Dar/mikoani. Uchaguzi wa Serikali za Mitaa jana
ulilazimika kuahirishwa katika baadhi ya maeneo nchini, kutokana ama na
kukosewa kwa majina ya wagombea, baadhi yao kuwekewa nembo za vyama
wasivyotoka au uhaba wa vifaa vya kupigia kura.
Mikoa iliyoripotiwa baadhi ya vijiji, mitaa na
vitongoji vyake kushindwa kupiga kura ni Dar es Salaam, Manyara,
Kilimanjaro, Tanga na Mwanza hali iliyozua malalamiko kutoka kwa
wananchi waliojitokeza.
Waandishi wa gazeti hili waliripoti kuwa kati ya
saa 4.30 asubuhi na saa sita mchana, masanduku na vifaa vingine vilikuwa
havijafika katika baadhi ya vituo, hali iliyowakatisha tamaa baadhi ya
wananchi hivyo kuanza kuondoka huku katika baadhi ya maeneo wakiamua
kusubiri hadi kieleweke.
Dar es Salaam
Maeneo ambayo uchaguzi huo umeahirishwa katika
Mkoa wa Dar es Salaam ni Mtaa wa Sharif Shamba Ilala, Gerezani na mitaa
yote ya Vingunguti.
Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Sharif Shamba, Rose
Magina alisema: “Uchaguzi umeahirishwa hadi Jumapili ijayo (Desemba 21)
baada ya kukosekana kwa karatasi za kupigia kura.”
Waandishi wetu walipokuwa katika mtaa huo walikuta
kituo cha kupigia kura kikiwa kimefungwa, huku kukiwa na tangazo
linaloeleza tarehe ambayo uchaguzi utafanyika.
Katika mitaa ya Gerezani Mashariki na Gerezani
Magharibi, ambako baadhi ya watendaji waliokuwa katika Ofisi za Kata ya
Gerezani walisema vifaa vilivyotolewa vilikuwa vichache kuliko idadi ya
watu waliojiandikisha na kwamba uchaguzi huo utafanyika tena Desemba 20,
mwaka huu.
Uchaguzi pia uliahirishwa katika mitaa yote ya
Kata ya Vingunguti baada ya kikao kilichowahusisha wagombea wote, huku
Ofisa Mtendaji Kata hiyo, Protas Tarimo akisema utafanyika Jumapili
ijayo.
Mitaa hiyo ni Miembeni, Butiama, Mji Mpya,
Mtakuja, Majengo, Kombo, Mtambani na Faru. Wagombea wa vyama vinavyounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walimtupia lawama ofisa mtendaji
huyo kwa kukubali kupokea karatasi za kupigia kura zikiwa pungufu na
kusababisha uchaguzi huo kuahirishwa.
Wakazi wa Mtaa wa Machimbo, Ugombolowa, Segerea
nao walikumbana na sintofahamu hiyo baada ya kufika katika kituo cha
kupigia kura alfajiri, lakini mpaka saa nne asubuhi hakukuwa na dalili
zozote- Mwananchi
Post a Comment