Dar/Mikoani. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa
na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia amevionya vyama vya Siasa
nchini kutokuwa chanzo cha vurugu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa
utakaofanyika Desemba 14, mwaka huu.
Waziri Ghasia alitoa kauli hiyo jana alipokuwa
akifungua mkutano wa siku mbili wa vyama vya siasa na msajili wa vyama,
uliolenga kuweka makubaliano katika uchaguzi huo.
Ghasia alisema kuna baadhi ya viongozi wameshaanza
kutoa matamko na kauli za vitisho kuwa wapo tayari kumwaga damu endapo
hawataridhika na matokeo ya uchaguzi huo.
Alisema kauli za aina hiyo zinalenga kuchochea vurugu na hazipaswi kufumbiwa macho.
“Hiyo siyo kauli nzuri kama tuna nia ya kuijenga
nchi yetu, nawasihi sana viongozi wa vyama vyote muwe wavumilivu na
watulivu na mjiepushe kutoa kauli zitakazoweza kuchangia machafuko,”
alisema.
Nchemba aagiza
Naibu Katibu mkuu wa CCM Bara, Mwigulu Nchemba
amewataka wananchi wa Musoma mkoani Mara kuacha tabia ya kuchagua
viongozi kwa mazoea au kwa kutimiza wajibu.
Akihutubia mkutano wa hadhara katika Viwanja vya
Shule ya Msingi Mkendo mjini hapa kwenye uzinduzi wa kampeni za uchaguzi
wa viongozi wa Serikali za Mtaa mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema
wananchi wengi hupiga kura kwa mazoea.
“Msichague viongozi kwa kushindanisha vyama
mithili ya mechi ya Yanga na Simba, ushabiki wa aina hiyo ndiyo huwa
chanzo cha kuwachagua viongozi wasio na sifa na wasiotambua wajibu wao
kwa jamii,” alisema Nchemba.
Mgombea mlemavu
Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa kitongoji
wilayani Magu mkoani Mwanza ambaye ni mlemavu wa macho, Maduhu Bugalale
(60), ameshinda rufani yake baada ya kuwekewa pingamizi kwa madai kuwa
hataweza kuona maandishi.
Bugalale alilalamikia kitendo cha Mtendaji wa
Kijiji cha Kahangala, Glaciana Ikomba kumuondoa kuwania nafasi ya
uenyekiti wa Kitongoji cha Ikelebelo kwa madai kuwa mtu asiyeona hataona
wala kusoma maandishi.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق