Kujiuzulu kwa Werema kwapokewa kwa hisia tofauti

Aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema
Uamuzi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, kujiuzulu, baada ya kuhusishwa na kashfa ya kampuni ya IPTL ya wizi wa zaidi ya Sh. bilioni 300 katika akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), umepingwa na wananchi, ambao wamesema hakutakiwa kujiuzulu, bali alitakiwa afukuzwe kazi, kuchunguzwa na kisha kufikishwa mahakamani.Msimamo huo ulitolewa na wananchi wa kada mbalimbali nchini walipozungumza kwa nyakati tofauti jana.
KIBAMBA
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba, alisema Jaji Werema hakutakiwa kujiuzulu na kwamba, kama yeye (Kibamba) angekuwa Rais, angemkatalia kujiuzulu, badala yake, angemfukuza kazi, kisha angeamuru uchunguzi ufanyike kabla ya kumfikisha mahakamani.

Kibamba alisema kujiuzulu kunamfanya Jaji Werema astahili kulipwa mafao ya kustaafu kazi wakati kwa aliyoyafanya hastahili kupata mafao.“Kujiuzulu siyo adhabu, bali ni kupisha msongamano. Tunasubiri adhabu kwa Jaji Werema,” alisema Kibamba.

Alisema unafiki uliokitihiri serikali ndiyo unaowafanya vigogo wengine waliohusishwa na kashfa hiyo kusubiri kubembelezwa ndiyo nao wapeleke barua kwa Rais kuomba kujiuzulu.

“Siridhishwi hata kidogo na ninasononeshwa na ulegelege wa uongozi wa awamu ya nne. Katika siku mbili zijazo, Rais awafukuze kazi wote waliobaki. Rais Kikwete achukue hatua, watu wameanza kuchoka kusubiri, anarembaremba, anapaka rangi. Achukue hatua dhidi ya waliobaki,” alisema Kibamba.

MBOWE
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alihoji pongezi zilizotolewa na Rais kwa Jaji Werema na kusema huo ni mkakati wa kulindana.

Alisema kitendo hicho kinaashiria kutokuwapo dhamira ya kweli ya kuwachukulia hatua wote waliohusishwa katika kashfa hiyo na kuhoji uadilifu wa Jaji Werema aliosfiwa na Rais wakati ameshiriki katika kuliingiza taifa kwenye hasara.

“Ofisi ya Rais haiku pamoja na wananchi na Bunge, kwani watu wanaweza kuiba wakapongezwa,” alisema Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai (Chadema).

MNYIKA
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, alisema kitendo cha Rais Kikwete kumpongeza Jaji Werema aliyejiuzulu kwa tuhuma za uzembe na matumizi mabaya ya madaraka, kimedhihirisha udhaifu mkubwa upande wa ofisi ya rais.

“Na kwa vyovyote vile, Werema hakupaswa kupongezwa kwa kujiuzulu kwake. Amejiuzulu baada ya shinikizo, baada ya kutakiwa kujiuzulu kwa nyakati mbalimbali na kukataa kwa nyakati mbalimbali,” alisema Mnyika, ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo.

Alisema alitarajia Rais Kikwete badala ya kumpongeza kwa utumishi wenye uaminifu mtu, ambaye ana tuhuma za kukosa uaminifu, angemwambia pamoja na barua yako ya kujiuzulu, kimsingi alikuwa kwenye taratibu za kumfukuza kazi.

Mnyika alisema pia alitarajia Ikulu watangaze kwamba, sasa Jaji Werema akamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, kwa sababu hivi sasa kuna viongozi wa serikali walioko mahakamani kwa kesi za uzewmbe na kuisababishia serikali hasara.

LILIAN LIUNDI
Kaimu Mkurugenzi wa Mtandao wa Kijinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi, alisema Jaji Werema alitakiwa kuwajibishwa, badala ya kujiuzulu na kuhoji sababu za kutochukuliwa hatua wengine wote waliohusishwa na kashfa hiyo.

ASKOFU KALLINGA
Askofu wa Kanisa la Bethel River of Life Ministries Tanzania, Nickson Kallinga, alimpongeza Jaji Werema kusikiliza maoni kutoka sehemu mbalimba na kusema uamzi huo ni wa busara na kujiuzulu kwake hakufanyi kuwa yeye ni mkosefu sana.

“Tendo alilolifanya Jaji werema ni la busara. Na kama jamii itamhitaji itasema na pia uamuzi huo ni wa kuheshimika na umeonyesha ukomavu wa uongozi, ambao viongozi wanatakiwa kuiga,” alisema Kallinga.

TAHLISO
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (Tahliso), Mussa Mdede, alisema kutokana na Jaji Werema kulidanganya  Bunge kuwa fedha ya Escrow siyo ya umma, alitakiwa ajiuzulu hata kabla ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kutoa ripoti na mapendekezo yake.

Alisema uamuzi wake umechelewa, lakini isiishie kujiuzulu tu, bali ashitakiwe mahakamani na fedha zirudishwe hata ikiwezekana kwa kufilisiwa au kwa namna yoyote ile.

MUKOBA
Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Gratian Mukoba, alisema watu wote waliohusika na kashfa hiyo wanapaswa kutimuliwa.
Alisema uongo wao kwamba, fedha hizo hazikuwa za umma sasa umedhihirika, hivyo hakuna sababu ya wengine kupata kigugumizi cha kujiuzulu na kutaka walizoiba zirudishwe zote.

“Sioni sababu ya wengine kuwa na kigugumizi cha kujiuzulu, kwani huo ni ushujaa, kuwa umefanya bila kukusudia kuwa ni mali ya umma,” alisema Mukoba.

SHINYANGA
Wakizungumza na NIPASHE jana, baadhi ya wananchi wa mkoa wa Shinyanga, walisema kujiuzulu kwa Jaji Werema ni jambo lililochelewa, lakini wale waliouguswa na sakata hilo wanatakiwa kufuata mkondo.

John Mwita, ambaye ni mkazi wa mjini Shinyanga, alisema maamuzi aliyoyachukua Jaji Werema ni mazuri, lakini viongozi wengine waliohusika na kashfa hiyo wanatakiwa kujiachia ili kukisafisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Werema kafanya maamuzi mazuri, ingawa kachelewa. Nampongeza kwa hilo. Lakini nawasihi mawaziri Sospeter Muhongo, Anna Tibaijuka na katibu mkuu wizara nishati na madini, Eliakimu Maswi, wamuige Werema,” alisema Mwita.

Masumbuko Kumalija, ambaye ni mkazi wa mjini Shinyanga, alisema kujiuzulu kwa kiongozi huyo hakutoshi, bali kinachotakiwa ni kurejesha fedha zilizochukuliwa ili zitumike katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

GEITA
Baadhi ya wananchi wa mjini Geita, wamepongeza hatua ya Jaji Werema ya kujiuzulu na kuomba mawaziri wengine kuiga.Sylvester Mwita, ambaye ni mkazi wa mjini Geita alisema wote waliotajwa katika tuhuma hizo kila mmoja awajibike.

Mwita, ambaye ni msomi, alisema Jaji Werema ameonyesha ujasiri wa kujiuzulu, lakini bado vyombo vingine vinayo fursa ya kutumia mamlaka yake kuweka ukweli wazi na kuondoa ushabiki iwapo hakuna mashaka au kuna mashaka ielezwe bayana mazingira husika ili asiyehusika asionewe na anayehusika awajibike.

Mashauri Luchagula kwa upande wake alimuomba Rais Jakaya Kikwete kuwachukulia hatua wote waliotajwa, lakini baada ya kujiridhisha ili kuepuka kuwajibishwa wasiohusika.
Alisema hatua ya Jaji Werema ni ya kiungwana.

Mkulima wa Kata ya Busanda, wilayani Geita, Emmanuel Petro, akizungumzia kashfa hiyo, alisema watu wengi wa vijijini hawana ufahamu wa kina kuhusiana na Escrow hivyo kama kuna mtu kajiuzulu kwa kula pesa ni jambo jema.

MWANZA
“Japokuwa amechelewa kujiuzulu, lakini ni vizuri amejiwajibisha kwa jambo ambalo na wengine waliotuhumiwa wanatakiwa kulifanya kuliko kusubiri kuwajibishwa,” alisema John Innocent wa Kiseke.

Innocent alisema mawaziri Prof. Muhongo na Prof. Tibaijuka, kwa kuwa wanahusika na kashfa hiyo moja kwa moja wanatakiwa wajiuzulu na wala wasisubiri kuwajibishwa.
Pia alisema licha ya kujiuzulu, serikali inatakiwa kuzuia mali zote za watuhumiwa wa wizi huo na kisha kufikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

LOISULIE
Mwenyekiti wa Umoja wa Wnataaluma katika Chuo Kikuu Cha Dodoma (Udom),Paul Loisulie, alisema anaamini Jaji Werema ameshauriwa kujiuzulu ili kumrahisishia Rais
Kikwete kazi ya kutekeleza maazimio ya Bunge.

Alisema watu nchini na nje ya nchi kwa sasa wanachosubiri ni kuona maazimio yaliyopitishwa na Bunge, Novemba 29, mwaka huu yanatekelezwa na mamlaka kuu ya uteuzi nchini.

Loisulie alisema siyo siri kwamba utata wa kushughulikia sakata zima la kashfa hiyo unatokana na kuwapo mawazo kinzani miongoni mwa wanasiasa na jamii kwa jumla, kwa kuwa baadhi wanaamini wanaotakiwa kuwajibika wameonewa.

Hata hivyo, alisema namna bora ya kushughulikia na kumaliza suala hilo ili hali ya hewa kisiasa nchini ibaki salama, ni kutekeleza maazimio ya Bunge kama yalivyopitishwa kwa kuwa yalitokana na maafikiano ya pande zote; yaani serikali, chama tawala na vyama vingine vya kisiasa vinavyowakilishwa bungeni.

KABUTARI
Kayumbo Kabutari, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chaumma),alisema hiyo ni hatua ya kwanza, ambayo inapaswa kufuatiwa na kuamriwa kurejesha fedha zilizochotwa kwenye akaunti hiyo.

Alisema kauli ya Jaji Werema kwamba ushauri wake haukueleweka vizuri, haupaswi kutumiwa na mamalaka kuu ya uteuzi, kama kigezo cha kulinda wezi.Alitahadharisha kuwa hilo likitokea, jamii haitaafiki kirahisi na kwamba, anahofia itaweza kusababisha mgawanyiko na migomo ya hapa na pale katika shughuli za ujenzi wa taifa.

“Sote tunafuatilia, kujiuzulu kwake kama ni kwa kushauriwa, kulazimishwa au kuamua mwenyewe, haituhusu ila tunachotaka ni fedha zilizokuwa kwenye akauti ya Escrow na kuchukuliwa wakati zilitakiwa kuwa za Tanesco na malipo ya VAT, irudishwe na wote waliohusika katika sakata hili,” alisema Kabutari.

ALISTIDES
Mwesigwa Alistides, ambaye ni mfanyabiashara wa Dodoma alisema sababuiliyoelezwa na Jaji Werema kuwa ndicho chanzo cha kujiuzulu kwake inatia aibu, kwa kuwa haiingii akilini kwamba, mamlaka zote zilizochunguza tukio hilo, watumishi wake hawana akili ya kuelewa mbichi, mbivu na mbovu za kinachoitwa ‘ushauri wake.

“Kama ameamua kujilipua kwa kigezo hicho ili ionekane kwa kuwa yeye ndiye aliyepotosha wahusika wote, anajidanganya. Kila mtu aadhibiwe kwa kosa lake kama Bunge lilivyoshauri,” alisema Alistides.

DOUGLAS
“Hata hivyo, pamoja na kujiuzulu sasa, alichelewa. Hatua hiyo alipaswa kuichukua mapema sana wakati kashfa hii ilipoibuka na kuonyesha wazi kuwa yeye alishindwa kusimamia majukumu yake ya kazi ipasavyo. Hivyo hivyo na kwa Prof. Tibaijuka na Muhongo,” alisema Douglas Raymond, ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu Eckernford jijini hapa.

AMBROSY
Mary Ambrosy, ambaye ni mwanasheria wa kujitegemea, alisema inasikitisha kuona viongozi wa Tanzania wanakosa uzalendo kwa ajili ya kulinda heshima yao na maslahi ya nchi, hasa pale wanapojua kabisa kwamba, walichangia kwa namna moja au nyingine kupoteza imani ya wananchi kwa serikali yao.

Imeandikwa na Muhibu Said, Thobias Mwanakatwe, Enles Mbegalo, Leonce Zimbandu, Isaya Kisimbilu, Dar; Daniel Mkate, Mwanza; Marco Maduhu, Shinyanga; Renatus Masuguliko, Geita; Editha Majura na Augusta Njoji, Dodoma na Lulu George, Tanga.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم