Wamtaka RC kufanya uchunguzi wa kumpotosha Dk. Bilal

Makamu wa Rais Dk.Mohammed Gharib Bilal.
Wakazi wa Kijiji cha Kilototoni Wilaya ya Moshi, wamemtaka Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, kuunda tume ya uchunguzi itakayoshughulikia madai ya kupotoshwa Makamu wa Rais Dk. Mohamed
Gharib Bilal kuhusu utekelezaji wa mradi wa usambazi wa umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati vijijini (Rea) katika Mamlaka ya mji mdogo wa Himo.

Wanadai, Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) lilimdanganya Makamu wa Rais kwamba miongoni mwa vijiji vitakavyonufaika na mradi huo kwa sasa ni pamoja na Kilototoni lakini kwa sababu zisizoeleweka, imechepusha mradi huo na kuutekeleza katika kijiji jirani cha Ghona, kata ya Kahe Mashariki.

Dk. Bilal alitoa ahadi hiyo Oktoba 7, mwaka 2013 akiwa kata ya Makuyuni wilayani hapa, wakati akizindua rasmi miradi ya ukarabati wa vituo vya kupooza umeme na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme katika mkoa wa Kilimanjaro.

Mkazi wa kijiji hicho, Alli Mfinanga, alisema Dk. Bilal akiwa ameongozwa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Mohongo na Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Felician Mramba, aliwatangazia wananchi kwamba kijiji hicho kimepata umeme wa mradi wa Rea na baada ya Makamu wa Rais kuondoka, waliambiwa wajiandae kuingiziwa umeme majumbani lakini cha kushangaza mradi huo uliyeyuka na kupelekwa Ghona.

“Tunamuomba mkuu wetu wa mkoa (Gama), aunde Tume ya Uchunguzi kwa sababu Dk. Bilal hakuwa kichaa, hadi aseme Kilototoni imepata mradi huu. Kama haukuwa wa kwetu kwa nini wamdanganye? Hapa tunaamini kuna mazingira fulani yametengenezwa; ndiyo maana wamechepusha mradi,” alisema Hafidh Hassan. Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji hicho, Robert Mosha, alisema mradi huo umetekelezwa nje ya matarajio yao licha ya ramani
kuonyesha kijiji hicho ndicho kilichopitiwa na umeme na badala yake kupitishwa kijiji kingine bila kushirikisha uongozi wa kijiji.

Akijibu madai hayo, Kaimu Meneja wa Tanesco mkoani hapa, Mhandisi,
Mathias Solongo, alisema mradi wa Rea, ulifanyiwa usanifu pamoja na tathimini mwaka 2009 wakati makazi ya wananchi wanaolalamika hayakuwapo.

“Huwa tunafanya tathimini kwa structure zilizopo na tunatekeleza mradi kwenye maeneo yaliyokuwa developed (yaliyoendelezwa). Wakati huo mradi huo ukifanyiwa Survey (Usanifu) kulikuwa hakuna makazi ya watu Kilototoni…Iweje sasa tutoe mradi hapo halafu tupeleke kule,” alisisitiza Solongo.

Mkuu wa mkoa huo, (Gama) alipotafutwa kwa njia ya simu ili kutoa ufafanuzi hakupatikana.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post