Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimelaani vikali vurugu zilizofanywa
na wafuasi wa Chadema na CUF kwa viongozi wa serikali za mitaa katika
maeneo kadhaa nchini ikiwemo mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam na Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa NEC;
Itikadi na Uenezi CCM taifa, Nape Nnauye amesema vurugu hizo mbali na
kuhatarisha na kuharibu mali pia zilizosababisha baadhi ya viongozi wa
CCM kujeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitali.
Amesema vurugu hizo zimetokea katika mkoa wa
Mwanza ambapo Christopher Mgeta kutoka Mtaa wa Ibungilo na Pascal
Charles wa Mtaa wa Kitangiri A katika wilaya ya Ilemela walivamiwa na
kupigwa wakati wa kuapishwa.
Alieleza kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam,
Sultan Jeta wa mtaa wa Ukwamani katika jimbo la Kawe alifanyiwa fujo na
wafuasi hao na Mtaa wa Msisiri A Kata ya Mwananyamala katika Jimbo la
Kinondoni Juma Mbena alipigwa na kuvunjwa mkono.
“Katika Manispaa ya Ilala, wafuasi wa vyama vya
upinzani walifanya vurugu wakati wa kuapishwa kwa viongozi wa serikali
za Mitaa, jambo lililopelekea zoezi hilo kuahirishwa.
Nnauye amesema katika Mkoani Mbeya pia vurugu za
aina hiyo zimetokea katika wilaya za Kyela na Rungwe ambapo wilayani
Kyela zoezi la kuapisha viongozi wa serikali za mitaa lilishindika na
kuahirishwa kutokana na vurugu za kurushiwa mawe zilizofanywa na wafuasi
wa Chadema walioletwa kutoka katika maeneo mbalimbali ya Mkoa huo.
Aliongeza kuwa katika Kijiji cha Ilundo wilayani
Rungwe wafuasi hao wa Chadema waliwapiga mawe viongozi na wanachama wa
CCM na baadae kufyeka mashamba yao ya migomba na kusababisha vijana sita
kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya wilaya ya Rungwe kwa sababu
ya hasira za kushindwa uchaguzi.
“Vurugu hizi ni mwendelezo wa tabia na mazoea ya
vyama vya upinzani nchini kutoheshimu na kufuata sheria na taratibu za
nchi, tabia hizi si za kiungwana na ni uthibitisho wa kuharibikiwa na
kufa kwa vyama vya upinzani nchini. Mara zote wamekuwa wakikataliwa na
wananchi kwa kura, wao hukataa uamuzi huo wa wananchi kwa kufanya fujo
na vitimbi, ”amesema Nnauye.
Wakati haya ya kijiri kesho Sekretarieti ya
Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), itakutana Jijini Dar es
Salaam, kwa lengo la kupanga ajenda zitakazojadiliwa kwenye mkutano wa
Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama hicho itakayokutana
Zanzibar Januari 13.
Aidha msemaji wa jeshi la Polisi SSP Advera J.
Bulimba amesema jeshi hilo halitawaonea huruma wale wote watakaohusika
katika vurugu, kwani litawachukulia hatua kali za kisheria, badala yake
limewaasa wananchi ambao hawakuridhika na uchaguzi huo kufuata taratibu
husika.

إرسال تعليق