Bagamoyo. Anguko la bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia
huenda likaifanya Serikali kupitia upya baadhi ya mikataba ya utafutaji
wa mafuta na gesi ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi.
Akiwasilisha mada katika warsha ya siku mbili
iliyoandaliwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) mjini
hapa jana, kaimu mkurugenzi wa mikakati wa shirika hilo, Dk Wellington
Hudson alisema hali hiyo inawatia wasiwasi na ikiendelea, shughuli za
utafutaji mafuta na gesi zitaathirika.
Alisema upitiaji wa mikataba mara nyingi hufanywa
kutokana na mabadiliko ya sheria, kuimarisha vipengele vya makubaliano,
kuongezeka kwa ugunduzi katika vitalu na mwenendo wa soko la mafuta
ghafi linalozidi kuyumba.
“Mwaka 2013 tulifanya mapitio ya mkataba wa
kugawana mapato (MPSA) baada ya kugunduliwa kwa maeneo mengi katika
ukanda wa Afrika Mashariki yenye kina kirefu, ikiwamo Tanzania mwaka
2010 na nchi jirani za Msumbiji, Uganda na Kenya,” alisema Dk Hudson.
Alisema wakati wakifanya mapitio ya mikataba hiyo
mwaka 2013, wastani wa bei ya mafuta ghafi katika soko la dunia ilikuwa
ni Dola 100 za Marekani (Sh165,000) kwa pipa wakati hivi sasa imeshuka
hadi wastani wa Dola 61 (Sh100,650) kwa pipa.
Akizungumzia kushuka kwa bei hiyo kutakavyoathiri
sekta ya gesi nchini, kaimu meneja wa utafutaji mafuta na gesi, Kelvin
Komba alisema kampuni nyingi zinazotafuta mafuta na gesi nchini
hutegemea mapato kutoka kwenye faida ya mafuta wanayopata katika nchi
nyingine.
“Ikitokea bei ya mafuta imeshuka sana, itawafanya kupunguza gharama za uwekezaji katika utafutaji mafuta na gesi,” alisema.
Kaimu mkurugenzi wa uzalishaji, Dk Meshacky Kagya
alisema kuna kila dalili ya matumaini mapya kwa Tanzania kugundua mafuta
katika Ziwa Tanganyika siku zijazo.
kutokana na ukanda huo kuonyesha matokeo chanya ya nishati hiyo adhimu ulimwenguni.
alisema matumaini hayo yanatokana na nchi jirani
ya Uganda kugundua mafuta katika Ziwa Albert lenye jiolojia inayofanana
na ya Ziwa Tanganyika.
“Utafutaji mafuta katika Ziwa Tanganyika umekuwa
na changamoto nyingi kutokana na kuwa na kina kirefu kama cha bahari cha
wastani wa kuanzia mita 500 hadi 2,500. Na eneo lile lina kina takriban
mita 1,500 hivyo meli kubwa zaidi zinahitajika kufanya shughuli hizo,”
alisema Kagya.
Mpaka sasa kuna kampuni zinazoendelea kufanya
uchunguzi na kuna matumaini watakuja na matokeo mazuri licha ya kazi
hiyo kuhitaji mtaji mkubwa.
إرسال تعليق