Korogwe. Polisi wilayani hapa imewakamata
wahamiaji haramu 12 wenye asili ya Ethiopia wakiwa wamefichwa katika
gari lililokuwa likielekea Dar es Salaam.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Tanga, Freisser
Kashai aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa wahamiaji hao
walikamatwa juzi saa 10:00 jioni katika kizuizi cha polisi kilichowekwa
Kijiji cha Bwiko, Barabara ya Mombo-Segera.
Aliwataja watu hao kuwa ni, Kashoma Bayen (24),
Berchano Gamada(32), Awal Jamal(23), Yanis Gatiso(28), Metson
Sipril(21), Tashona Hayalis(30), Adino Samiru(20)Kengeny
Siyun(22),Charnes Egesa(20), Abdi Badru(21), Siumanda Samadu (26) na
Malako Abuu (23).
Alisema wakati wa mahojiano ilikuwa vigumu
kuelewana kutokana na watu hao, waliokuwa katika hali mbaya kiafya,
kutojua kuzungumza Kiswahili wala Kiingereza, hivyo kupata majina yao
tu.
Alisema kwa sasa, polisi inaendelea kufanya
upelelezi na mara baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu
tuhuma za kuingia nchini bila kibali.
Akizungumzia kuhusu watu wanaofanya biashara ya
kusafirisha watu, kamanda Kashai alisema polisi itaendelea kufanya
upelelezi ili kuwabaini watu hao na kuwafikisha mahakamani.
إرسال تعليق