Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa Anna Tibaijuka.
Baada ya matokeo ya awali kuonyesha kwamba vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupata viti katika ngome za mawaziri kadhaa, matokeo yaliyopatikana jana yanaonyesha kwamba Ukawa wamezoa viti vingi katika Jimbo la Muleba Kusini, mkoani Kagera ambalo Mbunge wake ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.
Katika jimbo hilo, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kilipata vijiji 46, Chama Cha Wananchi (CUF) vijiji vinane na CCM vijiji 38.Kwa upande wa vitongoji, Chadema kilipata vitongoji 167, CUF vinane na CCM 146.
Jumla ya nafasi za vijiji na vitongoji zilizotangazwa matokeo yake katika jimbo hilo zilikuwa 413, kati ya hizo Chadema 213 (51.6%), CCM 184 (44.5%) na CUF 16 (3.9%).
Katika Jimbo la Muleba Kaskazini, ambalo Mbunge wake ni Charles Mwijage, hadi jana jioni matokeo hayakuwa yamekamilika kutokana na maeneo kadhaa kura kuwa na utata, lakini Ukawa walikuwa wakionekana kufanya vizuri.
Baadhi ya matokeo yaliyopatikana yalionyesha kuwa Chadema walikuwa wamepata vijiji 31 kati ya vijiji 64 (asilimia 49) huku kikipata vitongoji 118 kati ya vitongoji 285 (asilimia (41).
Ukawa pia walipata viti kadhaa katika Jimbo la Mtama la Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Jimbo la Bunda linaloshikiliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira.
Majimbo mengine ambayo Ukawa walipata viti ni la Bumbuli la Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na la Urambo Mashariki linaloshikiliwa na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
TAMISEMI YATANGAZA MATOKEO
Wakati huo huo, serikali imetangaza matokeo ya wilaya 142 zilizokamilisha uchaguzi, na ya baadhi ya maeneo katika wilaya 18 zilizokuwa na kasoro huku ya wilaya tatu ambazo hazijafanya uchaguzi yakitarajiwa kutolewa kuanzia Jumatatu ijayo.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Khalist Luanda, alisema kwa maeneo ambayo yalipata kasoro katika uchaguzi huo, yataurudia mwishoni mwa wiki hii zikiwamo wilaya hizo tatu.
Alisema katika sehemu ambazo wagombea walifariki dunia, taratibu za uchaguzi zitaanza upya na kwamba kutakuwapo na kura za maoni kwa ajili ya uteuzi katika vyama na kufuatiwa kampeni.
Akitangaza matokeo hayo, Luanda alisema katika nafasi ya vijiji ambavyo matokeo yake yamepokelewa ni jumla ya vijiji 9,047 ambapo CCM ilipata 7,290 sawa na asilimia 80.58, Chadema 1,248 sawa na asilimia 13.79 na TLP viwili sawa na asilimia 0.02.
Vyama vingine ni CUF vijiji 382 sawa na asilimia 4.22, NCCR-Mageuzi 14 sawa na asilimia 0.15, NLD viwili sawa na asilimia 0.02 na ACT vinne sawa na asilimia 0.04.
Kwa upande wa mitaa 3,231, CCM ilipata 2,194 sawa na asilimia 67.90, Chadema 828 sawa na asilimia 25.63, CUF 235 sawa na asilimia 7.27, NCCR Mageuzi minane sawa na asilimia 0.25, TLP mmoja sawa na asilimia 0.03, NLD tisa sawa na asilimia 0.28, UDP mmoja sawa na asilimia 0.03 na ACT mmoja sawa na asilimia 0.03.
Akizungumzia upande wa vitongoji 42,824, alisema CCM ilipata 35,564 sawa na asilimia 83.05, Chadema 5,970 sawa na asilimia 13.94, CUF 1,555 sawa na asilimia 3.63, NCCR-Mageuzi 80 sawa na asilimia 0.19, TLP 11 sawa na asilimia 0.03, NLD kimoja sawa na asilimia 0.00, ACT 10 sawa na asilimia 0.02 na UDP 21 sawa na asilimia 0.05.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment