SELEMANI
Msindi, ndiye msanii wangu bora kabisa wa tungo za kiume, zinazopeleka
ujumbe moja kwa moja pasipo mafumbo na kama itabidi liwe fumbo, kwa
wanazuoni, ni rahisi mno kujua mlengwa.
Wengi wanamfahamu kama Afande Sele, kijana wa pale Morogoro ambaye
wakati f’lani akitafuta maisha, aliwahi kujaribu kupata ajira katika
Jeshi la Polisi, chanzo hasa cha jina lake hili la kisanii. Kati ya
wasanii wakubwa ninaowafahamu kwa karibu kupitia kazi zao, huyu naye
yumo!
Kitu kimoja kizuri ni kwamba Afande Sele anajua vizuri lugha ya
Kiswahili, ndiyo maana tungo zake zimekuwa kielelezo cha msanii makini
anayejua nini anaimba, kwa ajili ya nani na kwa wakati gani.
Haikuwa ajabu alipotwaa taji la Mfalme wa Rhymes katika shindano la
pekee kuwahi kufanyika nchini. Nimefanya naye kazi kwa ukaribu,
ninamfahamu kwa kiwango cha kuridhisha. Ingawa ni mtu makini akiwa nyuma
ya mic, nje ya fani Afande anabaki kuwa mswahili tu kama tulivyo
waswahili wote, anacheka na kila mmoja na anawang’ong’a kila wakimpa
kisogo!
Ingawa mimi ni shabiki wa kweli wa Afande, mtu ninayemkubali sana,
huenda kwa sababu ya kuwa naye karibu kikazi, nimegundua tatizo lake
moja la msingi, kuna wakati, kwa sababu anazozijua mwenyewe, huamua
kuikwepa nafsi yake inayojulikana na kujivika asiyokuwa nayo.
Kwa hili, nimewahi kutofautiana naye mara kadhaa na ninachoshukuru,
hakikuwahi kuharibu ukaribu wetu. Afande anasema asichotenda na anatenda
asichosema! Wote tunajua, wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya
wamejitumbukiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya (Cocaine na Heroin)
na wapo rafiki na ndugu zetu wamepoteza maisha kwa kuhusishwa na jambo
hili, ingawa enzi za uhai wao, walikuwa wakikataa katakata kujihusisha
nalo.
Nimewahi kusema mara kadhaa, watu hawawezi kumzushia mtu kitu
kisichofanana na ukweli. Kwa mfano, tunao watu, ambao ni marafiki zetu,
ndugu zetu na hata wafanyakazi wenzetu, wanatajwa kuwa ni mashoga,
walevi, wezi na kadhalika. Hatuwezi kuamini moja kwa moja, lakini pia
hatuwezi kupuuza. Kwa nini watajwe wao na siyo wengine?
Hatuna ushahidi, lakini utapuuza vipi unaposikia kila siku watu
wanawataja Banzastone, Msafiri Diouf, Chid Benz, TID, Lord Eyez, Ray C
na wengine kuwa wanakula ‘sembe’?Juzi, nimesoma mahali, mshkaji wangu
Afande Sele akimtetea Daz Baba, yule mkali kutoka Kundi la Daz Nundaz,
aliyetamba na vibao vingi vikiwemo Umbo Namba Nane, Elimu Dunia na
kadhalika, kwamba kudhoofika kwake mwili hakutokani na utumiaji wa
madawa ya kulevya, bali ni unywaji pombe uliopitiliza.
Ninamfahamu Daz Baba na ninajua Afande na Daz Nundaz ni washkaji.
Anachofanya ni kujaribu kupooza sauti isiyokoma, inayopaza kuwa bwa’
mdogo anakula unga. Kama nilivyosema mwanzo, hatuna ushahidi, lakini kwa
nini tupuuze sauti hii, inayotolewa na watu wanaomfahamu?
Kumsaidia Daz Baba na wengine wanaotajwa ni kuwaambia ukweli kuwa
wanapoteza mwelekeo. Tuwaambie kuwa wanachokifanya sasa ni ujanja wa
kizamani, ambao umewapoteza watoto wengi wa Kariakoo, Magomeni,
Kinondoni, Mwananyamala, Ilala na Temeke, ambao leo hii wamekuwa
ombaomba kwa watu ambao wakati wanaingia mjini kutafuta maisha, wao
waliwaita wakuja!
Kwa hiyo ningetegemea Afande Sele, siku moja aachie kibao kinachowataja washkaji zake wabwia unga, akiwataka waache, kwa ajili ya Tanzania salama!
Kwa hiyo ningetegemea Afande Sele, siku moja aachie kibao kinachowataja washkaji zake wabwia unga, akiwataka waache, kwa ajili ya Tanzania salama!
Post a Comment