Arusha. Kampuni ya wazawa ya uchimbaji wa madini ya Sky
Associates Group (LTD) imenunua asilimia 50 ya hisa zilizokuwa
zinamilikiwa na Kampuni ya Richland Resources ya Uingereza ndani ya
Tanzanite One katika migodi ya Kitalu C cha machimbo ya Tanzanite,
Mererani, Wilaya ya Simanjiro.
Hisa za kampuni hiyo ambayo imekuwa ikichimba
madini ya Tanzanite Mererani tangu mwaka 1992 zimenunuliwa kwa kiasi cha
Sh32 bilioni ikiwa ni madai mbali mbali ya kodi na mikataba iliyokuwa
imeingiwa na kampuni hiyo.
Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Hussein
Gonga alisema hisa nyingine za asilimia 50 za mgodi huo zitaendelea
kumilikiwa na Serikali kupitia Shirika la Stamico.
Alisema Kampuni ya Richland Resources imeamua kuuza hisa zake zote 100 kwa kufuata sheria za ununuzi kimataifa.
Hata hivyo, alisema wafanyakazi wote 700 wa
kampuni hiyo, wataendelea na ajira zao sambamba na utawala uliokuwapo
kutokana na makubaliano yaliyoafikiwa na kampuni hizo.
“Tunawaomba Watanzania waliokuwa wameajiriwa na
Kampuni ya Tanzanite One wasiwe na hofu, ajira zao zitalindwa kwani
lengo la kununuliwa kampuni ni kuongeza uzalishaji na pato la taifa,”
alisema.
Naye mkurugenzi mwenza wa kampuni hiyo, ambaye pia
ni mfanyabiashara maarufu wa madini jijini hapa, Faisal Juma Shahbhai,
alisema wanatarajia kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wa sekta
ya madini.
“Tunaahidi kuendeleza miradi ya kijamii Mererani
na Naisinyai pamoja na kuboresha biashara ya Tanzanite na mazingira yake
kwa jumla,” alisema.
Kampuni ya Tanzanite One ilikuwa inamiliki leseni
ya uchimbaji madini (SML 8/92) kwa asilimia 100 kabla ya Serikali
kuingia ubia kutokana na kutekeleza matakwa ya kisheria ya uchimbwaji wa
madini ya vito.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق