Huko Nigeria mwanajeshi hunyongwa anapokataa kupigana dhidi ya
kundi la kigaidi la Boko Haram. Na karibuni huko Kenya ilipitishwa
Sheria ya Usalama, ambayo pindi busara haitatumika itaweza ikaipeleka
nchi hiyo pabaya na hata kuonekana mbele ya watu wa ndani na nje kwamba
ni dola ya kipolisi.
Serikali za nchi hizo mbili za Kiafrika- moja iko
Afrika Magharibi na nyingine Afrika Mashariki, zina kila sababu ya
kupambana na kuwazuia magaidi wanaohatarisha usalama wa raia na mali
zao. Lakini mara kadhaa malengo mazuri humalizikia kwa matokeo mabaya na
vurugu, ikiwa uangalifu hauchukuliwi.
Pia ikiwa watekelezaji wanakuwa wakakamavu na
kutokuwa tayari kuzidurusu hatua zao kila wakati kama zinaambatana na
tunu muhimu za kuheshimu utu wa mwanadamu. Kuna wasiwasi kwamba hatua
zilizochukuliwa na serikali za nchi hizo mbili zinakosa malengo na
hazitasaidia kuondoa mzizi wa fitina wa ugaidi.
Mashambulzi ya kigaidi
Katika kisa cha karibuni cha mashambulio ya
magaidi huko Nigeria ambayo yametia fora mwaka 2014, magaidi wa Boko
Haram waliwateka nyara watu kadhaa. Msemaji wa Serikali ya Nigeria
alikuwa hana zaidi la kusema ila kushtushwa, kusikitishwa na kukilaumu
kitendo hicho.
Baada ya shambulio hilo lililofanywa karibu na
Gumsuri, kijiji kilichoko katika Mkoa wa Kaskazini mwa Borno, mambo
yalibadilika na kuwa vurugu tupu. Barabara nyingi zilikuwa hazipitiki na
mawasiliano kupitia simu za mikononi yalikuwa hayawezekani. Kwa hakika
ilichukua siku kadhaa hadi sura kamili ya tukio hilo kupatikana katika
mji mkuu wa Abuja.
Inasemakana wanavijiji walikusanywa na kuhamishwa
kama ng’ombe, si chini ya 35 kati yao waliuawa kwa risasi. Habari
nyingine zinasema wanawake na wasichana 200 walipakiwa katika malori na
haijulikani walikopelekwa.
Japokuwa kikundi cha Boko Haram halijakiri
kuhusika, lakini mabingwa wa harakati za magaidi wanasema shambulio hilo
jipya lina sura kwamba Boko Haram ndio walioufanya ukatili huo. Idadi
ya ukatili unaofanywa na kikundi hicho, ambacho bila ya haki kinajigamba
kinausemea Uislamu, imeongezeka hivi karibuni.
Mwaka wa 2014 maelfu ya watu wasiokuwa na hatia
wameuawa Nigeria na kundi hilo, ambalo tangu mwaka 2009 limekuwa likidai
kuweko dola huru la Ukhalifa ( Mrithi wa Mtume Muhammad). Kwa mujibu wa
jumuiya zinazotoa misaada, Wanigeria milioni 1.5 wamekimbilia kwenye
mikoa ilio na amani au wameelekea nchi jirani kutokana na kitisho cha
Boko Haram.
Jeshi la Nigeria linaonekana kuelemewa, haliwezi
kuwalinda raia na zaidi haliungwi mkono na raia. Linakosa silaha za
kisasa. Maafisa pamoja na wanajeshi wao kwa muda mrefu wamekuwa
wakilalamika kwamba hawana silaha za kutosha kuweza kukabiliana na
kuwashinda wapiganaji wa Boko Haram walio na silaha za kutosha.
Nyingi ya silaha waliozonazo Boko Haram ni zile
zilizoachwa na wanajeshi wa serikali wanaokimbia kutoka uwanja wa
mapigano. Mara kadhaa kumetokea visa vya wanajeshi wa serikali huko
Borno kukataa kutii amri za wakuu wao. Wanajeshi hao husimamishwa mbele
ya mahakama za kijeshi wakishtakiwa kuwa waoga mbele ya adui au kufanya
uasi na 54 kati yao wameshapewa hukumu ya kifo.
Lakini haifikiriwi kwamba hukumu kali za kifo
dhidi ya wanajeshi waoga itaibadilisha hali ya mambo inayozidi kuwa
mbaya huko Nigeria. Ingekuwa bora kuushughulikia mzizi wa tatizo hilo la
ugaidi wa Nigeria.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق