Ulaji unavyopandisha,kushusha sukari katika damu

Tukila vyakula vya wanga kama vile wali, ugali, mikate, ndizi, mihogo, viazi, chapati, vitumbua na maandazi mwili hupata sukari ambayo bila ya kuwapo mtu atakufa.

Ili mtu aweze kufikiri vizuri, kupumua, kulima, kubeba mizigo, kutembea, kusoma, kutazama, kusikiliza, dawa alizokunywa kufanya kazi, lazima mwili wake upate nishati ya kutosha kutoka katika vyakula anavyokula.

Vilevile, nishati inahitajika kwa mjamzito au mtoto aliyezaliwa ili aweze kukua vizuri.

Vyakula vya mafuta na sukari kama soda, keki na asali, ingawa navyo vinaupa mwili nishati, vitumike kwa kiasi kidogo ili kuepusha maradhi mbalimbali.

Mtu kuwa na kiwango kinachotakiwa cha sukari mwilini ni muhimu sana ili kudhibiti uzito na unene kupita kiasi na magonjwa sugu kama vile kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na saratani. Kama mtu kiwango chake cha sukari kinapanda mara kwa mara, yupo katika hatari ya kupata magonjwa mengi na hivyo kuwa katika hatari ya kufa.

Mtu mwenye kiwango cha kupanda sukari cha kudumu anashauriwa akamwone daktari wake au mtaalamu wa vyakula ampe nasaha za jumla kuhusu ulaji unaomfaa. Zaidi ya hayo, mtu huyo atashauriwa namna ya kubadili mtindo wake wa maisha kama vile kufanya mazoezi bila ya kukoma, kuacha kuvuta sigara na kuacha kunywa pombe.

Lazima tujenge tabia ya kwenda hospitali kupima afya zetu ikiwamo kupima urefu, uzito, wingi wa sukari na mafuta mwilini.

Kupunguza ulaji kwa wingi wa vyakula vya wanga na mafuta, kunaweza kusaidia kushusha kiwango cha sukari mwilini, hasa kwa watu wasiofanya mazoezi au kazi za kutoka jasho.

Ulaji unaofaa wa vyakula vya wanga pia, unaweza kulikabili tatizo la mtu kushuka kiwango cha sukari kuliko inavyotakiwa kiafya baada ya mtu kula.

Dalili za mtu kupungukiwa sukari katika damu ni pamoja kuwa na ganzi, kuwa na wasiwasi, kutetemeka, kusikia njaa na kuchanganyikiwa.

Mtu akinywa vinywaji vyenye kafeini kama vile chai au kahawa au akiwa na msongo wa mawazo, tatizo lake la kushuka sukari linakuwa kubwa zaidi.

Moja ya sababu ya kushuka sukari mara baada ya mtu kula chakula ni mtu kula vyakula vyenye wanga vinavyofyonzwa kwa haraka tumboni.
- Mwananchi

Post a Comment

Previous Post Next Post