Wachezaji wa Simba wakimpongeza Ibrahim Haji 'Mido' (wa pili kulia aliyepiga magoti) kufuatia kupiha 'Hat-trick'
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
WEKUNDU
wa Msimbazi Simba wametinga kwa kishindo hatua ya nusu fainali ya kombe
la Mapinduzi 2015 kufuatia ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Taifa ya
Jang’ombe uwanja wa Amaan Zanzibar jana usiku .
Ibrahim
Hajib alifunga mabao matatu ‘hat-trick’ katika dakika ya 46, 62 na 75,
wakati bao la nne limefungwa na Shaban Kisiga katika dakika ya 80.
Mapema
kipindi cha kwanza Simba walianza kucheza mpira wa polepole wakigongeana
pasi za uhakika na kufika eneo la hatari la wapinzani wao, lakini
Maguli na Sserunukama walishindwa kujipanga vizuri na kupoteza nafasi
nzuri za kufunga magoli.
Kiungo wa
ulinzi, Jonas Mkude alipiga pasi rahisi na fupi fupi kwa viungo
washambuliaji wa Simba na mawinga wa pembeni na kuwafanya Simba wasogee
zaidi eneo la hatari wapinzani.
Mabeki wa
pembeni, Mohammed Hussein (kushoto) na Hassan Ramadhan Kessy (kulia)
walipandisha timu na kupiga krosi, lakini bado washambuliaji wa kati
hawakuwa na mipango mizuri.
Simba walitengeneza nafasi nyingi, lakini walikuwa na tatizo la umaliziaji.
Maguli
alionekana kucheza chini ya kiwango, akishindwa kumiliki mpira vizuri na
kupiga mashuti, lakini kocha Kopunovic aliendelea kumwacha mpaka
kipindi cha kwanza kinamalizika.
Hata
hivyo, Simba walijitahidi kupiga mashuti yaliyolenga lango na mpaka
kipindi cha kwanza kinamalizika walikuwa wamepiga mashuti matano dhidi
ya mawili ya wapinzani wao.
Katika kipindi hicho cha kwanza, Simba walimiliki mpira kwa asilimia 57 dhidi ya 43 za Taifa ya Jang’ombe.
Katika kipindi cha pili, Simba walianza kwa kushambulia lango la Taifa wakitafuta bao la kuongoza.
Mapema
dakika ya 46, Simba waliandika bao la kuongoza kupitia kwa Ibrahim Ajibu
kufuatia kuukuta mpira eneo la hatari baada ya purukushani ya mabeki wa
Taifa ya Jang’ombe na Danny Sserunkuma ambapo alipiga shuti lililozama
nyavuni.
Purukushani
hiyo ilitokana na pasi iliyopigwa na Kessy kwa Saimon Sserunkuma
aliyempatia pasi ndugu yake Danny ambaye alipambana na mabeki wa Taifa
na mpira kumkuta Ajibu akiwa eneo zuri.
Dakika ya
62 almanusura aandike bao la pili akijaribu kumalizia krosi ya Simon,
lakini mlinda lango wa Taifa, Karim Musa aliokoa na kuwa kona.
Katika dakika hiyo hiyo, Ajibu aliandika bao la pili kwa shuti akimalizia mpira wa kona uliochongwa na Simon.
Dakika ya
73 Ajibu alimpiga chenga Hassan Soud eneo la hatari akielekea kufunga,
lakini Abdallah Haji akamuangusha na mwamuzi akaamuru mkwaju wa penalty.
Akiwa
tayari ana mabao mawili, Ajibu alikwenda kupiga mkwaju huo wa penalti
katika Dakika ya 75 na kufanikiwa kufunga bao safi na kuandika
‘hat-trick’ ya pili katika mashindano hayo baada ya ile ya Saimon Msuva.
Msuva alifunga mabao matatu peke yake katika mechi ya ufunguzi ya kundi A Yanga ikishinda mabao 4-0 dhidi ya Taifa Jang’ombe.
Dakika ya
80, Shaaban Kisiga aliifungia Simba bao la nne kwa mpira wa adhabu
ndogo baada ya Mohammed Hussein kufanyiwa madhambi.
Mechi nyingine tatu za robo fainali zinatarajiwa kupigwa leo katika uwanja wa Amaan Zanzibar.
Mechi ya mapema inaanza saa 9:00 alasiri ambapo KCC watachuana na Polisi Zanzibar.
Azam fc wanashuka dimbani majira ya saa 11:00 jioni kucheza robo fainali ya tatu katika uwanja wa Amaan dhidi ya Mtibwa Sugar.
Mechi ya mwisho inapigwa majira ya 2:15 usiku ambapo Yanga wataoneshana kazi na JKU ya Zanzibar
إرسال تعليق