Waziri Ghasia avionya vyama vya siasa

Dar/Mikoani. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia amevionya vyama vya Siasa nchini kutokuwa chanzo cha vurugu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Desemba 14, mwaka huu.

Waziri Ghasia alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa vyama vya siasa na msajili wa vyama, uliolenga kuweka makubaliano katika uchaguzi huo.

Ghasia alisema kuna baadhi ya viongozi wameshaanza kutoa matamko na kauli za vitisho kuwa wapo tayari kumwaga damu endapo hawataridhika na matokeo ya uchaguzi huo.

Alisema kauli za aina hiyo zinalenga kuchochea vurugu na hazipaswi kufumbiwa macho.

“Hiyo siyo kauli nzuri kama tuna nia ya kuijenga nchi yetu, nawasihi sana viongozi wa vyama vyote muwe wavumilivu na watulivu na mjiepushe kutoa kauli zitakazoweza kuchangia machafuko,” alisema.

Nchemba aagiza

Naibu Katibu mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba amewataka wananchi wa Musoma mkoani Mara kuacha tabia ya kuchagua viongozi kwa mazoea au kwa kutimiza wajibu.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Shule ya Msingi Mkendo mjini hapa kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mtaa mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema wananchi wengi hupiga kura kwa mazoea.

“Msichague viongozi kwa kushindanisha vyama mithili ya mechi ya Yanga na Simba, ushabiki wa aina hiyo ndiyo huwa chanzo cha kuwachagua viongozi wasio na sifa na wasiotambua wajibu wao kwa jamii,” alisema Nchemba.

Mgombea mlemavu

Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa kitongoji wilayani Magu mkoani Mwanza ambaye ni mlemavu wa macho, Maduhu Bugalale (60), ameshinda rufani yake baada ya kuwekewa pingamizi kwa madai kuwa hataweza kuona maandishi.

Bugalale alilalamikia kitendo cha Mtendaji wa Kijiji cha Kahangala, Glaciana Ikomba kumuondoa kuwania nafasi ya uenyekiti wa Kitongoji cha Ikelebelo kwa madai kuwa mtu asiyeona hataona wala kusoma maandishi.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post