Wassira: Upinzani ni vyama vya matukio

Waziri wa nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na Mahusiano) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bunda mkoani Mara Stephen Wassira
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais (Uratibu na  Mahusiano) ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bunda mkoani Mara  Stephen Wassira, amesema kwamba vyama vya upinzani ni vya matukio.
Wassira alitoa kauli hiyo juzi wilayani Tarime wakati wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa.

Wassira alisema kwamba wapinzani walitumia muda mrefu kuzungumzia sakata ya wizi wa fedha katika akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kutoka ndani Bunge kwenda kupinga mchakato wa Katiba mpya na sasa wamejikita katika nyimbo za sakata ya wizi wa fedha za akaunti ya Tegeta Escrow katika BoT na Escrow na kupinga ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za kata.

Wassira ambaye alihutubia mkutano wa kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uwanja wa mpira mjini Tarime akiwa na Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine na Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Elias Mpanda  na Katibu Mwenezi wa Wilaya, Sospeter Samson, alisema vyama vya upinzani vimekuwa vikiibuka wakati wa uchaguzi na baada ya hapo havisikiki.

Kuhusu hali ya usalama wilayani Tarime, Wassira alisema:  “Wananchi mnakumbuka wilaya yenu ilivyokuwa wakati wa miaka 2005 hadi 2010 wakati Chadema iliposhinda ubunge na baadhi ya madiwani. Vita vya koo vilidumu kwa muda huo kutokana na kushindwa kuongoza na amani ilitoweka , sasa mnaona tangu CCM imeshinda jimbo hili la Tarime amani imerejea na Maendeleo mnayaona wenyewe.”

Aliongeza:  “Barabara zinapitika, shule zinaendelea kujengwa na maabara, wapinzani wanadai hakuna kuchangia maabara, shule bila maabara haijakamilika… masuala ya Escrow wanahubiri jambo hili na kuwahimiza wananchi kuipinga CCM bila kujua na kuwafahamisha Escrow kiini chake nini wanafuata mkumbo hawa watu ni vyama vya matukio.”

“Suala hili (Escrow) lipo kwa Rais wa nchi, yeye hawezi kushinikizwa na wapinzani kutoa maamuzi, amewapa watu wake kuchunguza zaidi naye atatoa maamuzi sahihi baada ya kuridhia taarifa yote ya Bunge.  CCM haikurupuki kama wanavyodhania wapinzani,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

Previous Post Next Post