Dar es Salaam. Kama ulidhani Frank alichukulia
poa baada ya kuharibiwa safari yake ya kwenda kuigiza filamu jijini
London, Uingereza mwaka jana, basi tambua kwamba alikuwa na nyongo
ambayo mwaka huu ameamua kuitema.
Akizungumza na Mwananchi, muigizaji huyo ambaye
jina lake halisi ni Mohamed Mwikongi, alisema suala hilo lilimfanya
ajisikie vibaya sambamba na kumjengea picha mbaya na hasa katika umoja
uliokuwepo katika klabu ya Bongo Movie na aliyemfanyia hayo alikuwa
mmoja wa wanachama.
“Bongo Movie tuko vizuri, sitaki kujilinganisha na
Bongo Fleva, ishu ndogo tu ya kutokujitambua ndiyo inaharibu. Chembe
chembe za ubinafsi ndiyo zilizotawala, zinashindwa kutuweka pamoja,
yamesalia majungu basi,” alianza kwa kusema mwigizaji huyo aliyedumu
kwenye tasnia kwa miaka 15 sasa. Alisema baada ya kupata taarifa kuhusu
safari yake, alijipanga na kufurahia sana, lakini alishtushwa na
kukatika kwa mawasiliano baina yake na kampuni ya Didas Entertainment
ambayo alifanya nayo makubaliano.
“Kuhusiana na ile safari yangu ya London,
nilifurahi sana kupata nafasi hiyo kwa sababu sikuwahi kufika nilikuwa
naisikia tu, sasa unapoona mtu anaingia katikati mazingira yanakuwa ni
tofauti kidogo katika mambo binafsi ambayo mimi nashindwa kuelewa,”
alisema na kuongeza:
“Sisi wasanii upande wa wasambazaji wanatugawa na
sisi wenyewe tunajigawa, ukija upande wa serikali imetugawa, wananchi
nao wanatugawa kutokana na sisi kutokuwa na msimamo hasa wa kimaendeleo
ya kisanaa.”
Frank anasema katika suala kama hilo msanii
anapopata kazi, halafu mwingine anamharibia ni tatizo kubwa sana ambalo
hurudisha nyuma maendeleo ya mtu binafsi.
“Mtu anaposema huyu hafai, mimi ndiyo nafaa tayari
hilo ni tatizo. Ina maana sisi wenyewe tumejigawa, kwa hiyo wasanii
hatuna msimamo, mtazamo, mshikamano na umoja ila tumejawa na unafiki
ambao umetutawala na ndiyo ambao tunaona ndiyo sehemu ya maisha, lakini
unaturudisha nyuma” alisema na kuongeza;
“leo hii mimi hata kama nikipata nyumba nikichukua
mkopo benki, ikija kunifuata kwa ajili ya marejesho kama sina
nikanyang’anywa nyumba wasanii watanicheka na siyo kushikamana na
kukusaidia kuikomboa ile nyumba.”
Frank alisema klabu ya Bongo movie bado ina
matatizo ambayo yanahitaji kupata kiongozi mzuri wa kuyatatua, lakini
kwa sasa haina kiongozi waliokuwapo walijiuzulu.
“Ili tuweze kukaa kwenye mstari unaonyooka katika
hali hii inatakiwa wasanii tuwe pamoja, katika suala la kimtazamo,
kujitambua na kisheria ili kujifahamu wapi tunakwenda na tunafikia kwa
kiasi gani maendeleo ambayo tunakuwa nayo, tukishayakamata hayo nina
imani kwamba kila mmoja anaweza kuwa na haki katika upande wake na
nafasi ya kumwambia mwenzake wapi tumekosea na tukaweza kusaidiana,”
alisema Frank. Mwezi Aprili mwaka jana mwigizaji Issa Musa “Cloud 112”
alidaiwa kumfanyia fitina na majungu Frank katika kazi ya kwenda kuigiza
filamu nchini Uingereza na badala yake alikwenda yeye.
Kampuni iliyoandaa filamu hiyo Didas
Entertainment, iliweka ushahidi wote hadharani Oktoba mwaka jana,
ikiwamo vielelezo vya ujumbe uliotumwa na Cloud 112 zilizokuwa
zikimwelezea Frank kama msanii asiyefaa kupata nafasi hiyo.
Licha ya vielelezo hivyo, Cloud 112 mpaka sasa bado anakana tuhuma hizo na kudai kwamba makubaliano yake yaliyokuwa ni tofauti.
Post a Comment