Fifa watua kuchunguza waamuzi

Dar es Salaam. Ujumbe maalumu wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) umetua nchini kwa siri kuchunguza tuhuma za upangaji matokeo unaowakabili waamuzi watatu waliosimamishwa tangu mwaka jana.
Waamuzi hao, Jesse Erasmos, Hamis Chang’walu na Oden Mbaga ambao awali walikuwa na beji ya Fifa, walisimamishwa kwa tuhuma ambazo hazijawekwa wazi.
Julai 24 mwaka jana, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi alitangaza kuwasimamisha waamuzi hao kwa tuhuma za kupanga matokeo, ambazo hakuziweka wazi.
“Waamuzi hao waliosimamishwa na TFF pamoja na watu wengine watahojiwa na ujumbe huo wa Fifa na matokeo ya uchunguzi huo, yatatangazwa na Fifa wenyewe baada ya shughuli hiyo kukamilika,” alisema Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura.
“Tunaendelea kuwahimiza wanafamilia wa mpira wa miguu nchini wazidi kuzingatia kanuni za maadili za TFF, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na zile za Fifa katika utendaji wao. Fifa kwa upande wake itahakikisha kuwa haki inatendeka katika uchunguzi ambao inaufanya,” alisema.
Hata hivyo, akifafanua suala hilo, Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa alisema: “Mwaka jana tulipokea barua ya Fifa ikitutaka kuwasimamisha waamuzi hao na kwamba wapo kwenye uchunguzi, sasa huo uchunguzi hatutajua unahusisha mechi za ndani au za nje za kimataifa au zote kwa pamoja.
“Sisi (TFF) tumewaandalia sehemu maalumu watakayofanyia shughuli yao, lakini hakuna kiongozi yeyote anayeruhusiwa kusikiliza hadi uchunguzi wao utakapokamilika, ndiyo watatuletea,” alieleza Mwesigwa

Post a Comment

Previous Post Next Post