Faini ya Sh10,000 ya ngono ni dhihaka

Dar es Salaam. Ni usiku na giza limetanda. Nakatiza mitaa ya Buguruni Madenge na Malapa jijini Dar es Salaam, nashuhudia wanawake wamejilaza kwenye vibaraza, mbele ya nyumba zao wakitumia mwanga wa vibatari.
Akili inanikumbusha simulizi zilizoenea mjini kuhusu kuwapo wanawake wanaojiuza kwa mtindo huo na baada ya kuchunguza, nabaini ukweli kwamba hao waliojilaza, wapo kazini wakisubiri wateja wa biashara ya ngono. Wanawake hao wa makamo, wengi wakiwa na umri wa kuanzia miaka 15 na hadi zaidi ya 35, huanza shughuli hiyo baada ya jua kuzama, pia wanatoa huduma hiyo hata wakati wa mchana bila kujali kuwa wanachofanya ni kosa kisheria.
Wanawake hao ni sehemu ya maelfu ya wanawake wengi wanaojihusisha na biashara hiyo haramu jijini Dar es Salaam.
Ingawa hakuna takwimu sahihi kuhusu idadi ya wanawake wanaofanya biashara hiyo, ukweli ni kwamba wanawake hao, maarufu kama machangudoa au madada poa, wametapakaa maeneo mengi jijini Dar es Salaam.
Maeneo yanayosifika kwa biashara hiyo ya ukahaba ya madanguro ni pamoja na Mwananyamala, Tandika, Temeke, Keko, Buguruni, Mbagala na Sokota.
Taarifa zinaonyesha kuwa kwa danguro la Sokota, wanaotafuta wanawake kwa ajili ya ngono hawahitaji kuumiza vichwa kutokana na kuwapo kwa kundi kubwa la mabinti ambao huvalia mavazi ya aibu, wakiwa nusu utupu, hali ambayo wanaamini kuwa huvutia wateja wao.
Hata hivyo, mamlaka husika zimeshindwa kudhibiti vitendo hivyo kwani hajizachukua hatua stahiki kukomesha hali hiyo.
Mwaka 2013, Jeshi la Polisi Kinondoni lilitangaza kufunga madanguro yaliyopo Mwananyamala na kuwakamata wasichana 35 waliokuwa wakiuza miili yao pamoja na mama wa miaka 72 ambaye anadaiwa kuwa ndiye mmiliki wa madanguro hayo na kuwafikisha mahakamani.
Hata hivyo, baadhi ya madanguro hayo, yamefunguliwa na kina dada poa wanaendelea kufanya kazi.
Uchunguzi wa gazeti hili katika baadhi ya maeneo umebaini wanawake hao wamekuwa wakiwatoza wateja wao ya Sh3,000 hadi Sh5,000 kwa tendo moja la ngono.
Hata hivyo, bei zinatofautiana na huwa kubwa zaidi kwa wale wanaofanya ngono kinyume na maumbile. Ukiondoa wanaume wakware, uchunguzi umebaini wanafunzi nao ni wateja wazuri wa wanawake hawa.
Kuna aina mbili za wanawake wanaouza miili yao. Kundi la kwanza ni la wale wanaoendesha biashara hiyo katika vyumba maalumu walivyopanga mitaani na jingine ni la wazururuaji. Hawa huonekana wakirandaranda barabarani, hasa nyakati za usiku wakitega wateja au katika klabu za pombe na nyumba za wageni maarufu kwa kazi hiyo.

Post a Comment

أحدث أقدم