Zanzibar. Mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi
(pichani) ameshangazwa na madai kuwa amechelewa kujiunga na timu hiyo
wakati uongozi wake haukumwambia muda anaotakiwa kurudi.
Okwi alisema aliomba likizo ili kukamilisha
masuala yake ya kifamilia na uongozi wa Simba ulimruhusu na wakati
anaondoka hakuambiwa anatakiwa kurudi lini kujiunga na timu yake.
“Sikupewa muda wa kurudi, nashangaa watu
wanavyosema nimechelewa kurudi, ni kweli niliomba kupumzika mara baada
ya kusaini mkataba na uongozi ukaniambia sawa,” alisema Okwi.
“Nafurahi kuwa hapa tena na wenzangu kwa sasa nipo
tayari kuanza kazi ya kuisaidia timu yangu kwa nguvu, mwili wangu
umepumzika sasa nataka kucheza.
Kocha wa Simba, Goran Kopunovic alisema alikutana
na uongozi wa klabu hiyo na kumtaka kuwa mpole kidogo kwa kuchelewa kwa
Okwi kutokana na wao kujichanganya na kumpa likizo hiyo.
“Nimekutana na uongozi wa juu wameniambia kwamba
natakiwa kupunguza jazba kwa kuchelewa kwa Okwi, wameniambia kwamba
nimvumilie kidogo atakuja,” alisema Mserbia huyo ambaye alitoa saa 24
kwa Mganda huyo kujiunga na kambi yake.
“Huu ni uamuzi uliochukuliwa huko nyuma, lakini
namtaka atambue kwamba umuhimu wake utatoka katika maeneo, mawili
kuifungia Simba au kutengeneza nafasi za mabao.” Awali, Makamu wa Rais
wa Simba Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alimsema kutokuwapo kwa Okwi katika
timu hiyo kunatokana na ruhusa maalumu aliyopewa ya kwenda kumalizia
taratibu za ndoa yake aliyoifunga wiki mbili zilizopita.
“Tuna taarifa kamili juu ya kutokuwapo kwa Okwi,
aliutaarifu uongozi kwamba anakwenda kumalizia taratibu nyingine za ndoa
yake ambazo huko nyuma alizikatisha.” Simba kesho itashuka uwanjani
kuikabili Mtibwa Sugar katika fainali ya Kombe la Mapinduzi
itakayofanyika kwenye Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
إرسال تعليق