Dar es Salaam. Zikiwa zimebaki siku tatu kabla ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano kuanza mjini Dodoma, sasa hakuna shaka kwamba Rais
Jakaya Kikwete atafanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri wakati
wowote kuanzia leo na kabla ya Jumapili (saa 48) kutokana na kukabiliwa
na safari ya nje.
Rais anatarajiwa kufanya mabadiliko hayo baada ya
kumwondoa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kwa kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji fedha kwenye
Akaunti ya Tegeta Escrow baada ya kuingiziwa Sh1.6 bilioni kwenye
akaunti yake.
Mwingine ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, ambaye anatuhumiwa kutoshughulikia kwa makini sakata
hilo na kusababisha Serikali kupoteza fedha hivyo kuwapo kwa uwezekano
mkubwa wa kumvua uwaziri utakaomlazimu Rais kufanya mabadiliko madogo
kwenye baraza lake, ikiwa ni miezi isiyozidi mitano kabla ya kuvunja
Bunge kupisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Habari ambazo Mwananchi imezipata zinaeleza kuwa Rais Kikwete anaweza kutangaza mabadiliko hayo wakati wowote kuanzia leo.
“Rais anaondoka Jumapili kwenda Davos (Uswisi
kuhudhuria mkutano wa Jukwaa la Kiuchumi la Dunia (WEF)), hivyo kwa
jinsi yoyote ile ni lazima atangaze baraza kesho (leo) au Jumamosi,”
alisema mpashaji habari wetu.
“Hawezi kutangaza baraza jipya akiwa nje ya nchi,
hivyo ni lazima atangaze kesho (leo) au ikishindikana Jumamosi ili
Jumapili afanye shughuli nyingine na kuondoka.”
Hata hivyo, mabadiliko ya mwisho ya Baraza la
Mawaziri yalitangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue ambaye pia
anaweza kupewa kazi hiyo.
Baada ya kujadili sakata la uchotwaji wa fedha
hizo kwa takriban siku nne, Novemba 28, mwaka jana Bunge lilifikia
maazimio manane, likiwamo la kutaka wote waliohusika kwenye kashfa hiyo
wachukuliwe hatua na mamlaka husika, akiwamo Profesa Muhongo ambaye Rais
Kikwete alisema Novemba 22, 2014 kuwa amemuweka kiporo hadi baada ya
“siku mbili au tatu” kusubiri matokeo ya uchunguzi.
Hata hivyo, shinikizo liliongezeka baada ya Kamati
Kuu ya CCM, iliyokutana Zanzibar chini ya uenyekiti wa Rais Kikwete,
kuitaka Serikali iwe imetekeleza kwa vitendo maazimio yote ya Bunge
kuhusu sakata hilo kabla ya kikao cha Bunge kitakachoanza Jumanne ijayo
na kutaka wahusika walioko kwenye dhamana za uteuzi wachukuliwe hatua
stahili na mamlaka zao kuwawajibisha mara moja.
Pia, Kamati ya Maadili ya CCM iliyokutana Dar es
Salaam mapema wiki hii, iliwajadili wanachama waliohusika kwenye kashfa
hiyo na kupeleka taarifa yake kwenye Kamati Kuu ya chama hicho kwa hatua
zaidi.
Wakati CCM ikisema hayo, wabunge wamekuwa
wakimkumbusha kiongozi huyo wa Serikali kuchukua hatua kabla ya kikao
cha Bunge. Wabunge wawili wa mkoani Arusha, Godbless Lema na Joshua
Nassari wote kupitia Chadema, wamediriki kusema kuwa watamwondoa Profesa
Muhongo kwa mabavu kwenye ukumbi wa chombo hicho cha kutunga sheria
iwapo Rais hatakuwa amemuondoa.
Pia, nchi wahisani zilieleza mapema mwezi huu kuwa
pamoja na kuruhusu kiasi cha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo,
bado zinasubiri tamko la Serikali kuhusu sakata hilo, ikiwa ni pamoja na
hatua ilizochukua kuzuia kashfa kama hiyo isitokee tena, ili Tanzania
inufaike kwa misaada hiyo ya fedha zinazotokana na walipakodi wa nchi
zao.

إرسال تعليق