Mkuu wa Mkoa wa Dodoma akerwa na tabia ya wananchi wa mkoa huo kujigeuza "Omba Omba"


MKUU wa mkoa wa Dodoma Chiku Gallawa ametaka wananchi wa mkoa wa Dodoma kuachana na tabia yenye aibu ya kuomba chakula wakati wana fursa za kuzalisha chakula cha kutosha, kujikimu mwaka mzima na ziada kuifanyia biashara.
 
Alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa wiki wilayani Kondoa wakati alipokuwa akizindua msimu wa kilimo mwaka 2015 kwa mkoa wa Dodoma.
 
Aliwataka wananchi kutambua msimu wa kilimo, umeanza kwa hiyo wao na familia zao wajikite kwenye kufanya kilimo ili wafanikishe azma ya kutokua ombaomba wa chakula kila mwaka.
 
Katika uzinduzi huo, ambapo pia alishiriki kwenye upandaji, Mkuu wa mkoa alifuatana na baadhi ya wakuu wa wilaya za mkoa wa Dodoma, viongozi wa halmashauri zote za wilaya mkoa wa Dodoma na wataalamu wa kilimo kutoka wilaya zote.
 
Uzinduzi huo wa kilimo umefanyika kwa vitendo katika kijiji cha Damai Kondoa. Gallawa alitumia nafasi hiyo pia kuwaagiza wakurugenzi wa halmashauri za wilaya za Dodoma, kuhakikisha kwenye kila kijiji kunakuwa na Daftari la Kilimo na Mifugo, ambalo litakuwa linatunza taarifa muhimu za shughuli za kilimo na mifugo zinazofanywa na wananchi vijijini.
 
Akijibu hoja ya changamoto ya soko la mazao wanayozalisha wananchi wa Dodoma, Gallawa aliwataka wataalamu wa Serikali ya Mkoa na Wilaya wa masuala ya biashara, kilimo, ushirika na masoko wawe wanakaa mapema kabla ya msimu wa kilimo kuanza ili watafute masoko, ikiwezekana hata utaratibu wa kilimo cha mkataba na kuwaelekeza wakulima mazao ya kulima kabla hata ya msimu.
 
Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma, Rehema Madenge alibainisha kuwa uzinduzi wa Msimu wa Kilimo Kimkoa, umekuwa ukifanyika kwa miaka mitatu mfululizo kweye wilaya za Kongwa, Chamwino na Bahi na malengo yake ni kuhamasisha wananchi kanuni za kilimo bora.
 
Mshauri wa Kilimo mkoa wa Dodoma, Bernard Abraham aliahidi yeye na wataalamu wenziwe wa kilimo, wataendelea kubuni mikakati zaidi ya kunyanyua kilimo mkoani Dodoma

Post a Comment

Previous Post Next Post