Dar es Salaam. Agizo la kumwandikia barua 
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wasira ya 
kumtaka kurejesha nyumba ya bodi hiyo, limetekelezwa baada ya barua hiyo
 kuwasilishwa kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC).
Agizo hilo lilitolewa na kamati hiyo chini ya 
Mwenyekiti wake Zitto Kabwe kwa Bodi ya Sukari Tanzania (SBT) ikitaka 
Wasira arejeshe nyumba hiyo.
“Bodi tuliiagiza imwandikie barua Wasira na nakala
 ya barua hiyo watuletee leo (jana), tayari wameileta hivyo tunasubiri 
utekelezaji,” alisema Zitto na kuongeza: “PAC haina ugomvi na Wasira 
bali Serikali ambayo inatakiwa kumlipia kodi waziri wake na siyo kukaa 
katika nyumba ya umma bila kulipia kodi.”
Januari 16, mwaka huu, PAC ilikutana na Bodi ya 
SBT na iliieleza kamati kwamba tangu 2010, Wassira amekuwa akiishi 
katika nyumba hiyo iliyoko Masaki na wakimtaka kuirejesha hakukuwa na 
utekelezaji wowote.
Wasira alinukuliwa na gazeti hili juzi akisema, 
“Mimi ni waziri, nina haki zangu, PAC haihusiki na mtu binafsi wala siyo
 ofisa ya mahesabu.”
Wakati huohuo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya 
alitolea ufafanuzi ukata unaozikabili halmashauri nchini na Serikali 
ikishutumiwa kutopeleka fedha.
Alisema halmashauri husika zinatakiwa kuboresha vyanzo vyake vya mapato badala ya kuitegemea Serikali Kuu.
“Kuna changamoto kama za wafadhili kutokutoa fedha
 lakini na halmashauri zenyewe zinatakiwa kuhakikisha zinaimarisha 
ukusanyaji wa mapato ya ndani na badala ya kutegemea kwa asilimia 100 
fedha kutoka serikalini,” alisema Mkuya.
Akizungumzia mafanikio ya mfumo mpya wa ulipaji wa
 mishahara ya watumishi wa umma, alisema umefanikiwa kuwabaini watumishi
 hewa 12,000 na kuokoa zaidi ya Sh400 milioni.
- Mwananchi

إرسال تعليق