
Katuni
Taarifa hiyo iliyoripotiwa katika gazeti hili jana ilieleza zaidi kuwa wazazi wa binti huyo ndiyo waliokuwa mstari wa mbele kufanikisha mpango wa kumuozesha binti yao kwa mtu mwenye umri ulio sawa na babu yake, hiyo ikiwa ni baada ya kukubali mahari yake inayotajwa kuwa ni sukari ya ujazo wa kilo mbili.
Ilielezwa zaidi kuwa binti huyo mwenye miaka 16 ni wa jamii ya wafugaji wa Kimasai kutoka katika Kata ya Orkolili na kwamba, kila kitu kilishakamilika na maisha ya ndoa yangeendelea pasi na uwezekano wowote wa msichana huyo kuendelea na masomo.
Hata hivyo, walitokea baadhi ya wananchi waliopinga kitendo hicho na kutoa ushirikiano uliosaidia taarifa kufika kwa wanaharakati wanaoshughulikia utoaji wa elimu kuhusu athari za ukeketaji mkoani humo na baadaye sakata hilo kufikishwa kwenye Dawati la Jinsia la Polisi wilayani Siha na mwishowe ndoa hiyo ya 'babu na mjukuu' ikavunjwa.
Aidha, ilibainika kuwa katika eneo kulikofanyika ndoa ya 'babu na mjukuu' (Kata ya Orkolili) kuna tatizo kubwa la kuwapo kwa vitendo vya ukeketaji kwa wasichana.
Mabinti takriban 15 waliokolewa wakati wakiwa katika hatua za mwisho za kukeketwa. Kwa ujumla, taarifa hizi zimekuwa za kusikitisha zaidi katika dunia ya sasa, hasa kutokana na kampeni za kila uchao kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Na maeneo mengine yanayotajwa kukumbwa zaidi na matukio haya ya kuozesha mabinti wadogo na pia kuwakeketa kwa idadi ya makumi ni pamoja na yale ya kata za Makiwaru, Karansi, Gararagua, Biriri.
Ni wazi kwamba matukio ya aina hii huyokea pia kwingineko nchini. Ni dalili kwamba bado kuna umuhimu wa kuendeleza harakati zaidi za kuelimisha jamii juu ya athari za kuwakatisha masomo watoto na kuwaozesha bila ridhaa yao, tena kwa watu wenye umri mkubwa wa kuweza kuwaita baba na babu.
Hakika, kazi hii ya kuelimisha umma haipaswi kukoma. Iongezewe kasi huku pia ikienda pamoja na uchukuaji wa hatua kali za kisheria dhidi ya wale watakaojitia pamba masikioni mwao na kukumbatia vitendo hivi.
Kamwe, haikubaliki hata kidogo kuona kuwa binti akikatishwa masomo yake ili aolewe. Ni unyama mkubwa. Ni ukatili usio na mfano. Katika hali ya kawaida, haingii akilini kwa baba mwenye umri wa miaka 50 kutoa fedha au zawadi yoyote ile kwa wazazi ili amuoe binti mdogo anayefikiria namna ya kutimiza ndoto zake kimaisha.
NIPASHE tunaamini kuwa tukio kama hili linaashiria kwamba bado kuna watu hawajui, au wanapuuzia madhara yanayoweza kutokea kutokana na vitendo hivi. Watu waliokula wakashiba hawapaswi kuachwa wawaharibie watoto maisha yao ili tu kutimiza matakwa ya tamaa zao za kimwili, kifedha na vitu kama sukari.
Kwa sababu hiyo, ni vyema jamii ikakumbushwa kuwa mbali na ukatili wa kijinsia, ndoa hizi za utotoni pia husababisha maafa makubwa. Kwa mfano, viungo vya uzazi vya wasichana huwa havijakomaa kiasi cha kuhimili changamoto za mimba na kujifungua. Matokeo yake, pale inapotokea kwamba wameshika mimba, mabinti wa aina hii huwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha yao na ya watoto wao.
Kadhalika, lipo pia tatizo la kuwa na jamii iliyojawa na kina mama wasioelimika. Kwamba, ikiwa wasichana watakuwa wakiendelea kukatishwa masomo ili waolewe, maana yake ni kuwa wengi hawatapata fursa ya kujiendeleza kielimu. Na hili husababisha matatizo mengine makubwa ya kiuchumin na kijamii.
Mfumo dume utaendelea kutawala na matokeo yake, jamii yenye kukumbatia taratibu hizi itaendelea kuwa nyuma katika maeneo mengi ya maendeleo.
Ni jukumu la jamii nzima kuamka sasa na kuungana katika kuhakikisha kwamba tukio kama hili la kuozeshwa kwa msichana aliyestahili kuendelea na masomo yanakomeshwa mara moja. Tuwalinde watoto wetu kwa namna yoyote ile kwani ni haki yao na pia wao ndiyo taifa la kesho.
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق