Wazawa wanunua nusu ya hisa Tanzanite One


Arusha. Kampuni ya wazawa ya uchimbaji wa madini ya Sky Associates Group (LTD) imenunua asilimia 50 ya hisa zilizokuwa zinamilikiwa na Kampuni ya Richland Resources ya Uingereza ndani ya Tanzanite One katika migodi ya Kitalu C cha machimbo ya Tanzanite, Mererani, Wilaya ya Simanjiro.

Hisa za kampuni hiyo ambayo imekuwa ikichimba madini ya Tanzanite Mererani tangu mwaka 1992 zimenunuliwa kwa kiasi cha Sh32 bilioni ikiwa ni madai mbali mbali ya kodi na mikataba iliyokuwa imeingiwa na kampuni hiyo.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Hussein Gonga alisema hisa nyingine za asilimia 50 za mgodi huo zitaendelea kumilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Stamico.

Alisema Kampuni ya Richland Resources imeamua kuuza hisa zake zote 100 kwa kufuata sheria za ununuzi kimataifa.

Hata hivyo, alisema wafanyakazi wote 700 wa kampuni hiyo, wataendelea na ajira zao sambamba na utawala uliokuwapo kutokana na makubaliano yaliyoafikiwa na kampuni hizo.

“Tunawaomba Watanzania waliokuwa wameajiriwa na Kampuni ya Tanzanite One wasiwe na hofu, ajira zao zitalindwa kwani lengo la kununuliwa kampuni ni kuongeza uzalishaji na pato la taifa,” alisema.

Naye mkurugenzi mwenza wa kampuni hiyo, ambaye pia ni mfanyabiashara maarufu wa madini jijini hapa, Faisal Juma Shahbhai, alisema wanatarajia kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa sekta ya madini.

“Tunaahidi kuendeleza miradi ya kijamii Mererani na Naisinyai pamoja na kuboresha biashara ya Tanzanite na mazingira yake kwa jumla,” alisema.

Kampuni ya Tanzanite One ilikuwa inamiliki leseni ya uchimbaji madini (SML 8/92) kwa asilimia 100 kabla ya Serikali kuingia ubia kutokana na kutekeleza matakwa ya kisheria ya uchimbwaji wa madini ya vito.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post