MKURUGENZI wa Benchmark Production, Madame Rita
Poulsen, amelia na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), chombo cha
serikali kinachosimamia utamaduni kwa ujumla, akilielezea kuwa halina
msaada wowote kwa shindano la kutafuta na kuibua vipaji vya wasanii wa
muziki nchini, linalofahamika kama Bongo Stars Search (BSS).
“Tunalipa fedha BASATA kwa ajili ya shindano, tunatoa ajira nyingi
kwa vijana na kubadili maisha yao, wasanii tunaowaibua ndio hao hao
wanaotumika katika shughuli nyingi za Serikali, lakini ajabu, hatuna
msaada wowote tunaopata toka kwao, ikifika fainali wanataka tiketi
nyingi za bure (complimentary), lakini tuliposhindwa kulifanya hili
shindano mwaka jana, hata simu tu ya kutuuliza sababu, au hata salam
hatupati,” alisema Rita.
Shindano la BSS halikufanyika mwaka jana kutokana na wadhamini
kushindwa kutoa taarifa mapema ya kutoendelea na udhamini wao, lakini
mwaka huu, Rita Paulsen amesema watafanya kila wanachoweza kuhakikisha
linafanyika.
إرسال تعليق