Kinara wa mtandao wa ujambazi katika Mikoa ya Kanda
ya Ziwa, Njile Samuel (46) maarufu John, amehukumiwa kifungo cha miaka
45 jela pamoja na kulipa faini ya Sh. milioni tatu baada ya kukiri
makosa yote mawili yaliyokuwa yakimkabili.
Mshtakiwa huyo alihukumiwa kosa la kwanza kifungo cha miaka 15 jela
na faini ya Sh. milioni tatu mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya
Wilaya ya Bariadi, Robert Oguda, baada ya kusomewa mashitaka yake.
Ilidaiwa katika shitaka la kwanza, Januari 10, mwaka huu, saa 9:00
alasiri, eneo la Lyoma wilayani Bariadi, Njile alikamatwa na risasi 272,
bunduki aina ya SMG na magazini saba.
Katika shitaka la pili lililosomwa mbele ya Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Aidan Mwilapa, mshtakiwa huyo alihukumiwa
kifungo cha miaka 15 kwa kupatikana na bunduki, huku kosa lingine
alihukumiwa kifungo kama hicho kwa kupatikana na umilikaji wa silaha
bila kibali.
Hata hivyo, adhabu hizo zitakwenda kwa pamoja na mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka 30 jela.
Wiki iliyopita, Makamanda wa Polisi wa Mikoa ya Mwanza, Simiyu,
Shinyanga, walikutana jijini Mwanza na kumuelezea Njile ni jambazi
hatari ambaye katika kazi yake alikuwa akiwaua wenzake baada ya kufanya
uhalifu.

Post a Comment