Dar es Salaam. Habari kuwa Kamati Kuu ya CCM
inayokutana Zanzibar kesho itajadili hatima ya vigogo sita wa chama
hicho waliopewa onyo kwa kuanza kampeni za urais mapema, zimezidi
kuyaweka makundi ya vigogo hao njiapanda.
Pamoja na ajenda nyingine, jambo kubwa
linalozisumbua kambi hizo ambalo lilizifanya zipige simu jana chumba cha
habari cha gazeti hili, ni kutaka kujua ni suala gani litajadiliwa,
wagombea gani watajadiliwa na uwezekano wa ama kufutiwa onyo
lililotolewa Februari mwaka jana au kuongezewa adhabu.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kikao cha
Sekretarieti ya chama hicho iliyokutana juzi Dar es Salaam, ilisema
suala hilo halitakuwa moja ya ajenda za mkutano huo wa kesho, licha ya
Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana kueleza akiwa Tanga kuwa moja ya
ajenda itakuwa suala la maadili.
Miongoni mwa ajenda zinazotajwa ni ya uchaguzi wa
Serikali za Mitaa uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana, kalenda ya chama
kwa mwaka huu na sherehe za miaka 38 ya CCM zinazotarajiwa kufanyika
Songea mkoani Ruvuma.
Vyanzo vingine vya habari vimeeleza kuwapo pia kwa
ajenda ya hali ya siasa inayohusishwa na harakati za urais, hususan kwa
vigogo wanaopishana kusaka nafasi hiyo na wale waliotajwa katika kashfa
ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kamati Kuu inatarajia kutumia vikao hivyo
kuangalia namna ya kupata wagombea watakaokubalika kwa wananchi kuelekea
kwenye kinyang’anyiro cha urais, wabunge na madiwani.
Akiwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa
kuipa CCM ushindi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Tanga,
Kinana alisema chama hicho kitafanya kikao hicho kwa lengo pia la
kupitia masuala mbalimbali yanayokihusu.
Alisema salamu za CCM kwa Watanzania kwa mwaka huu
ni ahadi ya kuweka mkazo katika maadili kwa viongozi wake na itafanya
tathimini kwa lengo la kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu.
Alipoulizwa kuhusu ajenda katika vikao hivyo wiki
iliyopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikuja juu
na kusema hakuna kitu kama hicho. “Hata mkiiandika vibaya CCM itashinda
tu,” alisema hivi karibuni.
Vigogo waliopewa onyo na CCM ni pamoja na Naibu
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na
mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Steven Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini
ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na waziri waliokumbwa na
kashfa ya escrow ni Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo
Post a Comment