS ambazo zinatarajiwa kufunguliwa katika maeneo ya Mtukula (Bukoba), Kasumulo (mpakani mwa Kyela na Malawi) na Tunduma.
Aidha, katika mwaka huu wa fedha, shirika hilo linatarajia kufungua ofisi za kanda katika mikoa ya Mwanza na Arusha lengo likiwa ni kupanua wigo wake nchini kote.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment