Juzi, serikali ilitangaza kuwa imeshindwa
kuwachukulia hatua watumishi wa Idara ya Uhamiaji nchini waliohusika na
ajira 200 za upendeleo.
Tangazo hilo limekuja likiwa ni kinyume na Kamati ya uchunguzi
iliyoundwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ambayo ilisema
ilibaini kuwapo kwa kasoro kadha wa kadha katika utoaji wa ajira hizo
kwa nafasi za Konstebo na Koplo.
Hata hivyo, Msemaji wa wizara hiyo, Isaac Nantanga, alisema kuwa
watumishi hao wameshindwa kuchukuliwa hatua kutokana na kukosekana kwa
ushahidi wa wazi wa kuthibitisha tuhuma za upendeleo zilizoelekezwa
kwao.
Alisema ndugu na jamaa za maafisa hao, walikuwa na sifa za
kuajiriwa ndani ya idara hiyo na hivyo kukosekana kigezo cha
kuwachukulia hatua.
Hata hivyo, alisema Wizara ilitoa onyo dhidi ya waliohusika na
mchakato huo kutokana na kutoa mwanya wa kuzuka malalamiko kutoka kwa
wananchi kuhusiana na ajira hizo.
Ajira hizo zilitangazwa na Kamishna wa Uhamiaji katika Gazeti la
Serikali, Februari 17, mwaka jana na kutoa tangazo hilo kwenye tovuti ya
wizara na idara ya Uhamiaji.
Baada ya kutangazwa ajira hizo, maombi 15,707 yalipokelewa na waombaji 1,005 waliitwa katika usaili.
Kati yao, 200 walishinda na kuitwa kazini, lakini baada ya kutoa
tangazo la kuitwa kazini, malalamiko yalitolewa kupitia vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii kuwa walioitwa katika ajira hizo ni watoto
wa jamaa na ndugu.
Lakini kwa mshangao, Msemaji wa Wizara juzi alisema walioitwa
kazini, walistahili kuajiriwa kwani walikuwa na sifa na kwamba
walistahili kuomba mara ya pili kutokana na maombi kutokubagua na badala
yake zilingatiwa sifa tu.
Natanga alisisitiza kuwa malalamiko ya kuajiriwa ndugu na jamaa za
maafisa hao, hayakuwa na msingi wowote ila onyo la wizara limelenga
kuwatahadharisha waliohusika na mchakato huo ili tukio kama hilo
lisijirudie tena ndani ya idara hiyo.
Kwa mujibu wa Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
watumishi wa umma nao pia wanalindwa na sheria ya ajira na kwa msingi
huo hawawezi kufukuzwa kazi kwa kutuhumiwa tu ni lazima uthibitisho
uwasilishwe na mamlaka husika zijiridhishe.
Tunakubaliana na Msemaji wa Wizara kwamba waliohusika na mchakato
huo, hawawezi kufukuzwa kazi kwa kutuhumiwa tu, bali ni lazima
uthibitisho uwasilishwe na mamlaka husika zijiridhishe.
Tunasema hivyo kutokana na Tanzania kuheshimu utawala wa sheria.
Hata hivyo, pamoja na kukubaliana na Msemaji huyo, bado kuna mambo mengi ya kujiuliza.
Kwanza, baada ya kuibuliwa kwa tuhuma hizo, Agosti 22, mwaka jana,
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil, alizungumza na waandishi
wa habari jijini Dar es Salaam kuzungumzia sakata hilo.
Abdulwakil alisema baada ya waombaji wa nafasi hizo kufanyiwa
usaili na kuitwa kazini, ziliibuka tuhuma mbalimbali zilizotolewa na
baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.
Alifafanua kuwa tuhuma hizo zilihusu upendeleo wa ajira kwa ndugu na jamaa za watumishi wa idara hiyo.
Kutokana na hali hiyo, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,
ililazimika kusitisha ajira hizo na kuunda kamati ndogo ya watu watano
kwa lengo la kufanya uchunguzi wa kina kuhusu madai hayo.
Kamati hiyo ilifanya kazi kwa siku 10 kuanzia Agosti Mosi, mwaka jana na kutoa matokeo.
Katika uchunguzi wao, kamati hiyo ilibaini kuwa baadhi ya wasailiwa
waliolalamikiwa, walithibitika kuwa ni watoto wa ndugu au jamaa wa
watumishi wa idara hii.
Aidha, kamati hiyo pia iligundua kuwa baadhi ya waombaji wa nafasi
hizo, walikuwa na umri mkubwa zaidi ya ule uliotajwa kwenye matangazo ya
kazi.
Tangazo hilo la kazi lilieleza kuwa muombaji wa nafasi ya Konstebo anapaswa kuwa na umri wa miaka 25 na Koplo miaka 30).
Hali kadhalika, ilibainika kuwa baadhi ya wasailiwa waliopata alama
za juu katika ufaulu, hawakuitwa kazini na hakuna sababu maalum ambazo
zilitolewa.
Matangazo ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari, yalikuwa
ya jumla na hayakuainisha viwango na madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza
kidato cha nne na sita.
Kwa mantiki hiyo, Katibu Mkuu Abdulwakil, alitangaza ajira hizo zimefutwa na zitatangazwa upya.
Kauli ya juzi ya Msemaji wa Wizara, inakinzana na ya kamati
iliyoteuliwa kufanya uchunguzi wa suala hilo pamoja na msimamo wa Katibu
Mkuu.
Sasa sisi tunajiuliza, nani mkweli kati ya Msemaji wa Wizara na kamati teule?
Ikumbukwe kwamba michakato hiyo ya tangu kutangazwa kwa nafasi za
kazi, usaili na kuundwa kwa kamati hiyo, ilitumia fedha nyingi za walipa
kodi.
Kama wizara iliona kuwa hakukuwa na tatizo katika usaili huo, kulikwa na sababu gani ya kuunda kamati ya kuchunguza suala hilo?
Vilevile, kama usaili huo ulikwenda kwa mujibu wa taratibu,
kulikuwa na sababu gani za msingi za kuwaonya maafisa waliohusika na
usaili huo?
Tunasema hapa kuna jambo nyuma ya pazia na tunaingiwa na shaka kwamba kuna mchezo wa kuwalinda waliohusika na kashfa hii.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment