Hali tete bomba la gesi Mtwara

*Zabaki mita nne lisombwe na maji, jeshi latuma magari 30
*Vitendea kazi vyapungua, wananchi waombwa kusaidia
Sijawa Omary, Mtwara
BOMBA la gesi lililopo mkoani Mtwara lipo hatarini kusombwa na maji kutokana na mmomonyoko wa ardhi uliotokea eneo la kiwanda cha kuchakata gesi mkoani hapa.
Kutokana na hali hiyo, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limetumwa magari 30 mkoani humo ili kurahisisha kazi ya kudhibiti mmomonyoko huo ambao unatishia uhai wa bomba hilo.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya kuwepo uhaba wa vitendea kazi hali inayosababisha shughuli ya kudhibiti ardhi inayomomonyoka kuwa ngumu.
Mkuu wa Brigedia katika mikoa yote ya kusini, John Chacha alitoa kauli hiyo jana wakati akizumngumza na waandishi wa habari hatua iliyofikiwa katika kudhibiti mmomonyoko huo.
Alisema tatizo linalowakabili ni la vitendea kazi ikiwemo makoleo, sepetu na zilizopo ni 15, magari makubwa ya kusomba mawe kutoka eneo la Msijute ikiwa ni kilomita 80 kutoka eneo la tukio.
Mkuu huyo alisema tatizo hilo wamelifikisha makao makuu ya jeshi pamoja na Wizara ya Ulinzi na Usalama ambapo magari 30 ya jeshi yapo njiani kwenda eneo. Alisema kulikuwa pia na tatizo la mafuta, lakini tayari wamepatiwa lita 10,000.
“Zimebakia mita 4 tu maji kufika katika eneo la bomba na kuweza kuling’oa na kazi iliyofanyika ni mzuri na hadi hivi sasa tayari mita 150 kutoka eneo lililokuwa msitu zimeondoka,” alisema.
Hata hivyo, alisema magari yanayotarajiwa kuwasili yatasaidia na mambo yanaweza kwenda vizuri, huku akiomba wananchi wajitokeze kutoa msaada.
“Siku zijazo itabidi pajengwe kitu cha kudumu kama vile ukuta ambao utasaidia kuzuia ili isiweze kutokea tena, kwa hiyo tatizo linalotukwamisha ni vitendea kazi na hii inakuwa ni tatizo,” alisema Chacha.
Alisema tatizo si askari kwani wapo wa kutosha. Chacha alisema jumla ya askari waliopo ni 192 wakiwemo wa JWTZ 150, polisi 23 na magereza 13 na kuongeza kuwa tatizo ni vitendea kazi.
Bakwata
Wakati huo huo, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) Mkoa wa Mtwara limeomba dua kutokana na athari iliyotokea hivi karibuni katika Kijiji cha Msimbati kutokana na maji ya bahari kumega eneo la ardhi kwenye kiwanda cha kuchakata gesi.
Tukio hilo lilitokea jana wakati baraza hilo kufiki katika eneo la tukio kwa lengo la kujionea athari hiyo kisha kuomba dua kwa kuitaka jamii kwa jumla kuwa na subira na kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kilichotokea kwani ni mipango ya Mungu.
Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Nurdini Mangochi katika dua yake alisema waumini popote pale huwa wanasubiri wakati wanapopata majanga na kusema ndiyo kazi ya Mungu.
“Kwani jambo la kushuka kwa ardhi ni jambo kubwa sana ila cha msingi ni kuwa na subira na kushukuru kwani kila jambo linatakiwa kuwa na subira,” alisema Mangochi.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendegu alisema wanaendelea kazi na kushukuru kampuni zilizojitolea kutoa vitendea kazi kama malori, ikiwemo Kampuni ya Dangote na kwamba mchango wa wananchi unahitajika.

Post a Comment

أحدث أقدم