Dodoma. Wanafunzi 84 wa programu maalum ya stashahada ya ualimu
katika Chuo Kikuu cha Dodoma(udom) waliofanya mgomo na kuandamana
kushinikiza kulipwa madai yao, juzi wamepandishwa kizimbani kwa kosa la
kukusanyika bila kibali maalum.
Wanafunzi hao ni wa programu maalumu katika masomo
ya Sayansi, Hisabati na Teknohama iliyoanza mwaka jana walifanya mgomo
huo juzi na kuandamana kuelekea ofisi ya Waziri Mkuu kwa lengo la
kuwasilisha madai yao.
Akisoma mashitaka hayo mbele ya hakimu mkazi
mwandamizi mfawidhi wa Mkoa wa Dodoma Kabate Richard, mwendesha
mashitaka Lopa, aliiambia mahakama kuwa wanafunzi hao walitenda kosa
hilo juzi majira ya saa kumi na moja na nusu alfajiri.
Wanafunzi hao wamegawanywa katika makundi manne ya kesi namba 5, 6,7 na 8 ya mwaka 2015 ambapo wanakabiliwa na kosa hilo.
Hakimu huyo baada ya kesi hiyo kusomwa aliwapa
dhamana ambapo wanafunzi hao walijidhamini wenyewe kwa shilingi elfu
ishirini, ishirini kauli ya maneno.
Wanafunzi hao wapo nje kwa dhamana ambapo kesi zao zimepangwa kusikiliza tarehe 16-19 februari mwaka huu.
Kufuatia uvumi ulioenea katika mitandao mbalimbali
ya kijamii na katika mji wa Dodoma na viunga vyake kuwa kuna wanafunzi
waliofariki dunia kufuatia maandamano yaliyofanyika juzi katika Chuo
Kikuu cha Dodoma (Udom), Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa
wa Dodoma, Dk Nassor Mzee amesema kuwa taarifa hizo si za kweli.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake
jana mjini hapa, Dk Mzee amesema kuwa hakuna maiti yoyote ya mwanafunzi
wa Chuo Kikuu cha Dodoma iliyopokelewa katika hospitali hiyo na
kusisitiza kuwa taarifa hizo siyo za kweli.
“Hapa hospitalini hakuna maiti yoyote ya
mwanafunzi wa Udom na hata baada ya kupata taarifa hizo nilikwenda
mapokezi kwa ajili ya kupata taarifa na kwenye wodi zote hapa
hospitalini lakini hakuna mwanafunzi hata mmoja wa kutoka Udom aliyefika
hapa kutibiwa,” amesema Dk Mzee.
Aliongeza kuwa, “Hata kwenye chumba cha kuhifadhia
maiti hakuna maiti yoyote ya mwanafunzi wa udom… labda kama waliamua
kwenda kuzihifadhi maiti hizo kwenye hospitali nyingine nje ya hapa
lakini hapa hakuna maiti yoyote kutoka Udom.”
Awali baadhi ya wanafunzi waliokuwa kwenye
maandamano ya kudai fedha zao za kujikimu walidai kuwa kuna baadhi ya
wanafunzi wenzao waligongwa na gari ya polisi iliyokuwa ikitawanya
maandamano hayo ambayo polisi waliyaita ni haramu na kufariki dunia.
Pia katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
iliyotolewa juzi na jeshi la polisi haikutaja vifo wala majeruhi zaidi
ya kutaja idadi ya wanafunzi waliotiwa mbaroni kufuatia maandamano hayo
kuwa ni 84.
إرسال تعليق