Mgombea CUF amwekea pingamizi mgombea wa CCM

Chama cha Wananchi (CUF)
Chama cha Wananchi (CUF) mtaa wa Mchangani katika Kata ya Makumbusho, jijini Dar es Salaam kimemuwekea pingamizi mgombea uenyekiti wa wa serikali za mitaa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kitwana Katembo, kwa madai kuwa amejaza fomu ya kugombea ujumbe badala ya uenyekiti.
Mgombea uenyekiti wa CUF, Ismail Shamsidin, amesema kuwa tayari ameandika barua ya pingamizi kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa ambaye ni Msimamizi wa uchaguzi akiwa ameambanisha na vielelezo tangu Novemba 24, lakini hadi leo hajapata taarifa yoyote.

“Nimepeleka pingamizi langu kwa Afisa Mtendaji wa Mtaa na nakala kwa Afisa Mtendaji Kata, lakini hadi leo sijajibiwa, hii inanipa wasiwasi kuwa huenda kuna kitu kinataka kufanywa,” alisema na kuongeza:

“Ninachotaka mimi ni kutangazwa rasmi kuwa Mwenyekiti mpya wa Serikali za Mitaa wa Mchangani kwani hakuna mgombea mwingine yoyote zaidi yangu kwa sababu yule wa CCM ninayeambiwa kuwa anagombea uenyekiti yeye amejaza fomu ya ugombea ujumbe wa Kamati ya Mtaa tu,” alisema.

Mgombea huyo anadai kuwa anataka Afisa Mtendaji wa Mtaa amtangaze kuwa Mwenyekiti mpya kwa mujibu wa sheria na miongozo ya Tamisemi.

CUF imesema kuwa walipeleka barua yao Novemba 24 yenye kichwa cha habari kisemacho ‘pingamizi dhidi ya Kitwana Mohamed Katembo katika nafasi ya kugombea uenyekiti wa mtaa’ ambayo NIPASHE  limeiona.

Kwa mujibu wa mashuhuda, awali fomu za mgombea wa CCM zilizokosewa zilibandikwa kwenye ubao wa matangazo za kwenye ofisi za Afisa Mtendaji, lakini inadaiwa kuwa baadaye ziliondolewa.

Hata hivyo, uongozi wa CUF unasema kuwa kabla hata ya kuondolewa kwa nakala za fomu hizo walizipiga picha pale pale ili kuthibitisha kuwa kulikuwa na makosa.
Akizungumza kwa njia ya simu mgombea uenyekiti wa CCM alidai kuwa madai hayo ya CUF si ya kweli.

Lakini pia alikataa kuzungumzia kwa undani madai kuwa haruhusiwi na chama chake.

“Maadili ya chama changu hakiniruhusu kuzungumzia suala hili, mimi nasubiri tu hayo maamuzi kama wameweka pingamizi,” alisema.

Msimamizi wa uchaguzi wa mtaa, Mary Kiango, ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Mtaa alipoulizwa kama amepokea pingamizi hilo, alidai kuwa si msemaji na kwamba anayeweza kulizungumzia zaidi ni Mkurugenzi wa Manispaa.

Afisa Mtendaji wa Kata, Husna Nondo, alipopigiwa simu alisema kuwa yuko kwenye eneo ambalo hasikii vizuri kutokana na kuwa kwenye watu wengi.

Hata hivyo alipopigiwa tena baadaye simu yake haikupokelewa.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم