Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo
Kijana huyo, Batholomew Edward, alipigwa risasi alipokuwa akisubiri matokeo ya uchaguzi huo wa mtaa wa Majengo mjini Nzega, baada ya kundi la wananchi wa mjini kuandamana kutokana na utata wa matokeo.
Aidha, polisi wanadaiwa kumjeruhi kwa risasi mtu mwingine, Lucas Daudi, wakati wa kutawanya wananchi waliokuwa wakisubiri matokeo hayo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, amethibitisha kupigwa risasi kwa kijana huyo katika tukio lililotokea siku ya uchaguzi Desemba 14, mwaka huu na kwamba ilikuwa ni bahati mbaya risasi ilimpata wakati polisi wakipiga mabomu na risasi za moto kujihami kutoka kwa waandamanaji.
Alisema siku ya uchaguzi majira ya usiku wakati msimamizi wa uchaguzi anasubiri kutangaza matokeo ya uchaguzi wa mtaa wa Majengo, mashabiki wa vyama walijikusanya na kuanza kurusha mawe baada ya kuona matokeo yamechelewa na kuharibu mali za serikali.
Kutokana na hali hiyo, alisema polisi walilazimika kupiga mabomu ya kutoa machozi, lakini wananchi hawakutii amri na ndipo waliporusha risasi za moto hewani na moja ikampata marehemu Edward.
“Polisi walipoona waandamaji hawatii amri, risasi za moto zilipigwa hewani na katika purukushani, mtu mmoja Batholomew Edward, alijeruhiwa kwa risasi na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya Nzega, lakini bahati mbaya alifariki dunia siku iliyofuata," alisema Kaganda.
Kutokana na mauaji hayo, wananchi walifanya maandamano yaliyoanzia katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega kuchukua mwili wa marehemu huyo na kupita katika mitaa mbalimbali ya mji wa Nzega.
Wakati wa maandamano hayo, wananchi walilaani vikali mauaji hayo na kuwaomba viongozi wa juu wa jeshi hilo kuchukua hatua kali za kinidhamu dhidi ya askari aliyefanya mauaji hayo.
Maandamano hayo ya wananchi yaliongozwa na viongozi wa vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutoka hospitali hadi nyumbani kwa marehemu mtaa wa Musoma na ibada fupi ilifanyika kabla ya kuusafirisha mwili huo nyumbani kwao mkoani Kigoma kwa maziko.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tabora, Francis Msuka, alimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake kwa askari waliompiga risasi mwananchi huyo.
Msuka akizungumza na wananchi nyumbani kwa marehemu, alisema kuwa Jeshi la Polis lisitumike kisiasa kukilinda chama tawala kwani jukumu lake kulinda raia na mali zao na siyo kuua.
Alisema kuwa vijana waliopigwa risasi kimsingi hawakuwa na hatia yoyote kwa sababu walikuwa wanasubiri matokeo yatangazwe ambayo yalichelewa kiasi cha kuwatia wasiwasi wananchi kwamba huenda kulikuwa na hujuma zilizokuwa zikifanyika.
Naye Diwani wa Nzega mjini, Domick Kizwalo, alisema ili kurejesha imani kwa wananchi kwa jeshi hilo, serikali ihakikishe inachukua hatua dhidi ya askari waliotekeleza mauaji hayo.
Alisema ni kosa kwa Jeshi la Polisi kutumiwa na CCM wakati chama hicho kimeshindwa kuwaletea maendeleo wananchi.
Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Nzega, Omary Omary, alisema wapo baadhi ya watu wanapenda uongozi lakini hawajui kuongoza na kuwataka wananchi kufanya mabadiliko ya kupata viongozi makini ambao wataweza kuongoza jamii kwa makini kwa kufuata taratibu na kanuni.
MABOMU YARINDIMA BUSEGA
Wakati huo huo, mabomu ya kutoa machozi yaliyorindimishwa na Polisi wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kwa saa tano katika kata ya Lamadi, wilayani Busega, mkoa wa Simiyu, yalisababisha wananchi kuathirika kwa kutofanya shughuli zozote juzi.
Shughuli zote katika eneo hilo zilisimama kutokana na polisi hao kusambaratisha vikundi vya wafuasi wa Chadema waliokuwa wakipinga wagombea wa nafasi ya uenyekiti kuenguliwa.
Hata hivyo, makundi ya wananchi yaliwapa wakati mgumu FFU kuwadhibiti. Inadaiwa sababu za wafuasi wa Chadema kuandamana ni kushinikiza kurejeshwa kwa wagombea 18 wa chama hicho walioenguliwa kwa sababu ya kukosea kujaza fomu za kugombea.
Wafuasi wa Chadema wanailalamikia serikali kwa kuenguliwa wagombea wao wa serikali ya kijiji na kuwabakisha wajumbe.
Mkuu wa Wilaya ya Busega, Paul Mzindakaya, alisema kulingana na taratibu, sheria na kanuni za uchaguzi za serikali za mitaa, vijiji na vitongoji, mgombea anatakiwa kudhaminiwa na chama chake pale anapogombea nafasi yoyote.
“Vipengele hivyo ndivyo vimewaondoa wagombea wa Chadema katika kata ya Lamadi…kama mlinzi wa amani na usalama, nimewaamuru polisi wadhibiti vurugu eneo hili,” alisema Mzindakaya.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Simiyu, Charles Mkumbo, alisema wamewakamata watu 149 kutokana na vurugu hizo.
Imeandikwa na Thobias Mwanakatwe,Dar; Halima Ikunji, Nzega na Shushu Joel, Busega
CHANZO:
NIPASHE
إرسال تعليق