Dk.Shein:Tofauti za Kisiasa na Vyama Zisitufanye Kukiuka Taratibu na Sheria za Kuendesha Shughuli za Kisiasa.

---
---
STATE HOUSE ZANZIBAR

OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
    Zanzibar                                                                                                 11 Januari, 2014
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesisitiza tena umuhimu wa viongozi wa kisiasa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa katika kuendesha shughuli zao za kisiasa na kuwa tofauti za vyama isiwe sababu ya viongozi hao kukiuka utaratibu na sheria hizo.
Akizungumza mara baada ya kupokea matembezi ya vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) katika viwanja vya Mnanzi Mmoja mjini Unguja jana ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi Dk. Shein alisema kuwa “tofauti za kisiasa na vyama zisitufanye tukakiuka utaratibu wa kisheria uliowekwa”
Alibainisha kuwa Zanzibar inaendeshwa kwa misingi ya kidemokrasia kwa kufuata Katiba na sheria zilizopo huku kukiwa na vyombo vya kusimamia sheria na utoaji haki kwa kila mwananchi.
Dk. Shein ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar aliwakumbusha wanasiasa kutumia mfumo uliopo wa vyama vya vingi kushindana kwa sera na hoja na kuepuka maneno ya kuwatisha wananchi na kuwatia hofu.
Alibainisha kuwa kumekuwepo na ushirikiano mzuri katika uendeshaji wa Serikali iliyo chini ya mfumo wa Umoja wa Kitaifa hivyo kuhoji kulikoni baadhi ya viongozi wakiwa nje ya serikali wanafanya mambo tofauti.
“Tumekuwa tukishirikiana vyema katika serikali kulikoni huko? Kwa nini baadhi wanasahau utamaduni wa uongozi, lugha za viongozi na wajibu wao katika jamii”alihoji Dk. Shein.

Kwa hivyo aliwaambia mamia ya vijana kuwa yeye binafsi hatishiki na maneno yanayosemwa na baadhi ya watu wanaodai ‘nchi yao’ kwa kuwa anaendesha nchi kwa mujibu wa Katiba na Sheria.
“Nchi hii ni yetu sote na tunaiendesha kwa misingi ya utawala bora na katika utendaji wangu natenda haki kwa mujibu wa Katiba na Sheria” Dk. Shein alisema.
Dk. Shein aliwaeleza mamia ya vijana na wananchi waliohudhuria hafla hiyo kuwa anashangaa kama wanavyoshangaa wananchi wengine wa Zanzibar kauli za baadhi ya watu visiwani hapa wanaodai kutaka ‘nchi yao’ huku akihoji nchi hiyo walimkabidhi nani.
“watuambie wamempa nani nchi yao kwa kuwa sisi Zanzibar mwanzoni tulikuwa tukijitawala wenyewe tukavamiwa na Wareno na baadae wakaja Waomani huku wakahamiwa na waingereza. Wazee wetu wakafanya mapinduzi kuirejesha nchi mikononi mwa wenyewe baada ya njia za kawaida kushindikana”Dk. Shein alieleza.
Aliwataka watu hao kusubiri uchaguzi kwa kuwa ndio njia pekee iliyopo sasa kupata madaraka nchini huku akiwatahadharisha kuwa Chama cha Mapinduzi kiko imara kuhakikisha kuwa kinaendeleza historia yake ya kushinda uchaguzi na kushika dola.
Aliwaambia vijana kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 halikuwa tukio la kupita bali mchakato uliotokana na madhila makubwa waliyokuwa wakifanyiwa wananchi wazalendo wa Zanzibar na utawala wa sultani uliokuwa ukihamiwa na Waingereza.
“Baada ya Afro Shirazi kunyimwa ushindi katika kila chaguzi na uamuzi wa Muingereza kuipa Zanzibar ‘uhuru’ chini ya Sultani wazee wetu hawakuwa na namna bali kufanya mapinduzi kuirejesha nchi mikononi mwa wananchi” Shein alisema.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Dk. Shein aliwakumbusha wananchi kitendo cha kuhuzunisha cha utawala wa kikoloni cha kuwalazimisha wananchi wa Zanzibar kwa vitisho kuhudhuria sherehe za kumkabidhi Sultani nchi yao.  
“’Uhuru’ ule uliwasononesha sana wazee wetu na sisi (tukiwa watoto) tulilazimishwa kuhudhuria sherehe huku tukitishiwa hata kufukuzwa skuli kama hatukuhudhuria” alisema Dk. Shein na kuvuta hisia za vijana na viongozi waliohudhuria halfa hiyo.
Aliongeza kuwa lengo la mapinduzi ilikuwa ni kuleta usawa na haki kwa kila mwananchi kinyume na utawala wa sultani ambao ulijengwa chini ya misingi ya kibaguzi ya kila aina.
Kwa hivyo waliwapongeza Umoja wa Vijana wa CCM kwa kuandaa matembezi hayo ambayo yanapeleka ujumbe moja kwa moja kwa wapinga mapinduzi kuwa wenye Mapinduzi wapo na wanayathamini na kuyalinda.
Mapema Mwenyekiti wa UVCCM Sadifa Juma Khamis alisema matembezi hayo ya vijana ni mchango wao wa kuimarisha na kuyaenzi Mapinduzi ya mwaka 1964 ambapo vijana wenzao wa Afro Shirazi walijitwisha jukumu kubwa la kuwakomboa wananchi wa Zanzibar dhidi ya uonevu na udhalimu wa wakoloni wa kisultani.
“Umoja wa vijana wa Afro Shirazi ulifanya wajibu wake wa kuleta Mapinduzi na sisi tunafanya wajibu wetu wa kuyalinda, kuyatetea na kuyaenzi” alieleza Mwenyekiti huyo.
Sadifa alieleza kuwa UVCCM unashangazwa na baadhi ya watu ambao aliwaita mabaki ya sultani kuendelea ‘kuidai’ Zanzibar tofauti na wakoloni wengine ambao baada ya kuondolewa hawarudi tena kudai nchi ilizozitawala hivyo kuwaonya watu hao kuwa kamwe hawawezi kurudi kuitawala Zanzibar.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar Shaka Hamdu Shaka alisema vijana 600 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania Bara walishiriki matembezi hayo yaliyoanza tarehe 6 Januari huko katika kijiji cha Unguja Ukuu katika Mkoa wa Kusini Unguja.
Alieleza kuwa matembezi hayo yalipita katika wilaya zote saba za kichama katika kisiwa cha Unguja na kuwapa nafasi vijana kujifunza na kutoa ujumbe wa Mapinduzi kwa wananchi kuhusu historia, malengo na mafanikio yaliyopatikana hadi sasa.
Katika maelezo yake alizidi kueleza kuwa katika vituo vya mapumziko vijana walijielimisha pia kuhusu Katiba iliyopendekezwa na kupata ufafanuazi wa vipengele mbalimbali vya Katiba hiyo hatua ambayo imewaongezea ufahamu zaidi ya Katiba hiyo.
Naibu Katibu Mkuu huyo aliwaeleza vijana na wageni walioshiriki hafla hiyo kuwa UVCCM imepanga kuifufua tena Jumuiya ya vijana Chipukizi wa CCM (young pioneers) kwa kufanya uzinduzi rasmi tarehe 01 Machi mwaka huu.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822 

Post a Comment

أحدث أقدم