Na Maelezo
Makamu
wa Pili wa Rais Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema serikali
inahamasisha wanawake kujiendeleza kinadharia na kivitendo ili kushiriki
kikamilifu katika kujenga uchumi wa kisasa unaohitaji wafanyakazi wenye
ujuzi wa maarifa ya sayansi na teknolojia kwa lengo la kijikwamua
kiuchumi.
Akizungumza
huko Kibokwa Kinyasini Wilaya ya Kaskazini A Unguja katika sherehe za
uwekaji wa Jiwe la Msingi wa Kituo cha Kufundishia Wanawake Utengenezaji
wa Vifaa vya Umeme wa Jua Amesema serikali imeanzisha kituo hicho ili
wanawake waweze kupiga hatua kubwa zaidi na kuonyesha uwezo wao ndani na
nje ya nchi.
Amesema
lengo la kituo hicho ni kuendeleza rasilimali watu kwa kuwajengea uwezo
na kuwawezesha wanawake wa vijijini kutengeneza vifaa vinavyotumia
umeme wa jua vikiwemo taa, mashine na majiko ya kupikia kwa lengo la
kujikwamua kimaisha.
Mhe
Balozi amesema kituo hicho kinatarajia kuwajengea uwezo wa kitaalamu
wanawake 16 kutoka katika vijiji 8 vitakavyochaguliwa kwa kila nusu
mwaka na baadae kueneza ujuzi huo kwa wanakijiji wenzao watakaohitaji
huduma hiyo.
“Mpango
huu utawawezesha wanawake wa vijijini kuondokana na umasikini na
kuwawezesha kiuchumi na hivyo kuyafikia malengo ya Dira ya 2020 na
Mkuza”, amesema Balozi Seif.
Aidha
Balozi Seif ameeleza kuwa ujuzi na elimu ndivyo vitakavyowawezesha
wananchi kufikia uchumi wa kisasa na kutambua uwezo na nguvu kubwa ya
wanawake katika mageuzi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Amefahamisha
kuwa kituo hicho kitakua ni cha kwanza cha aina yake Afrika Mashariki
Kusini na Kati ambacho kinatarajiwa kuwajengea uwezo wa kitaalamu
wanawake wa vijiji mbalimbali.
Mradi
huo wa kituo cha mafunzo ya wanawake ya kutengenezea vifaa vya umeme wa
jua unatekelezwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya
India kupitia Chuo cha Barefoot cha India na Washirika wa Maendeleo UN
Women ambao umegharimu shilingi milioni 400 za kitanzania.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI ZANZIBAR
Post a Comment