HAKUNA ADHABU NYINGINE ZAIDI YA KUMKATALIA FARAGHA?


Nisiku nyingine nzuri ya Ijumaa tunapokutana kwenye zulia zuri la mahaba, tukijuzana, kubadilishana mawazo na kuelimishana mambo mbalimbali yahusuyo uhusiano wa kimapenzi.

Ni matumaini yangu kwamba kwa uwezo wa Mungu uko poa kabisa, leo nataka tujadiliane kuhusu mada hii nyeti na muhimu kama inavyojieleza; hakuna adhabu nyingine ya kumpa mwenzi wako anapokukosea zaidi ya kumkatalia kuwa naye faragha?

Nimesukumwa kuandika mada hii baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa msomaji wangu aliyeomba hifadhi ya jina lake, ambaye alikuwa akilalamika kwamba kwa muda mrefu, mkewe amekuwa na kawaida ya kutumia tendo la ndoa kama silaha yake anapokosewa na mwenzi wake.



Kwamba ukimkosea hata kwa jambo dogo, basi anaweza kununa hata mwezi mzima na katika kipindi chote anachonuna, hataki kumpa haki yake ya ndoa mpaka atakapoamua mwenyewe.

Akaendelea kunieleza kwamba kutokana na tabia hiyo, amefikia hatua ya kutafuta mchepuko ambao huwa unamliwaza kipindi mkewe anapoamua kumuadhibu kwa kumnyima haki yake ya ndoa.

Huyu ni mmoja kati ya wanaume wengi ambao wamegeuka kuwa wahanga wa ndoa zao wenyewe, kwa wenzi wao kukataa kuwa nao faragha inapotokea wamegombana au kupishana kauli ndani ya nyumba.
Kama ambavyo nimekuwa nikisema mara kwa mara, mapenzi ni sanaa kama zilivyo sanaa nyingine na huwezi kuwa bora katika mahusiano kama hujifunzi mambo mapya na kuyaelewa kwa kina.

Katika utafiti mwepesi nilioufanya, nimegundua kuwa hata wanawake wa zamani, walikuwa wakitumia silaha hii ili kuwaweka sawa wenzi wao na kuwafanya waone umuhimu wa kuwa na mke.

Kwamba kama mwanaume amefanya kosa ambalo limemkasirisha mwanamke na hana namna nyingine ya kumfikishia ujumbe, basi njia nyepesi ni kukataa kuwa naye faragha. Kwa sababu wanaume wengi wana udhaifu katika suala hili, inakuwa rahisi kwao kushuka chini, kuzungumza kwa upole na unyenyekevu ili kutafuta suluhu na hatimaye mambo yaendelee kuwa mazuri kama ilivyokuwa mwanzo. Kama nitakuwa nimekosea, wanawake watu wazima mnaweza kunirekebisha kwa manufaa ya wasomaji wangu.

Hata hivyo, hali imekuwa tofauti kwa wanawake wa kizazi cha sasa ambapo hawaitumii silaha hiyo inavyotakiwa, badala yake wanaona ndiyo njia nyepesi ya kuwakomoa wenzi wao na siyo njia ya kufikisha tena ujumbe kama walivyokuwa wakifanya wanawake wa zamani.

Matokeo yake, wanaume nao kwa sababu wanaona wanaonewa, wanaamua kutafuta njia mbadala; kwamba kwa sababu wewe umeamua kumkomoa mwenzi wako kwa kukataa kuwa naye faragha kwa muda mrefu mpaka utakapoamua mwenyewe, naye anatafuta wa pembeni wa kumpoza mtima wake.

Mkirudi ndani, kila mmoja analala mzungu wa nne, wakati wewe ukifikiri umemkomoa kwa ‘kumlaza njaa’, mwenzako anatumia muda mrefu kutafakari mapenzi aliyopewa na mchepuko wake. Taratibu anaanza kuhamisha mapenzi kutoka kwako kwenda kwa mwizi wako na mwisho ananogewa.

Muda ambao wewe unataka suluhu, yeye tayari ameshazama kwenye dimbwi la mahaba ya mchepuko. Kutakuwa na ndoa tena hapo? Kutakuwa na amani tena hapo? Akili za kuambiwa changanya na zako.
Watafiti wa saikolojia ya mapenzi, wanaeleza kwamba hakuna njia inayoweza kuwaunganisha wawili wapendanao, hata kama walikuwa wamegombana kiasi gani, kama tendo la ndoa linalofanyika kwa ukamilifu.

Wewe unasemaje kuhusu hili? Ni sawa kumbania mwenzako kwa kipindi kirefu kwa sababu tu amekuudhi? Kuwa huru kutuma mawazo yako kupitia namba zilizopo hapo juu. Tukutane wiki ijayo tutakapoendelea kuijadili mada hii. Tchao!

Post a Comment

Previous Post Next Post