Serengeti. Polisi mkoani Mara imesema
itawachukulia hatua askari watakaobainika kuhusu katika kifo cha Samson
Nyakiha (70) baada ya uongozi wa jeshi hilo kukutana na ndugu wa
marehemu waliotelekeza maiti katika Kituo cha Polisi cha Wilaya.
Kamanda wa upelelezi wa makosa ya jinai wa mkoa,
RCO Rogathe Mlasani alitoa ahadi hiyo katika kikao cha pamoja cha ndugu
na uongozi wa polisi wa Wilaya ya Serengeti na kisha kutangaza kwa
wananchi waliokuwa wamekusanyika katika kituo hicho tangu Alhamisi
kusubiri hatma ya suala hilo.
Katika tukio hilo, mwili wa Nyakiha aliyefia
Hospitali ya Rufaa ya Bugando ulichukuliwa na ndugu ambao waliupeleka
kituo hicho cha polisi na kuutekeleza, wakidai ndugu yao aliuawa
kutokana na kupigwa na askari.
RCO Mlasani alisema tukio hilo si la kawaida kwa
kuwa limesababisha kupoteza uhai wa mtu na haliwezi kuvumiliwa kwa kuwa
limekiuka misingi ya haki za binadamu.
Aliwaomba wananchi wawe watulivu wakubali kuchukua mwili wa marehemu wakazike.
“Naomba mliamini Jeshi la Polisi kwa kitendo kama
hiki hakuna atakayelindwa, wote watachukuliwa hatua kulingana na makosa
waliyoyatenda. Kwa hili hatutamlinda mtu maana kila mmoja anajua mipaka
ya kazi yake,” alisema.
RCO alisema kuanzia sasa jalada la uchunguzi wa
tukio hilo analichukua yeye na litakuwa la kifo cha shaka na upelelezi
huo umehamishiwa ofisi yake.
Alisema hatua za kipolisi zinaanza haraka kwa
askari wa Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) na polisi waliohusika na
wakati huo taarifa ya kifo itakuwa inasubiriwa na baada ya hapo hatua
zaidi zitachukuliwa kwa watakaothibitika kuhusika bila kujali nyadhifa
zao.
Ndugu wa marehemu wakiongozwa na Wakili Stephen
Magoiga, walimtaka RCO kutoa taarifa ndani ya wiki moja kuhusu hatua
zitakazokuwa zimechukuliwa na watu gani wamehusika.
Nyamaisa Damas (40), mke mdogo wa marehemu alisema
Novemba 16, 2014 saa 12:00 asubuhi kundi la askari lilimvamia mumewe na
kufanya upekuzi na kuchukua silaha na risasi alizokuwa anamiliki
kihalali na wakachukua simu yake.
Alisema askari hao waliondoka naye akiwa mzima na baadaye ghafla alisikia mumewe amelazwa hospitali na hajitambui.
Hata hivyo, kwenye jalada Mug/Ir/31/74/2014
alilofunguliwa Nyakiha linaeleza kuwa alikutwa na ngozi tano za nyumbu,
mavi ya tembo, bangi, bunduki aina ya shortgun na risasi zake. Alieleza
kuwa anamiliki bunduki kihalali na kwamba shuhuda ni mkewe, lakini
polisi walikataa maelezo hayo.
إرسال تعليق