Kamati Kuu yayaweka njiapanda makundi CCM

Dar es Salaam. Habari kuwa Kamati Kuu ya CCM inayokutana Zanzibar kesho itajadili hatima ya vigogo sita wa chama hicho waliopewa onyo kwa kuanza kampeni za urais mapema, zimezidi kuyaweka makundi ya vigogo hao njiapanda.

Pamoja na ajenda nyingine, jambo kubwa linalozisumbua kambi hizo ambalo lilizifanya zipige simu jana chumba cha habari cha gazeti hili, ni kutaka kujua ni suala gani litajadiliwa, wagombea gani watajadiliwa na uwezekano wa ama kufutiwa onyo lililotolewa Februari mwaka jana au kuongezewa adhabu.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya kikao cha Sekretarieti ya chama hicho iliyokutana juzi Dar es Salaam, ilisema suala hilo halitakuwa moja ya ajenda za mkutano huo wa kesho, licha ya Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana kueleza akiwa Tanga kuwa moja ya ajenda itakuwa suala la maadili.

Miongoni mwa ajenda zinazotajwa ni ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliomalizika mwishoni mwa mwaka jana, kalenda ya chama kwa mwaka huu na sherehe za miaka 38 ya CCM zinazotarajiwa kufanyika Songea mkoani Ruvuma.

Vyanzo vingine vya habari vimeeleza kuwapo pia kwa ajenda ya hali ya siasa inayohusishwa na harakati za urais, hususan kwa vigogo wanaopishana kusaka nafasi hiyo na wale waliotajwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.

Kamati Kuu inatarajia kutumia vikao hivyo kuangalia namna ya kupata wagombea watakaokubalika kwa wananchi kuelekea kwenye kinyang’anyiro cha urais, wabunge na madiwani.

Akiwa katika ziara ya kuwashukuru wananchi kwa kuipa CCM ushindi kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Tanga, Kinana alisema chama hicho kitafanya kikao hicho kwa lengo pia la kupitia masuala mbalimbali yanayokihusu.

Alisema salamu za CCM kwa Watanzania kwa mwaka huu ni ahadi ya kuweka mkazo katika maadili kwa viongozi wake na itafanya tathimini kwa lengo la kujipanga kwa Uchaguzi Mkuu.

Alipoulizwa kuhusu ajenda katika vikao hivyo wiki iliyopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikuja juu na kusema hakuna kitu kama hicho. “Hata mkiiandika vibaya CCM itashinda tu,” alisema hivi karibuni.

Vigogo waliopewa onyo na CCM ni pamoja na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye.
Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wasira na aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na waziri waliokumbwa na kashfa ya escrow ni Profesa Anna Tibaijuka na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo

Post a Comment

أحدث أقدم