Goran kupimwa miezi 6 Simba

Kocha wa Simba, Goran Kopunovic (Kulia) akifurahia jambo na msaidizi wake Selemani Matola wakati wa mazoezi ya timu yao kwenya uwanja wa Fuoni, zanzibar mwishini mwa wiki.
Rais wa Simba, Evans Aveva amesema hamna ukweli kuhusu uvumi kwamba Simba imempa dola 60,000 (Sh. milioni 105) kocha Mserbia Goran Kopunovic kama ada ya kusaini mkataba wa kuifundisha klabu hiyo ya Msimbazi akisema hawawezi kumpa kiasi kikubwa hivyo cha pesa.
Aveva pia alikanusha uvumi kwamba wanamlipa kocha huyo mshahara mdogo kulinganisha na kocha aliyetimuliwa Patrick Phiri.

Uvumi ulidai kwamba Kopunovic analipwa mshahara wa dola 3,000 (Sh. milioni 5.3) jambo ambalo Aveva amelikanusha lakini hakukataa kwamba wanamlipa Mserbia huyo mshahara wa dola 5,000 (Sh.8.7) kwa mwezi.

Phiri alisaini kwa dola 25,000 (Sh. milioni 43.7) na mshahara wake ulikuwa wa dola 5,000 (Sh. milioni 8.7) kwa mwezi.

Goran mwenyewe alikataa kutaja mshahara wake wala ada ya usajili aliyopokea, lakini alisema ripoti za vyombo vya habari kwamba amesaini mwaka mmoja si za kweli bali amesaini miezi sita.

"Tumekubaliana na Simba nisaini mkataba huo mfupi ili waniangalie kwanza kabla ya kusaini mkataba mrefu zaidi," alisema Goran jana mjini Zanzibar.

Muda mfupi baada ya kufungwa bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar katika mechi yao ya raundi ya nane ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Desemba 26, uongozi wa Simba uliamua kumtupia virago Phiri kabla ya kumpa mkataba wa miezi sita Goran aliousaini siku ya Mwaka Mpya.

Mserbia huyo anakuwa kocha wa saba kuinoa klabu hiyo ya Msimbazi ndani ya miaka minne tangu 2012 ikianza na Mganda Mosses Basena, Mserbia Milovan Cirkovick (2012), Mfaransa Patrick Liewig (2013), mzawa Abdallah 'King' Kibadeni (2013), Mcroatia Zdravko Logarusic (2014), Phiri (2014) na Goran mwenyewe (2015).

Goran pia anakuwa kocha wa 19 kuinoa Simba ndani ya miaka 16 tangu 1998 vurugu za kutimua ovyo makocha zilipoanza Msimbazi, ikiwa ni wastani wa kocha mmoja kwa mwaka.

Orodha hiyo inawahusisha Goran menyewe, Phiri (2014), Loga (2013), Liewig (2013), Cirkovick (2012), Basena (2012), Mbulgaria Krasmir Benziski (2011), Phiri (2010), Cirkovick (2009), Talib Hilal (2007), Mbrazil Neider dos Santos (2006), Phiri (2005), Mkenya James Siang’a (2001- 2004), Syllersaid Mziray (2000), Kibadeni (2000), Mrundi Nzoyisaba Tauzany (1999-2000), David Mwamwaja (1999) na Mohamed Kajole (1998).

HASARA KUTIMUA MAKOCHA
Simba imekuwa ikitumia mamilioni ya shilingi kulipa mishahara na fidia ya kuvunja mikataba ya makocha, hasa wa kigeni huku klabu hiyo ikishindwa kujenga hata uwanja wa mazoezi wa timu yake.

Mfaransa Liewig alikuwa analipwa na Simba mshahara Sh. milioni sita kwa mwezi, alipewa gari ya kutembelea, posho ya simu na alikuwa anaishi hotelini huku akitafutiwa nyumba ya kuishi, ingawa hilo halikutimia kwa sababu aliondolewa mapema.

Hivi karibuni kocha aliyewahi kuinoa klabu hiyo, Cirkovic alirejea nchini akidai stahiki zake Simba dola 32,000 (Sh. milioni 56) ambazo Simba alidai ilikuwa inampiga danadana kumlipa.

Hali hiyo pia aliwahi kukutana nayo Mganda Basena ambaye alirudi kwa mara ya pili kuinoa Simba. Basena alivutana kwa kipindi kirefu na klabu hiyo 2011 akidai kiasi cha Sh. milioni 99 kama mshahara wake baada ya mkataba wake kukatishwa.

Post a Comment

أحدث أقدم