Efatha: Mamlaka ya Tanganyika irejeshwe

Naibu Waziri wa Maendeleo, Jinsia na Watoto, Dk. Pindi Chana.
Kanisa la Efatha, limefanya maombi maalumu likitaka kurejeshwa mamlaka kamili ya Serikali ya Tanganyika, ambayo ilifutwa na  kuundwa Tanzania baada ya Muungano kati yake na Zanzibar mwaka 1964.
Maombi hayo yalinguruma usiku wa mkesha wa mwaka 2015, uliofanyika makao makuu ya Efatha, yaliyopo Kibaha mkoani Pwani na kuhudhuriwa na maelfu ya waumini.

Miongoni mwa walioshiriki ibada hiyo ni pamoja na Naibu Waziri wa Maendeleo, Jinsia na Watoto,  Dk. Pindi Chana na Waziri wa Utalii na Maliasili, Lazaro Nyalandu ambaye ni mmoja wa viongozi CCM ambao wametangaza nia ya kugombea urais.

Maombi ya kudai Tanganyika yalifanywa kwa viongozi wa Efatha kutoka mikoa yote, kupanda Madhabahuni na kueleza idadi ya watu, wilaya, kata, vijiji na vitingoji vilivyo kwenye maeneo yao na kutoa sababu za kudai mamlaka ya Tanganyika.

Mmoja wa wawakilishi wa mkoa wa Ruvuma, akiongoza wenzake alisema wakazi wa mkoa huo ni miongoni mwa waliokuwa mstari wa mbele kutetea uhuru wa makabila mbalimbali na Watanzania kwa ujumla.

"Kutokana na historia hiyo, hatuko tayari kupoteza utambulisho wetu wa asili na kutawaliwa na wageni, tumedhamiria kutokaa kimya mbele za Mungu mpaka serikali ya Tanganyika itakaporejeshewa mamlaka yake,"alisema.

Naye kiongozi wa wawakilishi wa mkoa wa Tanga, alisema wameazimia kumuomba Mungu aingilie kati, kurejesha serikali hiyo kwa sababu bendera yake ndiyo iliyopandishwa wakati taifa likipokea uhuru kutoka kwa wakoloni.

"Tanganyika ndiyo asili yetu, ndiyo utambulisho wetu hatuko tayari kubeba laana ya kupoteza utambulisho wetu ambao uliondolewa kwa sababu za kisiasa," alieleza.

Alisema hawana wasiwasi na Mungu wanayemuamini, kwa kuwa ndiye muumbaji wa ardhi iliyopewa jina la asili Tanganyika na kwamba wanaamini serikali hiyo itarejea madarakani na kutambulika ndani na nje ya nchi.

Mwakilishi wa Kigoma  alisema ili serikali ya Tanzania iwe halali haina budi kurekebisha muundo wa Muungano, kwa kuainisha Tanganyika na Zanzibar, bila kuathiri asili ya nchi husika.

Pamoja na hayo, Kiongozi Mkuu wa Efatha duniani, Mtume na Nabii Josephat Mwingira, alitahadharisha wanasiasa wanaogombea urais wa Tanzania kutotumia njia chafu, ikiwamo ushirikina kwa lengo la kufanikisha azma yao.

"Atakayetumia ushirikina hata kama atapata nafasi hiyo, atakufa kabla ya kuingia Ikulu nimeishasema Tanzania haitaongozwa kwa nguvu za mapepo," alieleza.

Naye Waziri Nyalandu, akizungumza kwenye mkesha huo, saa 7:47 usiku alisema anaamini akipata kura moja kutoka kwa Mungu, hakuna atakayemshinda hata kama wengine watatumia rushwa, kiasi cha watu kubeba rumbesa za fedha.

"Tena wakati nikishiriki kuimba na kusifu pamoja na wanakwaya, nikashuhudia kwamba watakuwa miongoni mwa watakaotumbuiza, Novemba mwaka huu Mungu atakapojitwalia utukufu nchini Tanzania," alieleza Nyalandu.
 

Post a Comment

Previous Post Next Post