Wasira: Nyerere aenziwe kwa vitendo

Ofisi ya Rais Uratibu na Mahusiano, Stephen Wasira.
Watanzania wametakiwa kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa vitendo, kwa kuacha ubinafsi na kuwa waadilifu kama alivyokuwa yeye enzi za uhai wake kwa kusimamia misingi ya uzalendo.
Wito huo ulitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Uratibu na Mahusiano, Stephen Wasira, alipotembelea nyumbani kwa Baba wa Taifa eneo la Mwitongo kijiji cha Butiama.

Waziri Wasira alisema kuwa sasa baadhi ya watu wakiwamo baadhi ya viongozi, hawafuati misingi ya Baba wa Taifa, kwani wamekuwa wabinafsi na kutokuwa wazalendo wa kweli katika nchi yao, jambo ambalo kimsingi hawamuenzi.

Akizungumza na familia ya Baba wa Taifa, iliyowakilishwa na mtoto wake, Makongoro Nyerere, katika kikao chake na waandishi wa habari, Waziri Wassira alisema kuwa umoja na mshikamo wa Tanzania aliousimia hayati Mwalimu Nyerere kuanzia mwanzo, ulikuwa mfano kwa  Afrika na duniani kote kwa ujumla.

“Umoja na mshikamano ambao Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliusimamia kuanzia mwanzo pamoja na uzalendo wake kwa nchi yetu, ulikuwa ni mfano kwa Afrika nzima na duniani kote kwa ujumla, sasa kwa msingi huo tunatakiwa tumuenzi kwa vitendo,” alisisitiza.

 Aidha, Waziri Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda (CCM), alisema kuwa siku hizi  baadhi ya wananchi wakiwamo viongozi ni wabinafsi sana, jambo ambalo Baba wa Taifa hakulipenda kabisa enzi za uhai wake.

  Alisema kuwa kama Baba wa Taifa angekuwa mbinafsi, angelikuwa na mali nyingi na kuwa tajiri wa kutisha maana rasilimali zote zikuwa chini.
  "Sasa ni kwa nini baadhi ya watu wanashindwa kuiga mfano huo?," alihoji Wasira.

Aliongeza: “Uadilifu umekwisha kwa baadhi ya watu sasa hivi kila mtu anataka kuwa tajiri…Mwalimu mwenyewe hakutaka mambo hayo, alikuwa anaishi maisha ya kawaida kabisa, lakini kwa sasa mmomonyoko wa maadili na uadilifu kwa baadhi ya watu umekwisha."

  "Pale katika kambi ya Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Kiabakari kwa chini, kuna dhahabu, aliamua kuweka kambi pale na hata pale Buhemba sasa. Kama angekuwa mbinafsi, angechukua dhahabu hizo zote, lakini aliamua kuacha kwa ajili ya maslahi ya taifa letu na kwa faida ya kizazi kijacho,” alisema.

  Alisema kuwa ubinafsi huchangia kwa kiasi kikubwa kuwapo kwa mfarakano kwa wananchi kati ya aliyekuwa nacho na asiyekuwa nacho.

  Aliongeza kuwa kwa sasa kiwango cha uzalendo kinaendelea kushuka hapa nchini kwa baadhi ya watu, jambo ambalo ni hatari sana kwa sababu watu wa aina hiyo kimsingi wanashindwa kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم