CUF yagangamala, 30 kortini

Dar es Salaam. Wakati wafuasi 30 wa CUF jana walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kukaidi amri halali ya polisi na kufanya maandamano bila ya kibali, chama hicho kimesema kitaendelea kuenzi siku ya kukumbuka wenzao waliofariki wakati wa machafuko Zanzibar mwaka 2001.
CUF ilitoa tamko la kuendelea na maandamano na mikutano ya hadhara jana kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika ofisi za makao makuu ya chama hicho na baadaye alasiri wafuasi hao 32 walifikishwa mahakama kwa mashtaka hayo matatu yanayohusu maandamano ya kuadhimisha mauaji ya wenzao waliokuwa wakipinga matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Zanzibar mwaka 2000.
Wakili wa Serikali, Joseph Maugo alidai katika shtaka la kwanza kuwa washtakiwa walikula njama za kufanya uhalifu Januari 27,2015 wakiwa Temeke na kwamba katika shtaka la pili washtakiwa 28 kati ya 30 walikusanyika isivyo halali kwenye ofisi ya CUF karibu na Hospitali ya Wilaya ya Temeke na kufanya maandamano kuelekea Zakhem, Mbagala.
Katika shtaka la tatu, ambalo nalo pia linawakabili washtakiwa 28, inadaiwa siku hiyo hiyo, wakiwa eneo la Mtoni Mtongani waligoma na kutojali tangazo halali la polisi la kuwazuia kuandamana na kukusanyika.
Washtakiwa wanaokabiliwa katika kesi hiyo ni Shabani Ngurangwa (56), Shabani Tano(29), Shabani Abdallah (40), Juma Mattar (54), Muhamed Kirungi (40), Athuman Ngumwai (40), Shaweji Mohamed(39), Abdul Juma(40), Hassan Said (37), Hemed Joho (46) na Mohamed Ibrahim (31).
Wengine ni Issa Hassan (53), Allan Ally(53), Kaisi Kaisi (51), Abdina Abdina (47), Allawi Msenga (47), Mohamed Mtutuma (33), Salehe Ally (43), Abd Hatibu (34), Bakari Malija (43), Abdallah Ally(32) , Said Mohamed (40), Salim Mwafisi, Salehe Rashid (25), Abdallah Said(45),Rehema Kawambwa (47), Salma Ndewa (42), Athuman Said (39).
Washtakiwa Dickson Leasson (37) na Nurdin Msati (37) hawahusiki katika shtaka la pili na tatu.
Washtakiwa hao kwa pamoja walikana mashtaka yote na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika. Hakimu Emilius Mchauru, ambaye aliahirisha kesi hiyo hadi leo, alimtaka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja ambaye atasaini dhamana ya Sh 100,000. Hata hivyo, washtakiwa hao wamepelekwa mahabusu hadi leo ili kutoa nafasi kwa upande wa mashtaka kukagua barua za wadhamini.
Naye Ibrahim Yamola anaripoti kuwa CUF imesema itaendelea kufanya maandamano na mikutano ya hadhara kila ifikapo Januari 26 na 27 kuadhimisha mauaji ya wanachama wake.
Maadhimisho ya mwaka huu yalizuiwa na Jeshi la Polisi.
Makamu mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji, ambaye pia aliingia matatizoni wakati wa machafuko hayo ya mwaka 2001, alisema hakuna ubaya wowote kuwaenzi na kuwakumbuka wapendwa wao.
“Jeshi la Polisi linatakiwa kutambua kwamba kila Januari 26 na 27 tutaendelea kufanya mikutano na maandamano, kama hawataki kuelewa hilo, wakae mkao wa mapambano na wananchi kila mwaka,” alisema Haji.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post