Waziri wa Fedha akiri udhaifu Bandari

Dodoma. Waziri wa Fedha, Saada Mkuya amesema, Serikali itabadilisha kanuni kwa malengo mahususi ya kudhibiti misamaha ya kodi.
Waziri Mkuya alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu hoja zilizowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe kuhusu Ripoti ya Ukaguzi Maalumu wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Alisema Serikali itapitia misamaha ili kuhakikisha ile isiyokuwa na tija inaondolewa.
Akizungumzia suala la wafanyakazi wa Mamlaka Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kujilipa posho za safari kiasi kikubwa, Mkuya alisema walikuwa wakijilipa tangu Septemba mwaka 2009 bila kupata kibali cha Msajili wa Hazina kitu ambacho ni kinyume na utaratibu.
“Hivi sasa tunaidhinisha sisi wenyewe na mashirika yote ya umma yanatakiwa kupata kibali cha Msajili wa Hazina,” alisema.
Waziri Mkuya alisema ili kuhakikisha kunakuwapo na ufanisi katika hilo, watendaji wote wa Msajili Hazina wataondolewa kwenye bodi za mashirika ambako ni wajumbe ili kusiwe na mwingiliano wa kimasilahi.
Kuhusu tatizo la mtaji katika Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), alisema Serikali inalishughulikia na kwamba italipa deni la Sh22.5 bilioni zilizoelezwa na kamati.
Kuhusu deni la mashirika ya hifadhi za jamii ambalo Serikali inadaiwa, Waziri Mkuya alisema Serikali ina mpango wa kuuza bondi zake ili iweze kulipa deni hilo lakini akasema hiyo itakuwa baada ya kupeleka waraka wa kusudio hilo kwenye Baraza la Mawaziri.
Serikali za Mitaa
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia akijibu hoja za Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) alisema hatua mbalimbali zimechukuliwa katika mikataba ambayo haina masilahi kwa halmashauri.
Pia, alisema ili kudhibiti ununuzi usiozingatia sheria katika halmashauri, Serikali imeandaa mafunzo kwa wanunuzi wote ili wajue Sheria za Ununuzi na wale wasiozingatia watachukuliwa hatua.
Alisema kutokana na matatizo katika halmashauri mbalimbali nchini, Serikali imewavua madaraka wakurugenzi 21, wakurugenzi watano wamefikishwa mahakamani, 27 wamepewa onyo, pia watumishi 233 wamefukuzwa kazi na 277 wamefikishwa mahakamani, huku 10 kesi zao zimekwisha na wengine wamefungwa na wengine kulipa faini.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post