Dar es Salaam. Kamati Ndogo ya Maadili ya CCM
leo inaketi kutoa hatima ya makada wa chama hicho waliotajwa kuhusika
katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kikao hicho kitakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa
CCM - Bara, Philip Mangula kama ilivyoagizwa na Kamati ya CCM
iliyokutana wiki iliyopita.
Walioitwa katika kamati hiyo ni aliyekuwa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ambaye
ni mjumbe wa Halmashauri Mkuu (NEC) na Kamati Kuu ya CCM (CC) pamoja na
wajumbe wa NEC, Andrew Chenge (Mbunge wa Bariadi Magharibi) na William
Ngeleja (Sengerema).
Kwa kuwa uamuzi wa CC unasisitiza utekelezaji wa
maazimio ya Bunge, kwa vyovyote unamlenga pia Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo ambaye mpaka sasa amewekwa kiporo.
Kamati Kuu iliyofanyika Januari 13, mwaka huu
Zanzibar iliazimia kuwa hatua za kimaadili zichukuliwe kwa wote
waliohusika na ukiukwaji wa maadili kwenye sakata la Escrow ambao wako
kwenye vikao vya uamuzi vya CCM.
Pia kikao hicho kiliitaka Serikali kuendelea
kutekeleza maazimio ya Bunge kuhusu sakata hilo ambalo lilikiweka chama
hicho katika wakati mgumu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa
uliomalizika hivi karibuni.
Kutokana na azimio hilo, Ngeleja, Profesa
Tibaijuka na Chenge wanakabiliwa na adhabu ya kuvuliwa nyadhifa
walizonazo ndani ya vikao vya amuzi vya CCM.
Makada hao walitajwa bungeni kuwa walipokea
mamilioni ya shilingi kutoka katika akaunti ya VIP Engineering
inayomilikiwa na James Rugemalira. Chenge na Profesa Tibaijuka walipokea
Sh1.6 bilioni wakati Ngeleja alipokea Sh40.4 milioni.
Hata hivyo, Ngeleja anayetajwa kutaka kuwania
urais anaweza kukumbwa na adhabu nyingine iwapo atabainika kuwa
alikwenda kinyume na adhabu aliyopewa pamoja na wenzake watano ya
kuhusishwa na ukiukwaji wa maadili kwenye mchakato wa kutaka kuteuliwa
na chama hicho kugombea nafasi hiyo.
Adhabu hiyo aliyopewa Ngeleja pamoja na Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye,
January Makamba, Bernard Membe na Stephen Wasira inamalizika Februari
mwaka huu na baada ya hapo itafanyika tathimini kuona kama walizingatia
masharti ya adhabu zao.
Kwa mujibu wa taarifa ya CC, ambao hawakuzingatia masharti wataongezewa adhabu.
Tayari uteuzi wa Profesa Tibaijuka umeshatenguliwa
na sasa Rais Kikwete anasubiriwa kumtangaza mrithi wake na kumalizia
‘kiporo’ cha Profesa Muhongo.
- Mwananchi
- Mwananchi
إرسال تعليق